MKUU WA MKOA Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanafunzi wa vyuo
vya elimu ya juu walioko katika mkoa huo kujihoji nafsi zao na kucheki matendo
yao kama kweli ni ya kumpendeza Mungu kwa vile ndiyo yanachangia wao kutotambua
umuhimu wa nafasi walizonazo.
Dk. Nchimbi ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akihutubia
maelfu ya wanavyuo waliohudhuria Jumuiko la Wanavyuo wa Dodoma (Dodoma Campus
Night) lililoambatana na mkesha wa kusifu na kuabudu uliofanyika kwenye ukumbi
wa Chimwaga mjini Dodoma.
Jumuiko hilo lilihudhuriwa na wanafunzi zaidi ya 3,500 wa dini
mbalimbali kutoka vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM), St. John’s, Vyuo vya Mipango,
Madini, Mirembe, Hombolo, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na vyuo vya ualimu
vya Mitumba na Capital.
Dk. Nchimbi alisema wanavyuo wengi ambao walifaulu kidato cha sita
kwa alama za juu (first class) huwa wanaporomoka kimasomo wanapoingia kwenye
vyuo vya elimu ya juu kwa sababu hawajiweki sawa kwenye mahusiano yao na Mungu
aliyewaumba. “Wanaharibikiwa kwa sababu hawajiweki sawa na Mungu... hawakai pale
ambapo Mungu anataka wawe (their right position),” alisema.
Alisema idadi kubwa ya wanavyuo wakishapata fedha za mkopo hutumbua
maisha kwenye vilabu vya muziki ambavyo ni maarufu mjini humo kama vile Club
84, Club La Aziz na Maisha Club na hawarudi vyuoni hadi fedha yote
imekwisha.
Alisema yeye kama mzazi analazimika kuyasema hayo kwa sababu
anatambua kuwa watoto wa leo wamezungukwa na mitego mingi. “Hatutaki shetani
awachezee, ndiyo maana tunawaonya,” alisisitiza.
Alisema katika kundi kubwa kama hilo wamo viongozi wa kesho na kwamba
wasipojihadhari na kuweka mahusiano yao sawa na Mungu kuanzia sasa, watajikuta
wanafanana na baadhi ya viongozi nchini ambao wamekabidhiwa dhamana lakini
wanakengeuka na kufanya kinyume na matarajio ya wengi.
Mapema, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji
Gerald ole Nguyaine wa Kanisa la ICC –TAG Dodoma alisema wanafunzi walio katika
vyuo hivyo ni wababa na wamama wa kesho hivyo hawana budi kumtanguliza Mungu
katika yote wayafanyayo.
Naye Mchungaji Gavin Walker kutoka Kanisa la Calvary Christian Fellowship
lililoko Columbus, Ohio, Marekani ambaye alikuwa mnenaji mkuu katika mkesha huo,
aliwasihi wanavyuo kutambua makusudi ya Mungu ambayo ameyaweka juu yao. “Mungu
amekuumba wewe kwa kusudi maalum hivyo ni lazima ujue hilo kusudi”, alisema.
Alisema kwa kutotambua kusudi la Mungu katika maisha yao, wako watu
ambao wamejikuta wakitaka kufanana na wengine bila kujua ni kwa nini watu hao
wamekuwa hivyo. “Wanatamani nafasi za wengine kwa sababu tu wao ni maarufu, ni
waigizaji, ni wacheza sinema ama wasanii... hapana! Kila mmoja anatakiwa kujua kusudi ka Mungu katika maisha yake,”
alisisitiza.
Irene K. Bwire,
Email:
irenekaki@yahoo.com
No comments:
Post a Comment