Thursday, February 28, 2013

MAPYA YAIBUKA SAKATA LA MTUHUMIWA WA MAUWAJI YA MWANGOSI , WAANDISHI WATIMULIWA



Hapa mtuhumiwa  huyo akikimbiziwa mahabusu ili kukwepa picha ya  wanahabari leo
Hapa akiingizwa mahakamani leo

                                        
Huyu ndie mtuhumiwa wa mauwaji ya Daudi Mwangosi

SAKATA la mtuhumiwa  wa   mauwaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten mkoani Iringa marehemu Daudi Mwangosi askari  wa FFU mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23),limeendelea  kuchukua  sura  mpya  baada ya wanahabari  kunusurika  kichapo  kutoka kwa askari  polisi ambao  walikuwa  wakiwazuia  kusogea katika  chumba  cha mahakama  kusikiliza  kesi  hiyo .

Askari  polisi hao  wakiwa  zaidi ya  10  waliweza kutumia nguvu  za  ziada katika kuwathibiti wanahabari  wa vyombo mbali mbali  waliofika  kusikiliza na kuripoti mwenendo wa kesi hiyo  namba  1 ya mwaka 2012  ya mauwaji ya mwanahabari mwenzao ,Mwangosi  aliyeuwawa septemba 2 mwaka 2012  katika kijiji cha Nyololo wilaya ya Mufindi wakati wa polisi walipokuwa  wakitumia nguvu  kuwatawanya wafuasi wa chama  cha  Demokrasia na maendeleo  (CHADEMA)  aliokuwa katika shughuli za ufunguzi  wa matawi ya chama  hicho.

Hata  hivyo  moja kati ya mbinu  waliyopata  kuitumia  leo  wakati mtuhumiwa huyo akifikishwa mahakamani hapo ni  kuwafukuza  waandishi  wa habari  eneo hilo la mahakama na kumtoa mtuhumiwa huyo kwa  kificho cha hali ya  juu kwa  kumweka katikati ya  watuhumiwa  wa makosa mingine zaidi ya 8 huku mtuhumiwa akijificha sura  yake  kukwepa kamera za waandishi na baadhi ya askari  wakimkinga ili  kukwepa  kupigwa  picha.

Tukio  hilo  lilitokea muda wa saa 6.10 mchana  wakati mtuhumiwa  huyo askari  Saimoni alipokuwa akitolewa na  watuhumiwa  wengine  kutoka  chumba cha mahabusu ya mahakama  ya hakimu mkazi  mkoa  wa Iringa na kumpeleka katika  chumba cha mahakama ya wazi  kwa ajili ya  kesi hiyo  kutajwa tena.

Hivyo  katika hali ya  kushangaza ni pale askari  hao  kuwataka  wanahabari hao  kusongea  umbali  wa mita  710 kutoka  eneo la Mahakamani  hiyo  wakati mtuhumiwa   huyo akiingizwa katika  chumba  hicho  cha mahakama ya  wazi  mbele ya  hakimu mkazi  wa mahakama ya  mkoa  wa Iringa  Gladys Barthy  ili  kesi  hiyo  iweze  kutajwa  kwa zaidi ya mara  ya tano  sasa bila upelelezi  kukamilika.

Uamuzi  huo  wa askari  hao  kuwataka  wanahabari  hao  kusimama  umbali  wa mita 710 kutoka chumba  cha mahakama  ulionyesha kuwashangaza  hata  baadhi ya  wananchi  waliofika  kusikiliza  kesi na kuwawekea  dhamana  ndugu  zao  na kulazimika  kuungana na  wanahabari  kupinga  uamuzi  huo na kupelekea  askari  hao  kuwafukuza  pia  wananchi hao na kuwataka waungane na  wanahabari kuondoka eneo hilo la  chumba  cha mahakama.

Mbali ya  wanahabari hao  kunyanyasika  wakati mtuhumiwa  huyo akipelekwa  chumba  cha mahakama  kwa ajili ya  kesi hiyo kutajwa  bado  askari  hao  kabla ya  gari la mahabusu  (karandinga)  kufika na watuhumiwa eneo hilo la mahakama  mida ya saa 5.30 asubuhi  bado askari hao  walionyesha  kuwanyanyasa  wanahabari  hao na  mara kwa mara  kuwatawanya kwa kauli nzito za maneno kuwataka  kuondoka maeneo waliyokusanyika  kwa madai  hawapaswi  kusikiliza  kesi hiyo kwani  haipo  katika mahakama ya wazi jambo ambalo  halikuwa  la kweli.

Wakizungumza  juu ya uamuzi  huo  wa askari hao  kutumia  nguvu  za ziada katika kuwathibiti  wanahabari hao  baadhi ya  wananchi  walisema  kuwa  kinachofanywa na jeshi la  polisi mkoani Iringa ni kuzidisha jazba  zaidi kwa  wananchi na kuwa  hawakupaswa  kuwazuia  wanahabari  kutimiza  wajibu  wao.

Alisema Wistone kalinga  kuwa  hata  wao  wananchi  wanashindwa kujua  sababu ya  polisi  kumficha  mtuhumiwa  huyo wakati tayari amefikishwa mahakamani na  kuwa kinachofanywa na polisi ni  kuzidi kulipaka matope  jeshi la polisi na kuondoa kabisa  dhana ya  polisi jamii na ulinzi shirikishi pia uhuru  wa vyombo  vya habari katika  kulitumikia Taifa na  wananchi  wake.

Sanjari na  wananchi hao kushangazwa na tukio  hilo la  polisi kuzuia  wanahabari  pia kwa upande  wake mahakama  hiyo ya hakimu mkazi  mkoa  wa mkoa  wa Iringa  mheshimiwa  Barthy alisema  kuwa  kitendo  kilichofanywa na polisi hao  kuwazuia  wanahabari  si maagizo ya mahakama na kuwa  wanahabari hao  walikuwa  huru  kuingia  kusikiliza  kesi hiyo na  kuhabarisha  umma kwani  hakukiwa na siri wala hakuna maagizo ya mahakama  ya kuwataka  polisi  kuwafukuza  wanahabari mahakamani hapo.

"Kwanza  nawapa pore  sana  kwa misukosuko mlioipata  ....ila  mimi nilikuwa ndani   ya  mahakamani  sikujua  kinachoendelea  huko nje  ya  mahakama ila  nawahakikishieni  kuwa  kesi  hii ilikuwa ikisikilizwa katika mahakama ya  wazi na mlikuwa  huru   kusikiliza " alisema hakimu  huyo akiakimhoji mmoja kati ya  viongozi  wa  polisi kuhusu polisi hao  kunyanyasa  wanahabari na kuwataka  kutorudia kufanya   hivyo  tena.

Mwendesha mashitaka  wa  serikali Blandina Manyanda  aliiomba mahakama  hiyo  kupanga tarehe nyingine ya  kutajwa kwa  kesi hiyo na kuwa  upelelezi  bado haujakamilika na mahakama  hiyo  kupanga tarehe  14 machi ambapo  kesi hiyo  itafikishwa mahakamani  hapo kwa ajili ya kutajwa.

No comments:

Post a Comment