Wednesday, November 7, 2012

KASEJA ABWAGA MANYANGA SIMBA SC



Kaseja kulia akizungumza na kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen hivi karibuni


NAHODHA wa Simba, Juma Kaseja amewaaga wachezaji wenzake na kuwaambia yeye na klabu hiyo basi.
rizikimgaya amefika kwenye mazoezi ya Simba jioni ya leo Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam na kukuta wachezaji wote wakiendelea na mazoezi kujiandaa na mechi ya Toto African mwishoni mwa wiki, kasoro Kaseja na Amir Maftah.
Alipoulizwa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kwamba Maftah ana ruhusa maalum kwa sababu ameoa hivi karibuni, lakini Kaseja hawana taarifa zake, ila; “Nadhani hatakuwa vizuri kisaikolojia baada ya kufanyiwa fujo Jumamosi,”alisema Kamwaga.
Lakini rizikimgaya ilipozungumza na wachezaji wenzake, walisema Nahodha wao amewaaga kwamba yeye na Simba basi, kwani ameumia sana kwa jinsi alivyodhalilishwa na mashabiki Jumamosi Morogoro.
“Juma hapa ndio basi kaka, Kasema yeye na Simba basi, amesononeshwa mno na jinsi alivyodhalilishwa baada ya mechi ya Morogoro,”alisema mchezaji mmoja wa Simba baada ya mazoezi Kinesi leo.
Kaseja alitukanwa na kutishiwa maisha na mashabiki wa Simba baada ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakimtuhumu kufungwa mabao ya kizembe.
Lakini tayari uongozi wa Simba umelaani vikali vurugu na vitisho alivyotolewa kipa wao huyo namba moja,  na kusema wanafikiria kuwachukulia hatua kali watu waliomfanyia hivyo Nahodha wao huyo.
Juhudi za kumpata Kaseja mwenyewe kuzungumzia suala hilo, hazikuweza kufanikiwa kwani simu yake ilikuwa haipatikani.

No comments:

Post a Comment