Chelsea imetangaza kumfukuza kazi Meneja
wake Roberto Di Matteo mara baada ya jana kuchapwa Bao 3-0 na Juventus
kwenye Mechi ya UEFA CHAMPIONZ LIGI ambayo imewaweka katika hali ngumu
kusonga mbele Raundi inayofuata na hivyo kuwa hatarini kulitetea Taji
lao la Ubingwa wa Ulaya.
Msimu uliopita Di Matteo alitwaa UEFA
CHAMPIONZ LIGI na FA CUP akiwa Meneja wa muda na Mwezi Juni alisaini
Mkataba mpya wa Miaka miwili uliomsimika kama Meneja wa kudumu.
Chelsea, ikitoa taarifa ya kufukuzwa Di Matteo, pia imesema watatangaza hivi karibuni nani atashika wadhifa wa Meneja.
++++++++++++++++++++++++++++++
HIMAYA ya ROMAN ABRAMOVICH=MAMENEJA:
-Claudio Ranieri: Septemba 2000-Mei 2004
-Jose Mourinho: Juni 2004-Septemba 2007
-Avram Grant: Septemba 2007-Mei 2008
-Luiz Felipe Scolari: Julai 2008-Februari 2009
-Guus Hiddink: Februari 2009-Mei 2009
-Carlo Ancelotti: Juni 2009-Mei 2011
-Andre Villas-Boas: Juni 2011-Machi 2012
-Roberto di Matteo: Machi 2012-Novemba 2012
++++++++++++++++++++++++++++++
Inaaminika Mmiliki wa Chelsea, Tajiri
Roman Abramovich, ameshafanya mazungumzo na Meneja wa zamani wa
Liverpool Rafael Benรญtez ili ashike wadhifa wa Meneja.
Chelsea walianza vyema Msimu huu kwa
kushinda Mechi 7 kati ya 8 za kwanza kwenye Ligi na kutwaa uongozi
lakini tangu wachapwe 3-2 na Manchester United Uwanjani kwao Stamford
Bridge wamezidi kudidimia na wameshinda Mechi mbili tu kati ya 8 za
mwisho.
Kwa sasa wapo nafasi ya 3 kwenye Ligi
Kuu England wakiwa Pointi 4 nyuma ya vinara Manchester City ambao
Jumapili ijayo watapambana nao Uwanjani Stamford Bridge kwenye Mechi ya
Ligi.
Ikiwa Chelsea watashindwa kuvuka hatua
ya Makundi ya UEFA CHAMPIONZ LIGI, kitu ambacho ni kigumu hasa kwa vile
kwenye Kundi lao Shakhtar Donetsk washafuzu na Juventus wanahitaji sare
watakapocheza na Shakhtar katika Mechi ya mwisho ili wafuzu, itawafanya
Chelsea waweke historia ya kuwa Mabingwa wa kwanza watetezi kushindwa
kuvuka hatua ya Makundi.
Hivi sasa, Abramovich anasaka Meneja wake wa 9 tangu yeye mwenyewe atue Stamford Bridge Mwaka 2003.



No comments:
Post a Comment