FAMILIA za washtakiwa wanane katika kesi za uchochezi Zanzibar
wameandika barua kwa Waziri wa Katiba na Sheria na taasisi zingine,
wakilalamikia ukiukwaji haki za binadamu.
Pia, barua hiyo imepelekwa kwa Mkurugenzi wa Kituo
cha Sheria Zanzibar, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu cha Tanzania
kilichopo Dar es Salaam, Amnesty International na ofisi za balozi za nje
nchini.
Katika barua hiyo ya Novemba 13, mwaka huu familia
zinazolalamika ni za Sheikh Farid Hadi Ahmed, Msellem Ali Msellem,
Azzan Khalid Hamdan, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma, Khamis Ali, Hassan
Bakari na Gharib Ahmad ambao wanakabiliwa na kesi mbili za uchochezi
Mahakama Kuu Zanzibar na Mwanakwerekwe.
Barua hiyo ambayo imetiwa saini na watu wanane wa
familia hizo, wanadai ndugu zao wanachukuliwa zaidi ya wafungwa wakati
ni mahabusu na wanatuhumiwa tu na mahakama haijawatia hatiani.
Mambo ambayo wanadai kuwa wanafanyiwa, ni kuzuiwa
kubadili nguo kwa muda wa zaidi ya wiki tatu na hawaruhusiwi kuletewa
zingine kutoka nyumbani na kupatiwa chakula kutoka nyumbani.
Wanadai kuwa miongoni mwao wengine ni wagonjwa wa
vidonda vya tumbo na hawawezi kula, kitendo ambacho kinakwenda kinyume
na miiko ya kitabibu na kuzuiwa kuonana na familia zao.
Madai mengine ni kuzuiwa kuwaona kwa uhuru
mawakili wao, wanafamilia kusikiliza kesi zao, masharti magumu na
yasiyotekelezeka kama kuwataka washtakiwa wapate dhamana ya watu ambao
wanafanya kazi serikalini, mahabusu hao kutengwa kila mtu chumba chake.
Pia, wanafamilia hao wanadai kuwa watuhumiwa
wananyimwa haki ya kuabudu kwa kunyimwa vitabu vya Qur’an na kuzuiwa
kuswali pamoja wakati mahabusu wengine wanaruhusiwa.
“Huu ni udhalilishaji unaopita mipaka ya binadamu
na kinyume na sheria za nchi yetu inayodai ni ya demokrasia, ni kinyume
cha sheria za kimataifa ambazo Tanzania imezikubali,” inadai sehemu ya
barua hiyo.
Nakala za barua hiyo zimetumwa kwa Mwanasheria
Mkuu Zanzibar, Kamishna Chuo cha Mfunzo Zanzibar, Waandishi wa Habari
Tanzania, Waislamu wote Tanzania na Mkurugenzi wa Mshtaka Zanzibar
(DPP).
Washtakiwa hao wapo rumande na kesi zao zinatarajiwa kuendelea tena Novemba 20, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment