Thursday, November 8, 2012

AZAM YAFUKUZA KIPA NA MABEKI KWA TUHUMA ZA KUHUJUMU DHIDI YA SIMBA, YANGA



AZAM FC imewasimamisha wachezaji wake watatu wa safu ya ulinzi, kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Said Mourad na Erasto Nyoni kwa tuhuma za kuihujumu timu hiyo katika mechi zake za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya vigogo Simba na Yanga hivi karibuni.
Azam ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, mwaka huu kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Yanga Novemba 4, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi za Ligi Kuu.
Baada ya kufungwa na Simba, Azam FC ilimfukuza kocha wake Mserbia, Boris Bunjak na kumrejesha Muingereza, Stewart Hall.
Habari kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata taarifa hizo, uongozi ulizifanyia kazi taratibu na kujiridhisha kabisa wachezaji hao watatu walikula njama za kuihujumu timu katika mechi hizo.
Kwa sababu hiyo, uongozi kwanza umewasimamisha wachezaji hao na hatua zaidi zitafuatia baadaye.
Hata hivyo, Dida hakucheza mechi hata moja kati ya hizo, kwani Oktoba 27, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim, Himid Mao aliyempisha Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Herman Tcheche na Salum Abubakar.
Siku hiyo, Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka mabeki wa Azam.
Katika mechi na Yanga, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ally, Erasto Nyoni aliyempisha Samir Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris na Said Mourad, Jabir Aziz aliyempisha Ibrahim Mwaipopo, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyempisha Abdi Kassim ‘Babbi’, Salum Abubakar, John Bocco na Kipre Tcheche.
Siku hiyo, mabao ya Yanga yalitiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kvumbangu aliyeunganisha krosi ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia dakika ya tisa na Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 68, akiunganisha krosi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka wingi ya kulia.
Habari zaidi zinasema kwamba, uchunguzi unaendelea kufanywa juu ya wachezaji wengine wanaotuhumiwa kuwa katika mkumbo huo wa kuihujumu timu na ikithibitika ni ukweli, watachukuliwa hatua pia bila kujali majina yao.
Azam tayari iko Tanga tangu saa 8:00 mchana wa leo kwa ajili yao ya mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara keshokutwa dhidi ya Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani. 
Na Mahmoud Zubeiry

No comments:

Post a Comment