Saturday, December 22, 2012

LEMA ALEJEA BUNGENI ASEMA ATANYOKA NA PINDA


 Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kulia akiwa na Mnyika 
MAHAKAMA ya Rufani imemrejesha bungeni Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ikiwa ni miezi tisa tangu alipovuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Mahakama hiyo ilimrejesha Lema bungeni, baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Arusha iliyotolewa Aprili 5, mwaka huu.
Hukumu hiyo iliyosomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu imemtambua Lema kuwa mbunge halali wa Arusha Mjini na kuwaamuru wajibu rufaa kumlipa gharama za rufaa hiyo.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard Luanda kwa niaba ya wenzake wawili waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa wajibu rufani hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi.
“Rufaa imefanikiwa na tunatengua hukumu, tuzo na amri  ya Mahakama Kuu. Tunamtangaza mrufani kuwa Mbunge wa Arusha Mjini,” ilisema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo.
Uamuzi huo uliwafanya wanachama na wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika ndani ya ukumbi wa Mahakama hiyo, kulipuka kwa furaha huku wakiimba kibwagizo cha “People’s Power!” na wengine wakiongeza kwa kuimba “Lema! Lema! Lema!”
Wanachama na wafuasi hao wa Chadema walianza kusukumana kwenda kumkumbatia Lema, huku wengine wakipanda kwenye viti (mabenchi) ya mahakamani.
Tukio hilo lilisababisha taharuki kutokana na kusukumana, huku wengine wakianguka kwenye mabenchi, hali ambayo pia iliwapa wakati mgumu viongozi wa Chadema akiwamo, Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kutoka nje ya ukumbi huo.

Hoja mpya
Katika rufaa yake, Lema kupitia kwa mawakili wake, aliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, lakini katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iliibua na kutolea uamuzi hoja mpya ambayo haikuwa imetolewa na upande wowote mahakamani hapo.
Hoja hiyo ambayo iliibuka kwa mara ya kwanza kabisa siku ya kusikiliza rufaa hiyo ni kama warufani walikuwa ni wapiga kura waliojiandikisha.  
Katika uamuzi wake kuhusu hoja hiyo, Mahakama ilisema kuwa wajibu rufaa hao, hawakuwa wapiga kura kwa kuwa katika kumbukumbu za Mahakama hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa ni wapiga kura waliosajiliwa.
Mahakama ilipoibua hoja hiyo, Wakili wa warufani, Mughway alijibu kuwa wajibu rufaa hao ni wapiga kura halali waliosajiliwa na kwamba hata Mahakama ilijiridhisha kwa kuangalia kadi zao za kupigia kura.
Wakili Mughaway alidai kuwa suala hilo lilijitokeza Mahakama Kuu na wajibu rufaa hao wakawasilisha kadi zao mahakamani ambazo ilinakili majina na namba zao na kisha kuzirejesha kwa wenyewe.

No comments:

Post a Comment