Tuesday, May 29, 2012

MIRADI YA MAENDELEO YA MABILONI YA FEDHA YAZINDULIWA NA MWENGE WA UHURU MAKETE

Mwenge wa uhuru ukiwa eneo la mkesha Mabehewani wilayani hapa
 
Miradi tisa yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili imezinduliwa na mwenge wa uhuru ambao unaendelea na mbio zake katika wilaya ya Makete

Hayo yamebainika baada ya miradi hiyo kuzinduliwa rasmi na mwenge huo wa uhuru ambapo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bi Imelda Ishuza amewaeleza maelfu ya wakazi wa Makete waliofurika katika viwanja vya Mabehewani wilayani Hapo kuupokea mwenge huo ambao pia utakesha hapo

Akitoa taarifa hizo Bi Ishuza ameitaja miradi hiyo iliyozinduliwa na Mwenge huo wa uhuru kuwa ni pamoja na Ofisi ya kijiji kipya cha Ikovo, kituo cha CTC kilichopo ndani ya Kituo cha afya Matamba, Nyumba bora ya Nuhu Ngogo iliyopo Matamba na Hoteli ya Kitulo iliyopo Matamba


Mingine ni Vyumba vya madarasa na nyumba ya mwalimu mkuu shule ya msingi Manga, Mradi wa maji katika kijiji cha Nkenja, shamba la miti katika kijiji cha Ivalalila pamoja na nyumba tatu za watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Makete

Akizungumza na wakazi wa Makete kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Kapteni Honest Ernest Mwanosa amewataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi hiyo hasa mradi wa maji, ambao kwa kiasi kikubwa utawahudumia wananchi wenyewe

"Unajua wananchi utunzaji wa vyanzo vya maji ni kitu muhimu sana, wilaya ya Makete ni miongoni mwa wilaya chahe zilizojaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji, tujiepushe kulima kwenye vyanzo vya maji pamoja na kuendesha shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo na badala yake tuvitunze" alisema Mwanosa

Pia amewataka wananchi wa Makete kujitokeza kushiriki katika mchakato wa katiba mpya kwa kutoa maoni yao pamoja na kushirikkikamilifu katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchi nzima Usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu

Mwenge wa uhuru upo wilayani Makete na kesho utakabidhiwa katika wilaya ya Njombe, na kaulimbiu ya mwaka huu ni sensa ni msingi wa maendeleo yetu mwananchi shiriki kikamilifu Agosti 26 2012, mabadiliko ya katiba toa maoni

No comments:

Post a Comment