Saturday, November 10, 2012

KITUO CHA WATOTO YATIMA CHAKOSA CHOO



Kituo kilichojengwa kwa ajili ya kulelea watoto yatima kilichopo kijiji cha Maleutsi wilayani Makete kinakabiliwa na tatizo la kutokuwepo kwa vyoo.
 
Akizungumza na rizikimgaya blogspot team kituoni hapo msimamizi wa kituo hicho Mchungaji Simoni Ilomo amesema kuwa tatizo la vyoo limekuwa likikwamisha uzinduzi wa kituo hicho kilichoanza  kujengwa takribani miaka miwili iliyopita chini udhamini wa kanisa la Batheli Morogoro.
 
Amesema ujenzi wa kituo hicho ulisimamiwa na Askofu Mkuu wa kanisa la Tanzania Assemblies of God  [T.A.G] na changamoto kubwa kwa sasa ni kutokuwepo kwa vyoo ambapo ujenzi wa vyoo vinavyohitajika inatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni kumi na tatu.
 
Katika hatua nyingine Mch. Ilomo ameongeza kuwa kituo hicho mara  baada ya kuzinduliwa kitaanza kupokea watoto waishio katika mazingira hatarishi na yatima bila kubagua ukabila wala dini na wanatarajiwa kujenga chuo cha ufundi kwa ajili ya watakaoshindwa kuendelea  na sekondari au kidato cha sita.
 
Hata hivyo amesema watoto watakaolelewa pamoja na kusomeshwa na kituo hicho ni wale walio chini ya umri ya miaka saba pia amewaomba wahisani pamoja na serikali kusaidia ili kituo kianze kutoa huduma kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi.

No comments:

Post a Comment