ULINZI wa aina yake uliwekwa
katika mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam jana wakati
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh, Ponda Issa
Ponda alipofikishwa mahakamani hapo na watu wengine 49.
Ponda na wafuasi wake walifikishwa mahakamani hapo kusikiliza kesi inayowakabili ,wakidaiwa kufanya vurugu na kuharibu mali.
Hata
hivyo, wakati wafuasi hao wakiachiwa kwa dhamana, Mahakama hiyo ilisema
kuwa haina mamlaka ya kisheria ya kutoa dhamana kwa Sheikh Ponda
anayetuhumiwa kuchochea vurugu hizo.
Sheikh Ponda na wafuasi wake
walifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi chini ya ulinzi mkali. Katika
viwanja vya Mahakama ya Kisutu pia kulikuwa na ulinzi mkali wa vikosi
ya polisi pamoja na kuwekwa vyombo maalumu vya usalama vilivyotumika
kuwakagua watu waliokuwa wanaingia hadi Ponda alipoondolewa kurudi
rumande baada ya kesi kuahirishwa.
Mbali na wingi wa askari waliokuwa
wakilinda usalama katika eneo la mahakama hiyo wakiwa na silaha, mbwa
na farasi, pia jana kuliwekwa mashine maalumu ya ukaguzi kwa kila
aliyekuwa akiingia mahakamani hapo pamoja na kifaa cha kutambua
milipuko.
Mahakamani kulifungwa kamera maalumu za usalama(CCTV) kwenye lango kuu la kuingilia hapo.
Mahakamani
Washtakiwa
hao walipandishwa kizimbani na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali
Mwandamizi (SSA) Tumaini Kweka ambaye baada ya kesi kutajwa alisema
upelelezi wake umeshakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe ya
usikilizwaji wa awali.
Alisema siku hiyo washtakiwa hao watasomewa
maelezo ya awali ya kesi inayowakabili na kutakiwa kubainisha mambo
wanayokubaliana nayo na wasiyokubaliana nayo.
Hata hivyo, Wakili wa
washtakiwa hao, Juma Nassoro, aliikumbusha mahakama kuhusu dhamana ya
washtakiwa hao, akisema walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza,
maombi yao ya dhamana hayakushughulikiwa kwa vile hakimu aliyepangwa
kusikiliza kesi hiyo hakuwapo.
“Mheshimiwa hakimu, kwa kuwa leo upo
mwenyewe, basi tunaomba uamuzi wa maombi ya dhamana kwa washtakiwa,”
aliomba Wakili Nassoro.
Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Victoria
Nongwa alikubaliana na maombi hayo ya dhamana na kusema kuwa, dhamana
iko wazi kwa washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa kwanza tu (Sheikh
Ponda), ambaye dhamana yake imefungwa na DPP.
“Dhamana iko wazi kwa
washtakiwa wa pili hadi wa 50 kwa kuwa makosa yao yanaweza kuwekewa
dhamana, isipokuwa mshtakiwa wa kwanza tu, kwa sababu DPP alileta hati
ya kuzuia asipewe dhamana,” alisema Hakimu Nongwa na kuongeza:
“Hivyo
mahakama hii haina uwezo wa kisheria kutoa dhamana kwa mshtakiwa wa
kwanza mpaka hapo DPP atakapoleta hati nyingine ya kuondoa zuio la
awali.”
Kwa washtakiwa wengine, Hakimu Nongwa aliwapa masharti ya
dhamana, akiwataka kuwa na wadhamini wawili kwa kila mshtakiwa,
wanaotambulika, wenye vitambulisho, na kwamba wote kila mmoja asaini
dhamana ya Sh1 milioni.
Pia Hakimu Nongwa aliwaamuru washtakiwa hao
wasiende katika eneo la mgogoro uliowasababishia kesi hiyo (Malkazi,
Chang’ombe), hadi hapo kesi itakapokwisha.
Baada ya kutoa masharti
hayo ya dhamana, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15,
kesi hiyo itakaposikilizwa katika hatua ya awali, na kwamba dhamana kwa
washtakiwa hao itashughulikiwa kwa taratibu za kawaida kama ilivyo kwa
washtakiwa wengine.
Alisema kuwa kila mdhamini anaweza kupeleka
mahakamani barua yake ya udhamini wakati wowote, na kama atatimiza
masharti hayo ya dhamana, mshtakiwa husika ataachiwa huru kwa dhamana.
Ulinzi mahakamani
Kutokana
na kuwapo kwa kesi hiyo, kila mtu aliyekuwa anaingia mahakamani,
alikaguliwa kwa kutumia mashine maalumu, huku kamera ikiwa imefungwa
lango kuu kuhakikisha kuwa hali ya usalama na amani inatawala kabla,
wakati na baada ya kesi hiyo kuisha.
Jumla ya magari saba yakiwa na
askari polisi na askari Magereza, zaidi ya 50, waliovalia mavazi maalumu
huku wakiwa na mabomu ya machozi na bunduki, walikuwa wametanda katika
eneo lote kuzunguka mahakama.
Pia lilikuwapo gari la maji ya kuwasha, mbwa watano huku askari wengine wakifanya doria kwa kutumia farasi.
Hata
hivyo, kesi hiyo ilisikilizwa mapema sana na kutokana na hali ya ulinzi
na ukaguzi mkali uliokuwapo mahakamani hapo, watu wengine waliokuwa na
ndugu zao hao waliofikishwa mahakamani hapo, hawakuruhusiwa kuvuka lango
la mahakama.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, ndugu na jamaa wa
washtakiwa hao waliondoka katika eneo la mahakama kwa makundi, huku
askari wakiwasindikiza taratibu hadi walipotokomea.
Maoni
Wakizungumzia
hali ya ulinzi huo, baadhi ya wadau wa mahakama walilipongeza Jeshi la
Polisi kwa kuimarisha ulinzi kwa kiasi hicho mahakamani hapo na kushauri
hali hiyo iendelee katika kipindi hiki ambacho hali ya usalama ni
tete.
Wakili wa Kujitegemea, Majura Magafu aliiomba Serikali
kuendeleza mfumo huo wa ulinzi katika mahakama zote kwa sababu hali ya
usalama bado ni tete.
Naye Gray Hizza aliunga mkono kuwapo kwa mfumo
huo wa ulinzi mahakamani ili kukinga uwezekano wowote wa uvunjifu wa
amani unaoweza kutokea kwa sababu eneo hilo ni sehemu muhimu ya watu
kupata haki.
Ponda na wenzake walipandishwa kizimbani kwa mara ya
kwanza Oktoba 18, 2012 chini ya ulinzi mkali, na kusomewa mashtaka
matano yakiwamo wizi na uchochezi.
Tuhuma zingine ni kula njama,
kuingia kwa nguvu kwenye eneo lisilo mali yake kwa nia ya kutenda kosa
na kujimilikisha ardhi kwa nguvu na kusababisha uvunjifu wa amani.
Sheikh
Ponda alifikishwa mahakamani hapo akiwa na watu wengine 49 ambao
waliunganishwa naye katika mashtaka manne isipokuwa shtaka la uchochezi
ambalo linamkabili Ponda pekee.
Kauli ya Pinda
Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alisisitiza kuwa Serikali itavisambaratisha vikundi vyote
vinavyochochea vurugu nchini, kuwa itatumia kila njia kukabiliana navyo.
Pinda
alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Nzega CCM, Dk
Khamis Kingwangalla wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu akitaka kujua
Serikali inachukua hatua gani kuenzi amani baada ya kutokea vurugu za
kidini nchini za kuchoma makanisa na kukojolea Quran.
Pinda alisema
Watanzania waivumilie Serikali itakapokuwa ikichukua hatua kali dhidi ya
vikundi vya dini ambavyo vinaendelea kuvuruga amani.
“Napenda kuwaomba Watanzania watuvumilie pale tutakapochukua hatua kali dhidi ya vikundi hivyo,” alisema.
Alisema
anajua kuwa viongozi wa madhehebu ya dini wamekuwa wakikutana mara kwa
mara kuzungumzia amani, hivyo aliwataka waongeze kasi zaidi ya kukutana.
Kigwangalla
pia aliwataka Waislamu upande wao kutoa tamko kuhusu vurugu za kidini
zilizotokea hivi karibuni kama walivyofanya maaskofu.
KamandaKova
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana
jioni kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kwa yeyote atakayeanzisha vurugu
leo.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kova alisema: “Tunafahamu
wanaofanya hivi si wote Waislamu, nawasihi watu wasijihusishe na
maandamano kwa kuwa ni haramu.
“Hakuna kibali kilichoombwa, hakuna ruhusa ya kuandamana na maandamano yoyote leo hayako ndani ya sheria,” alisema Kova.
No comments:
Post a Comment