Thursday, November 21, 2013

KAMATI YA UTENDAJI YAMRUDISHA MADARAKANI RAGE MWANAUME WA SHOKA,

 

HATIMAYE kamati ya utendaji ya klabu ya Simba imebatilisha uamuzi wake wa kumsimamisha uongozi, mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.
Uamuzi huo umetangazwa mchana huu na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are 'Kinesi' alipokutana na waandishi wa habari Kinondoni, Dar es Salaam.
Awali, Kinesi alipanga kukutana na waandishi hao makao makuu ya klabu hiyo, mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, lakini akaamua kuhamishia kikao hicho nyumbani kwa mdhamini wa klabu, Hamisi Kilomoni.
Kinesi amesema, wamefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kwamba, kikao walichokiitisha na kutangaza kumsimamisha Rage, hakikuwa halali.
Kwa maana hiyo, hata uamuzi wa kumuondoa Kocha, Abdalla Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio' nao pia haukuwa sahihi.
Kamati ya Utendaji ya Simba ilitangaza kumsimamisha Rage kwa madai ya kutokuwa na imani na uongozi wake. Tuhuma zingine zilikuwa kufanya maamuzi binafsi bila kuishirikisha kamati ya utendaji na klabu kutonufaika na mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi.
Hata hivyo, Rage alipinga mapinduzi hayo kwa madai kuwa hayakuwa halali, kutokana na kamati ya utendaji kutompa nafasi ya kujitetea kutokana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Rage, ambaye wakati wa mapinduzi hayo alikuwepo safarini nchini Sudan, anatarajiwa kurejea nchini leo na amepanga kuitisha mkutano wa dharula wa wanachama Jumapili.

No comments:

Post a Comment