CHAMA cha watoa huduma za mitandao (intaneti) Tanzania (TISPA)
kimeilalamikia sheria mpya ya kodi na ushuru wa bidhaa hiyo
iliyotangazwa hivi karibuni na serikali kwa kusema itachangia ongezeko
la gharama za huduma hiyo kwa watumiaji wa kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa TISPA, Gregory Almeida, alisema kuongezeka kwa gharama
hizo kutafanya jitihada za kufikisha huduma hiyo nchini kufifia.
Alisema hoja ya ongezeko hilo la asilimia 14.5 katika huduma za
mtandao itakuwa ni moja ya sababu kuu katika kuongeza gharama za huduma
ya intaneti kwa wananchi kwa kuwa kodi hii itapita moja kwa moja kutoka
kwa watoaji huduma hiyo.
“TISPA inapenda kuharifu umma kwamba bei za huduma hii zitapanda kwa
asilimia 14.5 zaidi ikiwa na ziada ya kodi ya mapato ya asilimia 18
ambayo atabebeshwa mtumiaji wa mwisho wa huduma. Hali hii inatokana na
serikali kupandisha gharama,” alisema Almeida.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, walitarajia kabla ya kutangazwa kwa
ongezeko hilo, serikali ingefanya mazungumzo na wadau kwa lengo la
kupata mawazo yao kabla ya uamuzi iliouchukua.
Katibu wa TISPA, Frank Goyayi alisema ongezeko la kodi katika huduma
hiyo itazorotesha wanachama wao katika kusambaza huduma hasa maeneo ya
vijijini na hivyo kusababisha kurudi nyuma katika kufikia malengo ya
milenia ya kupunguza umasikini kwa kutumia teknolojia ya intaneti.
No comments:
Post a Comment