Monday, October 29, 2012

CHADEMA KUTINGA MAHAKAMANI KUPINGA USHINDI WA MGOMBEA WA CCM KATA YA LUWUMBU MAKETE


 Mwenyekiti wa BAVICHA taifa John Heche akiongea na wanahabari hii leo
 Hapa mwana habariri kutoka kitulo fm eddy mo blaze akimhoji Bw. Heche
Siku moja baada ya Mgombea udiwani kata ya Luwumbu wilayani Makete kwa tiketi ya CCM kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo, Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kimesema kinatarajia kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo muda wowote kuanzia sasa
CHADEMA kimesema uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya rushwa kwa kiasi kikubwa pamoja na sababu nyingine tano ambazo wameona kuwa ndizo watazisimamia mahakamani kupinga matokeo hayo
Akizungumza hii leo na mtandao huu wa rizikimgaya.blogspot.com mwenyekiti wa baraza la vijana wa chadema taifa BAVICHA Bw. John Heche amesema wameamua kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo kutokana na sababu tano walizozigundua ikiwemo sababu kuu iliyofanywa na naibu waziri wa maji na mbunge wa jimbo la Makete Dkt. Binilith Mahenge
“Tutakwenda mahakamani tukiwa na sababu kama tano hivi ya kwanza na iliyotushangaza ni ya naibu waziri kutumia cheo chake kutoa ahadi ya serikali kwenye mkutano wa CCM  wa kufunga kampeni pale Usililo kuwa wakichagua CCM basi atawaletea maji, huu ni ukiukwaji wa taratibu na hairuhusiwi, nadhani mlisikia aliyosema waziri wa ujenzi pale Igunga sina haja ya kurudia” alisema Heche
Pia kiongozi huyo hakutaka kuzitaja sababu nyingine zinazopelekea wao kwenda mahakamani, ila alizizungumzia kitendo cha watu wachache kujitokeza kushiriki uchaguzi huo kuwa kwa kiasi kikubwa limechangiwa na rushwa na vitisho
Amesema kwenye uchaguzi huo kulitawaliwa na aina mpya ya rushwa yaani rushwa ya pombe, ambapo watu walinunuliwa pombe ili wakichague chama cha CCM ilihali walitakiwa watoe sera zao na watu wawachague bila kuwapa chochote
Ameongeza kuwa mbali na na hilo pia ziligawanywa kofia, na t-sherts kwa wananchi hao, huku akisema kutokana na chama chake kutotambulika sana katika kata hiyo, wanakwenda kujipanga na watakuja kukiimarisha zaidi wakati wa kampeni ya M4C katika mikoa ya Iringa na Njombe na Makete ikiwemo
Kwa upande wao CCM kupitia kwa Katibu wa wilaya Bw. Miraji Mtaturu amesema waliutegemea ushindi huo tangu mwanzoni licha ya mgombea wao kupakwa matope na Chadema kwa kumuita fisadi
Amesema anawashukuru wanaluwumbu kwa kuwa matokeo ya uchaguzi huo yameonesha kuwa mgombea wao sio fisadi na ndio maana ameshinda kwa kishindo
Amekiponda chama cha chadema kusema kuwa kina siasa za uongo kwa kuzusha vitu vya uongo kwa CCm ikiwemo kumuita mgombea wao ni fisadi
“Unajua kama huna utafiti huna haki ya kuzungumza mtu unasikia tu kuwa Fulani ni fisadi na wewe unayachukua na kuyapeleka jukwaani kuwa Fulani ni fisadi, hii haipendezi, tufanye siasa za kisayansi na ndio maana tumewapiga bao tena kubwaa” alisema Mtaturu
Pia ameongeza kuwa kutokana na ilani ya CCM kutekelezwa katika kata hiyo kwa sasa wataendeleza kutekeleza shughuli walizozifanya tangu awali za kielimu na kiafya ili kuendeleza waliyowaahidi wananchi
Akitangaza matokeo hayo Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Makete Bw. Cyrus Kapinga amesema idadi ya wapiga kura walioandikishwa walikuwa ni 1,592 lakini idadi ya waliopiga kura ni 620, kura zilizoharibika 15
Amesema Mgombea kupitia Chadema Bw. Raphael Kyando alipata kura 40 huku mgombea wa CCM Mch. Enock Ngajilo akipata kura 565
Mtandao huu umeshindwa kupata maoni ya wagombea hao kutokana na mgombea wa CCM kupata  msiba wa mwanaye na mgombea wa chadema kutopatikana kwa simu yake ya kiganjani

No comments:

Post a Comment