Katika mkutano wao na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, Zitto ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, ameapa kuwa hayuko tayari kuondoka ndani ya chama hicho na atakuwa mtu mwisho kuondoka.
Wakati Zitto akiapa kwamba hayuko tayari kuondoka CHADEMA, Dk. Mkumbo ambaye amekuwa mshauri mkuu wa chama hicho maarufu nchini, amesema kuwa kile kinachoitwa uhaini ndani ya CHADEMA ni wasiwasi wa siasa za ushindani kwa watu wasiotaka mabadiliko.
“Wengi walifikiri nikija hapa leo nitajibu mapigo na kutoa uamuzi mgumu. Mimi sitoki CHADEMA, wanaotaka nitoke, wanitoe wao, na hiki kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia dhidi ya wahafidhina, ni mapambano ya wanaopenda siasa safi dhidi ya wale wanaotukuza siasa za maji taka,” alisema Zitto.
Akieleza sababu za kutokujitoa CHADEMA, Zitto alisema zaidi ya nusu ya maisha yake yamekuwa CHADEMA, kwani alijiunga tangu alipokuwa na miaka 16 hadi sasa ana miaka 37, na amekabiliana na vitisho mbalimbali dhidi ya wasiotaka mageuzi.
“Nataka niwaeleze wanachama wa CHADEMA kwamba mimi sitokuwa sababu ya CHADEMA kuvunjika, kimenilea na kunifikisha hapa na ningependa na mwanangu siku moja awe mwanachama wa CHADEMA, na huu unaoitwa usaliti kwangu dhidi ya CHADEMA ni sawa na mimi kujikata mguu wangu, sitoweza kufanya hivyo,” alisema Zitto.
Mbunge huyo ambaye amepata umaarufu mkubwa tangu alipoingia bungeni, alieleza kuumizwa na shutuma nyingi ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kwa muda mrefu.
Alisema amekuwa akiItwa msaliti, mnafiki, mla rushwa akihongwa kwa ajili ya kukisaliti chama.
“Naomba wanachama wanielewe, nimejiunga na chama hiki nikiwa na miaka 16, ninaposingiziwa, naumia sana, nimefanya kazi ya kuchomeka milingoti ya bendera za chama kwa viongozi wanaofika katika kijiji chetu, ninapozushiwa naumia, nimefanya kazi zangu za kibunge kwa weledi mkubwa kwa nia ya kukitumikia na kukipandisha chama changu, ninaambiwa ninakihujumu, inaniuma sana,” alisema.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema akiwa mwanasiasa kijana na binadamu, anaamini ana makosa kwa kuwa hakuna binadamu aliye mkamilifu, na kwamba upungufu wake unapaswa kupimwa na mema aliyoyafanya.
Ataja tuhuma zake
Akizungumzia tuhuma zilizomfanya apokwe nyadhifa zake zote na kubaki kuwa mwanachama, Zitto alisema kuna upotoshaji mkubwa wa taarifa kwani tuhuma alizoambiwa ndani ya Kamati Kuu ni tofauti na zilizotolewa kwa waandishi wa habari.
Alisema tuhuma zote zimekuwa katika taswira mbili zinazomuonyesha kuwa ni mbinafsi na mtu anayetumiwa kukisaliti chama kwa kupokea rushwa kwa ajili ya kufanya hujuma.
Alisema anadaiwa kutoshiriki katika kampeni za mgombea urais mwaka 2010 tuhuma ambazo alidai zimekuwa zikijirudia kila wakati.
Akitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, Zitto alisema kuwa yeye ndiye kiongozi na mgombea ubunge pekee mwaka 2010 aliyezunguka majimbo 16 kumfanyia kampeni mgombea wa urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa na Mkoa wa Kigoma uliongoza kwa kutoa kura nyingi za urais kuliko mingine kwa kupata asilimia 46.
Kwa mujibu wa Zitto, tuhuma nyingine iliyoelekezwa kwake ni madai kuwa alishiriki kuwashawishi baadhi ya wagombea katika baadhi ya majimbo wajitoe katika uchaguzi ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.
Akijibu hilo, Zitto alisema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha hali hiyo, na kwamba aliomba uchunguzi ufanyike kubaini ukweli.
Mbunge huyo alisema pamoja na tuhuma zote, kuna tuhuma kubwa ya kudaiwa kukidhalilisha chama chake kwa kutoa tamko kwamba hesabu za chama hicho, hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba chama chake kilimtaka awafahamishe mapema ili wajiandae.
“Kwamba ‘kutowatonya’ kwangu ndio nimekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM, na kwamba nastahili kuadhibiwa kwani katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo. Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zilezile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha.
“Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani,” alisema Zitto.
Akizungumzia usaliti, alisema kuwa tangu alipoacha kuchukua posho mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chake wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma, alianza kuitwa msaliti.
Alisema suala la kukataa posho za vikao limo ndani ya Ilani ya CHADEMA na kwa upande wake kama waziri kivuli wa fedha alikuwa na wajibu wa kutekeleza jambo hilo kwa vitendo na sio kama alivyotuhumiwa na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, kwamba anachukua fedha nyingi sehemu tofauti.
Kuhusu ripoti ya siri iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, kwamba amehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama chake, alisema kuwa viongozi wenzake walikana kuuandaa na kuusambaza.
Alisema hoja iliyopo ni kuwa waraka huo umesambazwa na watu wa usalama kwa kushirikiana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kwa vile chama kimekana kuhusika, tayari anakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaohusika iwe ndani au nje ya chama hicho.
Waraka wa mabadiliko ya uongozi
Akizungumzia waraka wa siri unaoeleza mkakati wa mabadiliko ya uongozi CHADEMA ulionaswa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Zitto alisema hajawahi kuuona wala kuusoma na kwa mara ya kwanza aliusikia kwenye kikao cha Kamati Kuu.
Alipobanwa kueleza kama anakubaliana na mapendekezo ya waraka huo wa kumtaka agombee uenyekiti wa CHADEMA taifa wakati ukifika, Zitto alisema kwa bahati mbaya alichelewa kuuona na kama angeupata mapema, angeyafanyia kazi mapendekezo yake.
“Changamoto hizi tunazopitia zimewahi kupitiwa na wanasiasa mahiri duniani kama vile akina Mahadhir Mohammed aliyefukuzwa na baadaye akawa waziri mkuu, Mahindra Gandhi alifukuzwa akiwa waziri mkuu wa nchi aliondolewa na kwenye uongozi wa chama chake, Zuma, na watu walijua alikwisha kabisa, lakini matokeo sasa ndiye Rais wa Afrika Kusini, haya ni lazima kupitia katika kuhakikisha tunajenga demokrasia imara, siasa safi na uongozi bora katika nchi yetu,” alisema Zitto.
Kuhusu siku 14 alizopewa na Kamati Kuu kwa ajili ya kutoa utetezi, Zitto alisema hadi sasa hajapata barua ya mashitaka yake na kwa hali hiyo hajui anatoa utetezi gani.
Dk. Mkumbo amsafisha Zitto na waraka
Kwa upande wake Dk. Mkumbo ambaye alikuwa wa kwanza kuzungumza, alisema alikiri kuuandaa waraka huo kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Alisema waraka huo uliandaliwa kwa siri bila kumshirikisha Zitto, na kwamba hajui lolote kwani walipanga kumpelekea endapo chama kingetangaza tarehe ya uchaguzi.
“Ule waraka ulikuwa wa siri, unaelezea mikakati ya kuweka mgombea tuliyeamini kwamba ana sifa za kushika nafasi hiyo, baada ya kukamilisha tungeenda kwake kumwomba agombee, na tungemwonyesha waraka huo ambao unaainisha udhaifu na uwezo wake wa kuwa kiongozi, na hili ni jambo la kawaida na sio la uhaini maana tungetumia boksi la kura kumpata kiongozi,” alisema Dk. Mkumbo.
Katika waraka huo, Zitto alipewa jina la MM, M1 (Mkumbo), M2 ambaye hajulikani hadi sasa na M3 Samson Mwigamba.
Dk. Mkumbo Aliongeza kuwa hata kukiri kwake kwamba anaujua waraka huo kulikuwa na lengo la kuamini mawazo yake katika kupata viongozi ndani ya CHADEMA, aliyoeleza kuwa baadhi ya wajumbe waliutafsiri kuwa ni uhaini.
“Mimi ni miongoni mwa watu ninaoamini kuwa kuna haja ya kubadilisha uongozi wa juu wa chama, na kwa kuwa tulitambua uchaguzi huu ungefanyika kabla ya mwaka huu kuisha, tuliandaa sifa za mtu tuliyemuona anaweza kupokea kijiti na hili hata kwa hao wanaotafsiri ni uhaini limefanyika, sema kwa upande wao waliamua kuweka mkakati wao katika mitandao ya kijamii,” alisema Dk. Mkumbo.
Alisema kuwa hawezi kufanya uhaini wala kukihujumu chama kwani amepewa nafasi nyingi kubwa na kamwe hakuzitumia kukihujumu.
Akitolea mfano, Dk. Mkumbo alisema kuwa yeye ndiye aliyeandaa Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA katika uchaguzi uliopita, amemaliza mgogoro wa kupata viti maalumu ndani ya chama nafasi ambazo angeweza kuzitumia kukihujumu chama.
“Chama kiliniamini na kunipa nafasi nyingi nyeti, na kama ningekuwa mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo, nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010 nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa Baregu, na nilishiriki kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata wabunge wa viti maalumu katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti mno ambazo kamwe huwezi kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’,” alisema.
Alisema kuwa hata sababu ya kutaka kujiuzulu haikuwa kuogopa aibu ya kufukuzwa, bali ni baada ya kubaini wenzake katika Kamati Kuu hawakuwa na imani naye.
No comments:
Post a Comment