MAMLAKA ya Mapato Kenya(KRA),inamshikilia mwandishi wa habari wa
Tanzania kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kiasi
cha kilo 5.436 zenye thamani ya karibu Sh234 milioni.
Mtanzania huyo ambaye aliwahi kuwa mtangazaji
katika kituo kimoja cha redio nchini, alikamatwa akiwa anataka
kusafirisha dawa hizo kwenda China.
“Mamlaka ya Mapato Kenya inataka kutaarifu
maendeleo ya sakata la kukamatwa kwa kilo 5.436 za heroin zilizokamatwa
Januari 23 mwaka 2013 saa 4:40 usiku.”
“Imethibitika kuwa kilichokamatwa ni dawa aina ya
heroin yenye thamani ya Sh13 milioni za Kenya…kwamba mtuhumiwa… (Jina
tunalo kwa kuwa hajafikishwa mahakamani) hakuwa mwanafunzi lakini ni
mtangazaji wa redio nchini Tanzania.”
Ametambulika kuwa mtangazaji wa kituo kimoja cha
redio kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye
thamani ya Sh234 milioni.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kenyatta akiwa katika jaribio la kuelekea nchi za Ulaya
na kwamba kukamatwa kwake kulifanikiwa kutokana na mtego ulioandaliwa
na maofisa wa usalama uwanjani hapo.
Taarifa zinasema kuwa, mtuhumiwa huyo
alijitambulisha kama mwanafunzi anayesoma Sweden, lakini hata hivyo
ilikuja kubainika kuwa alikuwa na kibali cha ukazi alichokipata Novemba
28 na kilitazamiwa kuisha muda wake Novemba 28,2014.
Naibu Kamishna wa KRA, Kenned Onyonyi alisema kuwa
maofisa wa usalama wanaendelea na uchunguzi zaidi na taarifa zaidi
zitatolewa baadaye.
Habari zinasema kuwa, mtuhumiwa huyo alikuwa na
uhusiano wa kimapenzi na raia mmoja wa Sweden, ambaye alimtambulisha kwa
maofisa usalama kwamba amekuwa akisafiri mara kwa mara katika nchi za
Ghana, Kenya na Mauritius.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, mtuhumiwa huyo
amewahi kufanya kazi na Clouds fm akiwa kama mtangazaji mwanafunzi
katika kipindi cha Leo tena na baadaye aliachana na kampuni hiyo na
kujiunga na gazeti hili akiandika habari za burudani. Aliachana na
gazeti hilo na kuendelea na maisha yake ya kawaida.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Kikosi cha
Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema kuwa
hawajapata taarifa za kukamatwa kwa Mtanzania huyo, bali wamezisoma tu
kwenye baadhi ya vyombo vya habari.
“Kuna utaratibu ambao inabidi watujulishe kwani
kuna tume ya kuratibu dawa za kulevya hivyo tunasubiri atuambie kuhusu
tukio hilo,”alisema Nzowa.
No comments:
Post a Comment