Wednesday, August 7, 2013

UPINZANI WAMSHUKIA MWAKYEMBE

Na Ibrahim Yassin,Kyela

VIONGOZI wa vyama vya Siasa kambi ya upinzani Wilayani Kyela Mkoani Mbeya wamemtahadharisha Mbunge wa jimbo la Kyela ambaye pia ni  Waziri wa uchukuzi Dr,Harrison Mwakyembe kutimiza ahadi alizozito wakati akiomba kura kwenye  kampeni  za mwaka 2005 na 2010 vinginevyo yeye pamoja na Chama chake watakuwa wamejiweka rehani katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.
 
 Tamko hilo lilitolewa jana na umoja wa vyama vya Siasa kambi ya upinzani mbele ya vyombo vya habari ambapo viongozi wa vyama vi tano walipounda umoja huo na kutoa tamko la pamoja baada ya kuona Wilaya hiyo ikidumaa kwa kukosa maendeleo huku ahadi zilizotolewa na Mbunge huyo zikiwa hazitekelezeki na wananchi wakikosa fursa ya kuona matunda ya muwakirishi wao.
 
Gabriel Mwalukasa Mwenyekiti UDP Wilayani humo alisema kuwa anapenda kumkumbusha Dr, Mwakyembe kutimiza ahadi alizozitoa kwa wanakyela za kuleta maji safi,Barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe na viwanda vidogovidogo kwa ajili ya kupunguza ugumu wa ajira kwa vijana lakini alipoingia madarakani ameshindwa kutimiza ahadi hizo.
 
Haki Matola Katibu wa CUF Wilayani humo naye alimtaka Dr,Mwakyembe kuwatendea haki wananchi wake waliomuamini kwa kumpa kura kutimiza ahadi hizo ili waondokane na kinyongo walichonacho moyoni mwao na kuwa wao wanajiona kuwa hawana muwakirishi katika wilaya hiyo kwa kuwa fursa za maendeleo zinayumba huku yeye akiendelea kupata sifa Serikalini huku jimbo lake likiwa lipo hoi.
 
Willy Mwasyeka katibu wa NCCR Wilayani Kyela alisema kuwa Dr,Mwakyembe wakati wa kampeni za mwaka 2005 aliwaahidi wana nchi kuwa akipata ubunge ataweka viwanda vya kutengeneza juisi za matunda ili vijana wapate kujiajiri,lakini alipopata ubunge hakufanya hivyo na ilipofika mwaka 2010 alipokuwa akiomba kura tena aliwaeleza wana nchi kuwa ameshindwa kuweka viwanda hivyo kwa kuwa matunda wilayani humo ni ya msimu.
 
Aliongeza kuwa baada ya kuwaeleza wananchi kuwa miti ya  matunda yaliyopo ni ya msimu ndiyo maana hakuanzisha viwanda aliwaomba wananchi kwamba akipita tena ubunge atawaletea mbegu za matunda zinazokomaa kwa muda mfupi kutoka ulaya ili viwanda vya kusindika matunda atakavyoviweka viwe ndelevu lakini muda wa utawala wake unafikia kikomo na mbegu hizo hawazioni.
 
Mkama Mganji Mwenyekiti wa ADC Wilaya alimtaka Mbunge huyo kutimiza angalau ahadi moja tu ili kujinusuru yeye pamoja na Chama Chake Cha CCM kinachopoteza mvuto siku hadi siku kutokana na kukosa muelekeo kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu ya kawaletea wananchi maendeleo.
 
Mwiteni Mohammed katibu Chadema na Donald Mwaisango Katibu mwenezi Chadema Wilaya nao kwa upande wao walisema kuwa mbunge huyo ameshindwa kutimiza ahadi alizozitoa kwa wananchi wa Kyela kwa kuwa amepata sifa kubwa Serikalini akidhani kuwa sifa hizo zitawashawishi wana nchi wa kyela kumpa tena kura wakati wa uchaguzi ujao badala ya kuwaletea maendeleo yenye tija aliyowaahidi.
 
Walisema walifanya mikutano kadhaa katika vijiji vyote wilayani humo kilio kikubwa kwa wananchi wakielekeza kwa mbunge wao ambao wengi wao walianzisha vikundi vya ujasilia mali yaani Vikoba ambavyo vilianzishwa na mbunge huyo lakini havikumaliza hata mwaka mmoja Vikoba hivyo vimekufa na yeye hakuna hatua alizozichukua juu ya kufa kwa Vikoba hivyo.
 
Waliongeza kuwa atimize ahadi hizo alizozitoa vinginevyo yeye pamoja na Chama Chake atakuwa amejiweka rehani katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 kwa kuwa wananchi wa kyela wamekata tamaa juu ya mbunge huyo pamaja na chama chake kuleta msukumo wa maendeleo katika jimbo la Kyela.
 
Walizitaja ahadi alizozitoa mbunge huyo kuwa ni kuleta viwanda vya kutengeneza matunda,kiwanda cha kusindika mpunga pamoja na kutafuta soko,kuboresha zao la Kakao,kuanzisha vikundi vya wajasilia mali (Vicoba),kuinua kiwango cha elimu,kusambaza bomba za maji safi na salama,Barabara vijijini, kuliboresha soko kuu, kujenga Benk ya Vicoba na zinginezo lakini hakuna hata ahadi moja kati ya hizo aliyoitekelaza.
 
Mbuge wa jimbo hilo Dr,Harrison Mwakyembe alipopigiwa simu kujibu malalamiko hayo simu yake haikupatikana Tanzania Daima inaendelea kuwasiliana naye ili kupata majibu juu ya sakata hilo.
Mwisho.
 

No comments:

Post a Comment