Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
amejibu madai yaliyotolewa hivi karibuni na Katibu wa Itikadi na Uenezi
wa CCM, Nape Nnauye kwamba ni mmoja wa mawaziri walioshindwa kazi, hivyo
kustahili kung’olewa.
Katika madai yake, Nape alisema Dk Kawambwa
ameshindwa kusimamia vyema madai ya walimu na kwamba akiwa Waziri wa
Miundombinu, aliingia mkataba na Kampuni ya ujenzi ya Progressive
iliyopewa zabuni ya kujenga Barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati
mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga.
Nape alikaririwa akisema kwamba umefika wakati kwa
waziri huyo na wenzake wa Fedha, Dk William Mgimwa; Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza; na Naibu wake, Adam Malima kuhojiwa na
Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.
Akijibu madai hayo Mjini Bagamoyo jana, Dk
Kawambwa alisema anasubiri kwa hamu kuitwa CC kueleza tuhuma
zinazomkabili huku akijigamba kuwa yeye ni mti wenye matunda ndiyo maana
unapigwa mawe.
Alisema hayo alipokuwa akikabidhi vifaa vya
michezo kwa timu 16 zitakazoshiriki michuano ya Kombe la Kawambwa
inayofanyika katika Jimbo la Bagamoyo ambalo yeye ni mbunge wake.
“Kuna maneno yanayoendelea hivi sasa eti na mimi
mbunge wenu natajwa kuwa fisadi kwa mkataba wa ukandarasi wa barabara,
siyo kweli. Wakati mkataba ule unasainiwa mimi nilishatoka kwenye Wizara
ya Miundombinu, sihusiki kabisa na mkataba ule,” alisema na kuongeza:
“Mwaka 2010 mimi ndiye niliyeshawishi Ubalozi wa
Japan ukatoa fedha kwa ajili ya mradi ule wa Barabara ya Namtumbo -
Tunduru lakini mkataba ukasainiwa Desemba 24, 2012 kati ya Wizara na
Kampuni ya Progressive.
“Walipovurunda Wizara ikawatimua, mimi sikuhusika
hata kidogo kwani wakati wanasaini mkataba ule mimi nilishahamishiwa
wizara nyingine.”
“Mimi nipo baridi, nasubiri kwa hamu kubwa kuitwa
kwenye Kamati Kuu, mimi si mtu wa kupiga kelele na tuhuma zote dhidi
yangu ninaamini si za kweli... wakati mwingine maadui wanatafuta njia za
kunichonganisha na chama changu.”
“Wanasema kila wizara ninayopelekwa ninavurunda,
nasema, mimi ni mti wenye matunda. Mti wowote ambao unazaa vizuri lazima
utapigwa mawe, nasubiri siku hiyo ya kuitwa CC ambako pumba na mchele
vitajulikana.”
Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo, Waziri
Kawambwa alisema anamshukuru Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
aliyemfukuza mkandarasi huyo Progressive kwa kushindwa kazi. Hata hivyo,
katika madai yake, Nape alisema kumfukuza mkandarasi huyo pekee
hakutoshi, bali aliyehusika kumpa mkataba naye anapaswa kuchukuliwa
hatua kwani uchunguzi unaonyesha kuwa alishashindwa kazi wakati anapewa
mkataba.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue alikaririwa na Gazeti la The Citizen akisema kuwa Chama Cha
Mapinduzi hakina mamlaka ya kuingilia utendaji wa Serikali kwani
kinatakiwa kuishia katika ngazi za watendaji wa chama.
No comments:
Post a Comment