Saturday, November 10, 2012

ELCT MAKETE WAWANUSURU WATOTO WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU



watoto yatima wakiwa na magodoro yao

Wafanyakazi wa shirika la ELCT Makete - Pamoja Tuwalee program

Mratibu wa pamoja tuwalee MCh. Ezekiel Sanga (katikati) akiwa na wafanyakazi wenzake


Mgeni rasmi Mh. Daniel Okoka akimgawia mtoto yatima viatu


Mh. Daniel Okoka akitoa hotuba yake



Serikali imewataka viongozi wa kijiji cha Lumage kata ya Iniho wilayani Makete kuhakikisha inafuatilia na kujua kama nyumba ni hitaji muhimu la watoto yatima waliopo kwenye kijiji hicho pamoja na walezi kutowanyang’anya misaada wanayopewa watoto hao na kuifanya yao
Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi katika hafla ya kugawa magodoro tisa kwa watoto yatima waliopo kijijini hapo yaliyotolewa na kikundi cha kuweka na kukopa kijijini hapo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh. Daniel Okoka
Mh. Okoka amesema wakati mwingine ni vigumu kuona mtoto yatima hana hata ndugu mmoja hivyo anakosa mahali pa kukaa, ila anachoamini ni kwamba watoto hao wana ndugu lakini wengi wao wanawatesa watoto hao
“Ndugu zangu mimi sidhani kama kuna mtoto hata mmoja ambaye hana ndugu, inawezekana yupo lakini sina uhakika, ndugu walioachiwa watoto hawa wanapaswa kuwatunza kwa upendo ili wasitoroke majumbani” alisema Okoka na kuongeza “ leo tumewapa magodoro haya, ni kwa ajili ya watoto yatima sasa walezi masije mkawanyang’anya watoto na mkayafanya ya kwenu kwa sababu hiyo ndiyo tabia ya watu wengi, mnamnyang’anya mtoto godoro yeye anaendelea kulala chini, watoto mkiona mmefanyiwa hivyo toa taarifa kwa uongozi wa kijiji haraka”
Akizungumzia ushirikiano uliofanywa na Mratibu wa program ya Pamoja Tuwalee wilayani hapa Mch. Ezekiel Sanga, mh Okoka amesema serikali inatambua msaada unaotolewa na mashirika ya dini kuleta maendeleo hivyo akaomba ushirikiano huo uendelee zaidi na zaidi
Pia amesema wazo la program hiyo kuanzisha vikundi vya SILK ni muhimu na lenye kuinua kipato cha wananchi wake huku akisema uongozi wa wilaya ya Makete upo kwenye mchakato wa kuanzisha Benki ya wananchi wa Makete ambayo itakuwa ikishirikiana na vikundi hivyo vya SILK kuinua uchumi wa wanamakete
“Nawahakikishieni sisi kama wilaya tumeshakutana na wanamakete waliopo Dar es Salaam ambao wanafanya kazi kwenye benki mbalimbali na hata kwenye nafasi zingine, wamekubali na wanalishughulikia na muda si mrefu benki hiyo itaanza” alisema Okoka
Katika kukiunga mkono kikundi hicho mgeni rasmi Mh. Okoka alikipa shilingi 50,000/= pamoja na ada ya kujiunga kama mwanachama wa kikundi hicho ya shilingi 50,000/=, viatu kwa watoto hao yatima pamoja na kuahidi kutoa shuka na blanketi kwa kila mtoto aliyepewa godoro
Akizungumza hatua hiyo mratibu wa Program ya Pamoja Tuwalee inayofanya shughuli hiyo kupitia shirika la ELCT Makete Mch. Ezekiel Sanga amesema jukumu la kuwalea watoto yatima ni la kila mmoja hivyo kila mmoja wetu anapaswa kuwasaidia kwa chochote kile ili kuwapa faraja kutokana na kupoteza wazazi wao
Katika kuliunga mkono hilo Mchungaji huyo alianzisha harambee Fulani ya fedha kwa ajili ya yatima katika kijiji hicho ambapo jumla ya fedha taslim tsh. 153,600/- zilichangwa kwa ajili ya watoto yatima wengine kununuliwa mahitaji mbalimbali
  

KWAHISANI YA MAKETE YETU CLUE

No comments:

Post a Comment