WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa,
amesema kuwa iwapo serikali zote mbili; ile ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na ya Zanzibar, zitatekeleza kwa usahihi maelekezo ya mkutano
mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya suala la ajira, chama hicho
kitashinda kiurahisi katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana kuhusu
uchaguzi wa Kenya, Lowassa alisema amefurahishwa na jinsi Wakenya
walivyolichukulia tatizo la ajira kama moja ya ajenda muhimu katika
uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Alisisitiza kuwa, kama CCM nayo italichukua tatizo la ajira kwa vijana
kama moja ya ajenda yake, kitashinda kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa
urais kabisa.
“Nimefurahi wenzetu Kenya wameliona tatizo la ajira kama moja ya
ajenda muhimu katika uchaguzi wao. Nimefurahi Waziri Mkuu Odinga
alieleza jinsi serikali yao ilivyojaribu kulishughulikia suala hili,”
alisema Lowassa.
Alisema CCM imepiga hatua kubwa, kwanza kwa kukiri kwamba suala la
ajira kwa vijana ni tatizo na kutoa maelekezo kwa serikali
kulishughulikia.
“Moja ya maazimio ya mkutano mkuu wa CCM ni juu ya suala la ajira, na
katika kikao cha Halmashauri Kuu hivi karibuni, tulilijadili kwa kina
tatizo hili, na kwa kweli kama serikali zetu hizi zitatekeleza maelekezo
yake, sina shaka yoyote CCM tutashinda kiurahisi 2015,” alisema.
Lowassa ambaye amekuwa msemaji mkuu wa suala la ajira kwa vijana
akiliita kuwa “ni bomu linalosubiri kulipuka”, aliongeza kuwa uamuzi wa
vikao hivyo ukitekelezwa vizuri utaifanya CCM iingie kwenye uchaguzi
mkuu ikiwa na majibu sahihi yaliyokwishajibiwa juu ya tatizo la ajira
kwa vijana.
“CCM imeanza kulishughulikia ili tusiulizwe na vijana 2015, tuangalie
uchaguzi wa Kenya, hii ni moja ya ajenda muhimu katika kujinadi,”
alisema.
Alisema kilimo ni moja ya eneo ambalo linaweza kwa kiasi kikubwa
kutatua tatizo hilo pamoja na kwamba bado anaamini kuwa elimu ni muhimu
kabla kilimo kwanza.
Aidha, alisema viwanda vikubwa vya nguo ni eneo jingine ambalo
linaweza kwa kiasi kikubwa kusaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana.
“Hii inawezekana kabisa, viwanda vya nguo ndiyo vyenye kutoa ajira
kubwa, tusingoje mpaka vijana waje kutuuliza 2015,” alionya Lowassa
ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa watu wanaotaka kuwania urais katika
uchaguzi mkuu ujao.
Kauli hiyo ya Lowassa imekuja siku moja tu baada ya Shirika la Utafiti
la Synovate kutoa matokeo ya utafiti wake yanaoonesha kuwa chama tawala
CCM kimeongezeka umaarufu ambapo asilimia 52 ya wananchi waliohojiwa
wamesema wangependa kujiunga nacho.
Ama kwa upande wake, Lowassa kwa mujibu wa utafiti huo umaarufu wake
kuelekea 2015 umepanda kwa asilimia sita na kufikia asilimia 7 akiwa
miongoni mwa vigogo watano wa juu wanaopewa nafasi ya kushinda urais
iwapo uchaguzi ungefanyika leo.
Lowassa kwa mujibu wa utafiti huo anatanguliwa na Waziri wa Ujenzi,
John Magufuli mwenye asilimia nane, Zitto Kabwe wa CHADEMA na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda wenye asilimia tisa kila mmoja na Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa mwenye asilimia 17.
No comments:
Post a Comment