BAADA ya Kanisa la Assemblies of God kuchomwa moto katika vurugu
zilizoanza mwishoni mwa wiki iliyopita, jana Kanisa Katoliki Parokia ya
Mpendae nalo limechomwa moto.
Akizungumzia hali hiyo jana, kiongozi wa Kanisa hilo, Ambaros
Mkenda, alidai kwamba Kanisa hilo lilichomwa moto na watu wasiojulikana
na kusababisha uharibifu mkubwa.
Alidai Kanisa hilo lilichomwa moto jana saa 8.30 mchana na watu
wanaohisiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho, waliokuwa
wakitoka katika Mahakama ya Mwanakwerekwe kusikiliza kesi ya wenzao
waliokamatwa juzi.
Mkenda alidai kuwa watu hao waliwazidi nguvu walinzi wawili wa
Kanisa hilo na kuvunja lango kuu la kuingilia ndani ya Kanisa na kuchoma
moto na waliharibu madirisha na vifaa kadhaa vyenye thamani ya Sh
milioni 20.
“Tunasikitika sana na uharibifu mkubwa uliofanywa katika Kanisa letu
ambalo lilikuwa tegemeo kubwa kwa wafuasi wapatao 2,000 wa eneo la
Parokia ya Mpendae na jirani,” alisema Mkenda.
Mkenda alidai kuanzia juzi, viongozi wa makanisa mbalimbali
waliwasilisha maombi yao Polisi kuhusu kupewa ulinzi katika nyumba za
ibada, baada ya kupokea vitisho. Hata hivyo, Mkenda alidai ombi lao
hilo halikutekelezwa na Polisi na uharibifu mkubwa ukatokea katika
Kanisa la Assemblies of God la Kariakoo.
Wafuasi na waumini wa Kanisa hilo walikusanyika nje ya jengo hilo,
huku vijana wakishikwa na hasira wakitaka kwenda kulipiza kisasi katika
maeneo ya jirani wakidai wanawatambua vijana waliofanya vitendo hivyo.
Mmoja wa waumini wa Kanisa hilo ambaye ni mwandishi wa habari wa
Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Susan Kunambi alilazimika
kuwatuliza wafuasi vijana wa Kanisa hilo waliopandwa na jazba wakitaka
kulipa kisasi.
“Hakuna sababu ya kupandisha jazba na kutaka kufanya vitendo ambavyo
vitasababisha hasara na uharibifu ... Kanisa siku zote linahimiza amani
na upendo na si chuki,” alisema Kunambi.
Polisi walifika haraka katika eneo la tukio na kurusha mabomu ya
machozi ili kutawanya makundi ya vijana waliojikusanya na wengine
kurusha mawe.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alithibitisha kuchomwa
moto Kanisa hilo na kusema ulinzi umeimarishwa katika baadhi ya maeneo
ya nyumba za ibada yakiwamo makanisa. Baadhi ya mitaa ya Jang’ombe na
Mwanakwerekwe njia zimewekwa mawe na vikundi vya vijana waliochoma
mipira ya gari na kusababisha moshi mkubwa.
Vikundi marufuku Wakati huo huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ) imepiga marufuku maandamano, mihadhara ya kidini na mikusanyiko
isiyo na kibali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud
alisema hayo wakati akitoa taarifa rasmi ya SMZ baada ya vurugu
zilizofanywa na wafuasi wa Uamsho baada ya kukamatwa kwa viongozi wao wa
kidini.
Aboud alisema Serikali haitakubali kuona kikundi cha watu wanafanya
vitendo vya uvunjifu wa amani na kuvuruga utulivu wa nchi kwa kisingizio
cha kudai mabadiliko ya Katiba na imani ya dini.
“Wapo watu wanataka kuona tunarudi nyuma katika kipindi cha fujo na
vurugu za kisiasa...wakati huo umepita,” alisema Aboud. Kutokana na
hatua hiyo ya Serikali, mihadhara na maandamano kuanzia sasa
italazimika kupata kibali kutoka taasisi husika ikiwamo Polisi.
Alitaka wazazi wakataze watoto wao kujishughulisha na ushawishi wa
kufanya vitendo vitakavyohatarisha amani na utulivu wa nchi.
Utulivu wajirudia mjini Jana hali ya utulivu ilirejea kisiwani hapa
ikiwamo Mji Mkongwe na sehemu za mitaa ya Ng’ambo, huku wananchi
wakifanya shughuli zao za maendeleo na biashara bila matatizo.
Maduka na huduma za usafiri viliendelea kama kawaida huku
wafanyakazi wa Manispaa wakifanya usafi ikiwa ni pamoja na kuondoa
matairi ya magari yaliyochomwa barabarani katika vurugu za juzi.
“Tunasafisha barabara zilizoharibiwa na waandamanaji kwa kuchoma
moto mipira ya magari,” alisema Ali Juma mfanyakazi wa Manispaa ya Mji
wa Unguja. Kamishna Mussa alisema Polisi waliendelea kuweka doria
katika maeneo mbalimbali ya mji kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ.
“Tutaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ikiwamo nyumba za
ibada ili kuhakikisha hakuna vitendo vya uvunjifu wa amani,” alisema
Mussa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alionya kuwa suala la
amani na ulinzi wa raia na mali zao halina mjadala na kuvihadharisha
vikundi vinavyohatarisha amani, kwamba vitapambana na mkono wa Dola.
Dk Nchimbi aliyekuja hapa ili kukutana na viongozi wa vikundi vya
dini na mihadhara na Polisi, alisema athari ya kuvunja amani na utulivu
ni kubwa na wananchi wa Zanzibar wanafahamu vizuri mazingira
yalivyokuwa miaka ya nyuma.
Alitaka viongozi wa dini wajifunze sheria za nchi na kuzifuata na
kuwataka wasihusishe Uislamu na vurugu na fujo kiasi cha kuhatarisha
amani ya nchi.
Pia alitaka wananchi walioharibiwa mali zao kwenye vurugu na fujo kutoa taarifa Polisi kwa hatua zaidi.
Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema,
alisema Polisi itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo
yote ya nchi.
Watu 30 wakiwamo wafuasi wa Uamsho walifikishwa katika Mahakama ya
Wilaya ya Mwanakwerekwe kujibu mashitaka yakiwamo ya kuandamana kinyume
cha sheria na ukorofi wa kuwashambulia polisi kwa mawe.
Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka katika makundi matatu tofauti;
kundi la kwanza likiwa la viongozi wawili wa jumuiya hiyo; Mussa Juma
Issa (57) na Mbarouk Said Khalfan (45). Walisomewa mashitaka mbele ya
Hakimu Mohamed Ali Sheni ya kujikusanya kinyume cha sheria na kufanya
maandamano ambayo yalianzia Uwanja wa Lumumba kupitia Msikiti wa
Kwabiziredi na kumalizia uwanjani hapo.
Watuhumiwa hao walikana mashitaka na kupewa dhamana ya masharti ya
Sh 300,000 kila mmoja kwa kiasi hicho hicho; walitimiza masharti na
wako nje kwa dhamana hadi Juni 11 kesi yao itakapotajwa. Kundi la pili
la watuhumiwa wengine sita walisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Janet
Sekihola ambayo ni ya uzembe, ukorofi na kushambulia polisi waliokuwa
doria.
Watuhumiwa hao ni Abdulrahman Simai Khatib, Hashim Juma Issa, Martar
Said Ramadhan, Mbwana Hamad Juma, Masoud Hamad Mohamed na Mohamed
Juma Salum.
Kesi ya watuhumiwa hao iliahirishwa hadi Juni 11 itapotajwa huku
baadhi yao wakitafuta wadhamini na kutakiwa kuwa na wadhamini wawili
kila mmoja kwa Sh 500,000.
Maimamu wawakana Jumuiya ya Maimamu na Mihadhara ya Jumaza,
imesema waliofanya fujo na vurugu zilizosababisha uharibifu mkubwa wa
mali za wananchi si wafuasi wao.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Muhidin Zubeir
Muhidin ambayo pamoja na jumuiya hiyo ndizo taasisi zinazojishughulisha
na mihadhara ya dini ya Kiislamu ambayo hutoa elimu kuhusu marekebisho
ya Katiba.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Shehe Zubeir alisema jumuiya
hiyo haijatuma watu kufanya fujo, kwa sababu katika dini hiyo ni makosa
mtu kuharibu mali ya mwenzake. “Tunataka Waislamu wote na wafuasi wa
Jumaza na Uamsho kuacha fujo na kurudi nyumbani kusubiri hatma ya
viongozi wao,” alisema Shehe Zubeir.
Serikali ya Marekani imesema matukio yaliyotokea kwa siku mbili
Zanzibar yanaweza kuchafua taswira nzuri iliyowekwa na visiwa hivyo,
katika uchaguzi mkuu uliosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa mwaka 2010.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari kutokana na ghasia zilizotokea
visiwani humo na kusababisha Kanisa na gari la kiongozi wa Kanisa
kuchomwa moto.
“Kudumisha mazingira ya amani visiwani Zanzibar ambayo yanaruhusu
utalii na maendeleo kuna maslahi kwa Wazanzibari wote na hata wageni
waingiao visiwani humo,” alisema Balozi Lenhardt katika taarifa yake
iliyotolewa jana Dar es Salaam.
Alisema ni muhimu kwa kila mtu kujizuia na kulinda maisha na mali za
watu wasio na hatia na aliunga mkono waliozitaka pande zinazozozana
kushirikiana kuleta amani na utulivu katika visiwa hivyo.
“Tunatambua umuhimu wa mjadala wa kisiasa unaoendelea lakini
tunavitaka vyama vyote kuendelea kuufanya kwa njia ya amani na
kidemokrasia zaidi,” alisema Balozi huyo.
Aliongeza kuwa anakubaliana na anaunga mkono hatua za haraka
zilizochukuliwa na viongozi waandamizi wa kisiasa waliojitokeza
kushughulikia masuala yaliyosababisha matukio hayo ya kusikitisha.
No comments:
Post a Comment