Watu
42 kwenye kaya 12 katika kitongoji cha Mji Mwema, kijiji cha Matandi,
kata ya Ndumeti, wilayani Siha hawana mahali pa kuishi kufuatia nyumba
zao kuteketea kwa moto majira ya usiku wakiwa wamelala.
Akizungumza na NIPASHE mjini hapa jana, Afisa Mtendaji wa kijiji
hicho, Valence Silayo, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 6
usiku na kuteketeza maduka 12 ambayo pia yalikuwa yanatumika kwa ajili
ya makazi na biashara na kutokana na mbinu hafifu za kuzima moto
walilazimika kubomoa vibanda vitatu kuvinusuru kuteketea.
Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mtu mmoja amejeruhiwa na amelazwa
Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.
Silayo alisema moto huo ulianzia kwenye makazi ya Rashidi Nelson,
na kwamba vibanda hivyo vya mbao vilikuwa vinatumika kwa ajili ya
biashara kwa upande wa mbele na makazi kwa upande wa nyuma.
“Hadi sasa watu hawa hawana makazi na wanahitaji msaada wa chakula
na mahali pa kuishi kwa muda, moto ulizidi na kutufanya wazimaji
kushindwa kuukabili ili kuokoa mali kutokana na upepo mkali uliokuwapo”
alisema.
Silayo alisema vibanda hivyo wamekuwa wakivitumia kama sehemu ya
biashara na makazi ya familia zao na kwamba kwa sasa wanahitaji msaada
wa haraka wa chakula na mahema na wamejihifadhi kwa ndugu na marafiki.
Mkuu wa wilaya ya Siha, Dk. Charles Mlingwa, alisema serikali
inafanya tathimini ya tukio hilo na polisi wapo eneo la tukio
wakiendelea na uchunguzi ili kujua chanzo halisi na thamani ya mali
iliyoteketea.
“Sina taarifa za watu 42 kutokuwa na makazi bali watu 12, najua
kulikuwa na vibanda vya biashara na si nyumba za kuishi, wenye maduka
walikuwa na makazi katika eneo jingine, hivyo hakuna watu wa kupatiwa
msaada wa makazi” alisema Dk. Mlingwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo.
Hata hivyo, kumekuwapo na taarifa za kukanganya juu ya tukio hilo,
huku uongozi wa kijiji ukisema tukio limetokea Matandu kata ya Ndumeti
na taarifa ya polisi ikisema kijiji cha Ngaranairobi na Mkuu wa wilaya
akisema ilikuwa ni vibanda vya biashara na si makazi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment