Thursday, February 7, 2013

ACHOMWA MOTO KWA MADAI YA UCHAWI


Wananchi wakishuhudia mwili wa mwanamke huyo ukiteketea kwa moto.

Mama mmoja kijana alitupwa huku akipiga mayowe kwenye matairi na kuchomwa moto akiwa hai baada ya kutuhumiwa kwa mauaji ya mtoto wa kiume wa jirani yake mwenye miaka sita kiushirikina.
 
Kepari Leniata mwenye miaka 20, 'alikiri' baada ya kuwa ameburutwa kutoka kwenye kibanda chake, kuvuliwa nguo zake zote na kubaki uchi na kuchomwa kwa nondo ya moto.
 
Kisha baadaye alikokotwa hadi kwenye dampo lenye taka mbalimbali, kuzamishwa kwenye petroli na, huku akiwa kafungwa mikono na miguu yake, akatupwa kwenye matairi yaliyokuwa yakiwaka moto. Mama huyo wa watoto wawili alipiga kelele kwa maumivu makali, matairi yaliyokolea moto wa petroli yaliporushwa juu yake.
 
Tukio hilo la kutisha lilifanyika katika kijiji cha Paiala, kwenye milima ya Papua New Guinea ambako wengi wanaamini kwamba uchawi upo na ushirikina unatumika kuwaua maadui.
 
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri lililoko katika wilaya hiyo juzi alilaani mauaji hayo.
 
"Ushirikina na mauaji yanayohusiana na uchawi yanazidi kukua na serikali inahitaji kutunga sheria kuzuia vitendo hivyo," David Piso aliliambia gazeti la The National.
 
"Wengi wasio na hatia na watu wasiojiweza wamekuwa wakiuawa na kuteswa kwa tuhuma za uchawi, lakini kukatisha uhai ni kinyume cha mafundisho ya Biblia na sheria za nchi hiyo," alisema.
 
Tukio hilo liliibuka baada ya kijana mmoja jirani wa Kepari kuugua Jumanne asubuhi. Alikuwa akilalamika maumivu ya tumbo na kifuani na alipelekwa katika hospitali ya Mt Hagen ambako alifariki masaa kadhaa baadaye.
 
Jamaa wa kijana huyo walihisi kwamba uchawi ulihusika katika kifo chake na kuelezwa kwamba kuna wanawake wawili walikuwa wamekwenda kujificha kwenye msitu mnene.
 
Baada ya kuwa wamewaona, wawili hao walikiri kujishughulisha na uchawi lakini hawahusiki na kifo cha kijana huyo. Walisema kuwa Kepari ndiye anayehusika na kifo hicho.
 
Familia ya kijana huyo walikwenda kwenye kibanda chake majira ya Saa 1 asubuhi ya Jumatano, wakamvua nguo na kumkokotea mbali ambako walimtesa na kumuua.
 
Picha za tukio hilo la kutisha baadaye zikasambazwa kwenye mtandao wa kompyuta. Gazeti la The Post Courier lilisema mateso na mauaji ya kutisha ya mama huyo wa watoto wawili 'yametoa fursa ya picha kwa wengi walioshuhudia, wakiwamo watoto wa shule, ambao walijazana kuzunguka eneo hilo na kupiga picha ya mwanamke huyo akichomwa moto huku akiwa hai.'
 
Polisi ambao alikimbilia eneo la tukio walirudishwa nyuma na umati mkubwa wa watu wenye hasira, lakini waliweza kuwatawanya.
 
Polisi wa Papua New Guinea wameanza uchunguzi wa mauaji na imeripotiwa kwamba wameandaa mashitaka kwa wote wanaohusika.
Gari la kikosi cha zimamoto ambalo liliitwa eneo la tukio lilishambuliwa na umati huo na kulazimika kuondoka.
 
Mamlaka na wanadiplomasia wa kimataifa wamezungumzia kuhusu tukio hilo la kuchomwa moto mama huyo kijana, na kuwaacha watoto wawili yatima, mdogo akiwa binti wa miezi minane.
 
Waziri Mkuu wa nchi hiyo Peter O'Neill ameapa kuwafikisha katika mikono ya sheria wauaji hao, wakati akielezea tukio hilo kwenye taarifa yake.
"Hakuna yeyote anayefanya kitendo kiovu kama hicho katika jamii ambayo sisi sote, akiwamo Kepari, anaishi," alisema.
 
"Mauaji ya kinyama yanahusishwa na tuhuma za uchawi. Ukatili dhidi ya wanawake sababu ya imani hizi ni mauaji ya kishirikina. Mauaji haya yamekuwa maarufu sana kwenye sehemu fulani za nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment