Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi tarehe 26 Agosti 2012 na
kuendelea kwa takriban siku saba. Hii itakuwa Sensa ya tano (5) tangu Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na kufuatiwa na Sensa nyingine za
mwaka 1978, 1988 na 2002.
Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua na
kusambaza takwimu za kidemografia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote
na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum. Kwa maana nyingine, Sensa ni
zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na
jinsi, mahali wanapoishi, hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na
vifo na hali ya makazi.
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ina umuhimu wa kipekee kwani
mbali ya kutimiza malengo ya kawaida ya sensa, takwimu zitakazokusanywa katika
sensa hiyo zitatumika katika kutathmini utekelezaji wa mipango yetu mikubwa ya
maendeleo ambayo imekuwa ikitekelezwa katika kipindi kilichopita.
Mipango hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza
Uchumi Tanzania - MKUKUTA kwa Tanzania bara Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar - MKUZA
kwa upande wa Zanzibar. Halikadhalika, takwimu za Sensa ya mwaka 2012
zitatumika kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Milenia 2015.
Nafasi zenu katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi
Hamna budi kufahamu kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ndizo
zitakazoiwezesha Serikali kutambua hali halisi na mahitaji halisi ya huduma
zilipo katika maeneo yenu hivyo kuingizwa katika mipango ya maendeleo ya taifa.
Kwa hiyo mnapaswa kuwahamasisha wananchi ili wahesabiwe na wahesabiwa mara moja tu, ili takwimu
zitakazokusanywa ziwe sahihi na za uhakika. Usahihi wa takwimu katika kila eneo
ndio utimilifu wa takwimu za taifa.
Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuhamasisha wananchi: tarehe ya Sensa, umuhimu wa Sensa na
yatakayojiri wakati wa zoezi la kuhesabu watu. Jambo jingine la kuzingatia ni kuwepo kwa
mawazo au hofu dhidi ya zoezi la Sensa. Ni muhimu sana kuwatoa hofu wananchi
kwa kuwaelimisha kuwa zoezi la Sensa halihusiani kabisa na hofu au imani
walizonazo. Hamasa ifanyike hasa kwa
wanawake, wanaume, vijana, watoto na watu wenye ulemavu.
Ningependa muwahakikishie wananchi kuwa taarifa watakazozitoa wakati wa
Sensa zitakuwa siri na zitatumika kwa masuala ya kitakwimu pekee.
Nawasihi ndugu wananchi mtekeleze jambo hili.
SENSA KWA MAENDELEO: JIANDAE KUHESABIWA
No comments:
Post a Comment