WAWAKILISHI
pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba leo inashuka dimbani jijini Dar es Salaam kucheza mchezo wa kwanza
raundi ya tatu ya mashindano hayo dhidi ya timu ya Al Ahly Shendi ya
Sudan.
Simba ilifika hatua hiyo baada ya kutumia nguvu nyingi
kuziondoa kwenye mashindano miongoni mwa timu bora na ngumu katika
kinyang'anyiro hicho, Kiyovu ya Rwanda na ES Setif ya Algeria. Ilitoka
sare ya bao 1-1 na wawakilishi wa Rwanda katika mchezo walioanza
ugenini, na kisha kuja kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano
jijini Dar es Salaam.
Raundi ya pili, iliifunga ES Setif 2-0
kwenye mechi ya nyumbani, na kisha kufungwa mabao 3-1 ugenini, kipigo
ambacho hakikuwazuia kusonga mbele kutokana na sheria ya faida ya bao la
ugenini. Kabla hata ya kutoa kauli yetu kwa wawakilisha hao,
tunaamini wanaelewa umuhimu wa mchezo huo na hasa zaidi ukizingatia
wanaanza nyumbani na kwenda kumaliza ugenini.
Tunafahamu
wamejiandaa kupambana kufa na kupona lengo likiwa ni kupata ushindi
mnono nyumbani ili kuepuka kujitwisha mzigo mzito wa kutafuta ushindi
kwenye mchezo wa marudiano. Tunasema hivyo kwa sababu, ushindi wa
mabao mengi bila kuruhusu bao utawasaidia kuifanya mechi ya marudiano
jijini Khartoum kuwa ya kukamilisha ratiba tu.
Tunapenda
kuikumbusha Simba kutumia fursa hii ya kuanza nyumbani kuhakikisha
wanapata ushindi mkubwa, na hilo linawezekana iwapo tu wachezaji
watajituma muda wote wa mchezo.
Ikumbukwe, Al Ahly Shendi siyo
timu ya kubezwa pamoja na kwamba inashiriki michuano hiyo kwa mara ya
kwanza, lakini iliweza kuiondoa kwenye mashindano Ferroviario Maputo kwa
kuifunga bao 1-0 ugenini, na kisha wakashinda 2-0 kwenye mchezo wa
marudiano nyumbani.
Tunatarajia Simba ambayo haisumbuliwi na
wachezaji majeruhi itafanya vizuri katika mechi ya kesho kama
inavyofanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania bara, ambapo
inaongoza ligi hiyo. Tunaitakia kila la kheri Simba. SHUURANI KWA MWANACHI COMMUNICATION |
No comments:
Post a Comment