Tuesday, May 8, 2012

Mwalimu mkuu ajitia kitanzi afisini mwake


Mikonge
Shamba la mikonge katika kijiji cha Singila, eneo la Mwatate. Mwalimu mkuu wilayani Mwatate alijiua siku ya kwanza ya muhula wa pili Jumatatu. Picha/MAKTABA 
Na KENYA NEWS AGENCY  ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, May 8  2012  at 10:54
Kwa Mukhtasari
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Mwandala, Taita Taveta alijifungia ndani ya afisi yake na kujinyonga siku ya kwanza ya muhula. Baada ya matokeo ya KCPE, alikuwa amezomewa na kufurushwa nje ya shule na wazazi waliokuwa na hasira kutokana na matokeo mabaya. Haijabainika nini hasa kilimfanya ajitoe uhai.

MWALIMU Mkuu wa shule ya msingi ya Mwandala, wilayani Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta, alijiua baada ya kujifungia ndani ya afisi yake, siku ya kwanza baada ya shule kufunguliwa kwa muhula wa pili.
Mwili wa Bw Peter Mwabili ulipatikana ukining’inia kwenye paa na walimu waliokuwa waliovunja mlango waweze kuingia ndani ya afisi yake.
Polisi wakiandamana na viongozi wa eneo hilo, waliwasili baadaye na kuuchukua mwili huku wakiwaacha wakazi, walimu na wanafunzi wakiwa wameshangazwa na kushtushwa mno na tukio hilo.
Marehemu aliacha barua iliyoelezea jinsi ambavyo mali yake ilistahili kugawanywa kati ya wanawe na mkewe. Alisema mkewe anafaa kurithi robo ya mali huku watoto wake wanne wakipata thumni (sehemu moja kati ya nane), huku kitinda mimba akipata sehemu moja kati ya 16 ya mali yake.
Barua hiyo pia iliwataja watu aliokuwa akiwadai na kiasi cha pesa anazowadai na kuwataka walipe madeni kwa familia yake.
Mapema asubuhi
Mkuu wa tarafa ya Mwatate,  Bw Aswani Were, alisema Bw Mwabili alifika shuleni mapema asubuhi Jumatatu na kujifungia ndani ya afisi yake kabla ya kujitoa uhai.
“Alifika kazini kama kawaida na kujifungia afisini mwake. Walimu wengine waliompata walilazimika kuvunja mlango kwani alikuwa amejifungia kutoka ndani,” akasema.
Marehemu alikuwa na wakati mgumu katika shule ya Mwandala huku wazazi wakati mmoja wakimfurusha na kumfungia nje ya shule mwishoni mwa mwaka jana wakiitisha kuhamishwa kwake kutokana na matokeo duni ya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE).
Alikuwa amehudumu kwa muda mrefu kama mwalimu mkuu katika shule za eneo hilo, ikiwa ni pamoja na shule za msingi za Kamutonga na Mwachabo kabla ya kuhamishiwa Mwandala kutoka shule ya msingi ya Mwandisha ambapo alikuwa akihudumu kama naibu mwalimu mkuu.
Mkuu wa polisi wa kituo cha Taita Charles Kibet alisema mwili ulipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti cha Wesu kusubiri kufanyiwa upasuaji.
“Uchunguzi umeanzishwa kuhusu kisa hicho,” akasema. “Tunajaribu kuchunguza tubaini ni nini huenda kilimfanya ajitoe uhai,” akasema Bw Kibet.

No comments:

Post a Comment