Viongozi wa dunia katika mkutano wa kilele wa nchi saba zilizowendelea
kiviwanda ,kundi linalojulikana kama G7 leo wanaandaa lengo la pamoja
kuanzia mapambano na vitisho vya ugaidi kutoka kwa wapiganaji wa Jihadi.
Hatua hiyo imetiliwa mkazo vilevile kutokana na kile kilicholaaniwa na
Rais Barack Obama wa Marekani kuwa ni,” uchokozi wa Urusi nchini
Ukraine.” Mkutano huo ulioanza jana katika mji wa Elmau kusini mwa hapa
Ujerumani, haumshirikishi Rais wa Urusi Vladimir Putin ,ikiwa ni mara ya
tatu.
Viongozi wa kundi hilo la nchi saba zilizoendelea kiviwanda
G7,wamewaalika viongozi wengine nje ya kundi hilo, wakiwemo Waziri mkuu
wa Iraq Haider al-Abadi na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ambao wote
wawili wanapambana na makundi ya itikadi kali ya Kiislamu katika nchi
zao-Kundi linalojiita dola la Kiislamu-IS huko Iraq na Boko haram nchini
Nigeria.
Sauti ya Iraq kusikika
Waziri mkuu Abadi anatarajiwa kuzungumzia kampeni inayoongozwa
na marekani kuisaidia nchi yake kuyakomboa maeneo yanayoshikiliwa na
wapiganaji hao wa IS, ambalo limetangaza Dola la Kiislamu nchini humo na
katika nchi jirani ya Syria ambako pia inayadhibiti maeneo kadhaa.
Kwa upande wake Rais Buhari wa Nigeria aliyeshika madaraka Mei 29, baada
ya kumshinda Rais Goodluck Jonathan katika uchaguzi wa kidemokrasi,
anatarajiwa kuwasilisha orodha ya msaada kwa viongozi hao kupambana na
kundi la Boko haram linalolaumiwa kwa mauaji ya watu 15,000 tangu 2009.
Hapo jana siku ya kwanza ya mkutano wao, suala lililotawala lilikuwa ni
mzozo wa Ukraine, huku Rais Obama wa Marekani na mwenyeji wa mkutano huo
kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakiitaka jamii ya kimataifa
kusimama kidete dhidi ya Urusi hadi imeheshimu makubaliano ya kusitisha
mapigano nchini Ukraine yaliofikiwa katika mji mkuu wa Belarus-Minsk.
Wasiwasi wa Urusi
Ingawa Rais wa Urusi Vladimir Putin amesisitiza kwamba hakuna haja ya
kuihofia Urusi, kupamba moto karibuni kwa mapigano kunatia wasiwasi
kwamba makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliofikiwa kutokana na
juhudi kubwa za Ufaransa na Ujerumani miezi mine iliopita yanaweza
kuvunjika.
Merkel aliiambia stesheni ya matangazo ya televisheni ya ZDF kwamba ,
tunapaswa kutuma ujumbe mkali hapa na kuwa na vikwazo vitakavyofikia
malengo .
Suala jengine katika mkutano huo wa G7, ni mvutano baina ya Ugiriki na
wakopeshaji wake wa kimataifa-Umoja wa Ulaya, Benki kuu ya Ulaya na
Shirika la Fedha la Kimataifa,IMF- na hofu ya kwamba kufilisika kwa nchi
hiyo kutaisababisha kujiondoa katika kundi la nchi zinazotumia sarafu
ya euro , wakati athari zake kwa uchumi wa dunia zikiwa hazijulikani
zitakuwaje.
Wakati huo huo, Kansela Merkel na Rais Francois Hollande wa Ufaransa
wanatarajiwa kupigania kupatikane maridhiano ndani ya kundi hilo la G7
kuhusu suala jengine zito la kimataiaf-mabadiliko ya tabia nchi- kabla
ya mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa mjini Paris mwezi Desemba.
No comments:
Post a Comment