DEREVA wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika Dodoma (Coasco) (jina linahifadhiwa) (42) mkazi wa Dodoma anashikiliwa polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuusababishia ajali Msafara wa Mkuu wa Polisi Tanzania (IGP) Said Mwema.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Faustine Shilogile alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuwa tukio hilo lilitokea Januari 29, mwaka huu saa 12 jioni maeneo ya Mkundi, Manispaa ya Morogoro.
Kamanda huyo alisema msafara wa IGP ulikuwa ukitokea jijijni Dar es Salaam kuelekea Dodoma na kwamba ulipofika maeneo hayo ya Mkundi gari la polisi lenye namba za usajili PT 2574 Toyota Landacruiser lililokuwa likiendeshwa na E 3365 Koplo Emanuel Kitima (48) liligongwa na dereva huyo aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Landcruiser lililokuwa likitokea Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam.
Kamanda huyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva huyo wa Coasco kuzidi upande wa kulia zaidi huku akiwa mwendo kasi. Alisema hakuna aliyeumia katika tukio hilo na kwamba atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Wakati huohuo, watu wawili wamefariki dunia mkoani hapa kwa kuuawa na watu wasiojulikana katika matukio mawili tofauti.
Alisema tukio la kwanza lililotokea Januari 29 mwaka huu saa 8.30 mchana hukohuko Kiswago Tarafa ya Mtimbira, wilayani Ulanga ambako mwanafunzi wa kidato cha pili, Shule ya Sekondari ya Sofi, Enis Ndugalizi (21) alikutwa amekufa huku akiwa na majeraha kichwani, usoni na kitovuni.
Kamanda Shilogile alisema kuwa mwanafunzi huyo anadaiwa kutoweka nyumbani kwao tangu Januari 26, mwaka huu akielekea shambani na kwamba hakuonekana hadi Januari 29 alipokutwa akiwa amekufa.
Chanzo cha kifo hakijajulikana na kwamba inadaiwa aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo. Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi.
Katika tukio lingine, mtu mmoja Joseph Woga (29) aliuawa na watu wasiojulikana kwa tuhuma za wizi huko Chamwino Manispaa ya Morogoro.
Kamanda huyo alisema kuwa mtu huyo aliuawa Januari 29, saa 8 usiku huko Chamwino akidaiwa kuiba gunia la mkaa na kwamba hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na kifo hicho.
No comments:
Post a Comment