RAIS Barack Obama wa Marekani akiwa katika ziara
yake Afrika Kusini ameshauri viongozi wa Afrika na duniani kwa jumla
kufuata mfano wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela kwa
kulitanguliza mbele taifa kabla ya nafsi yake.
Obama alisema kama viongozi wanashikilia nyadhifa hizo kwa muda na
wasidanganyike kiasi cha kufikiri kwamba hatima ya nchi yao haitegemei
kadiri watakavyoendelea kuwa madarakani. Obama alikuwa akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari uliomjumuisha pia Rais Jacob Zuma
mjini Pretoria akiwa katika ziara yake ya wiki moja barani Afrika ambayo
tayari imemfikisha Senegal na anatazamiwa kuzuru Tanzania hapo
Jumatatu.
Obama anafanya ziara hiyo wakati nchi nyingi za Kiafrika zikiwa
kwenye mizozo ya kidini, kikabila na mengineyo. Obama ameamuwa kukwepa
kuizuru Kenya kwa sababu ya nchi hiyo kuhusika kwenye mzozo wa
kimataifa. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imemfungulia mashtaka Rais
Uhuru Kenyatta kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu yakiwemo mauaji kuhamisha
watu kwa nguvu, ubakaji, ukandamizaji na vitendo vya kinyama
vilivyofanywa na wafuasi wake kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa
mwaka 2007 nchini Kenya.
Obama amekaririwa akisema “Wakati sio muafaka akiwa kama rais wa
Marekani kuitembelea Kenya wakati masuala hayo yakiwa bado yanafanyiwa
kazi na nataraji yatapatiwa ufumbuzi.” Amesema tayari ametembelea Kenya
mara kadhaa na ataitembelea tena nchi hiyo kipindi cha usoni.
Obama na Zuma walikuwako kwenye Majengo ya Umoja ambako ndiko kuliko ofisi za serikali na ndiko mahala ambapo Mandela alikoapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini hapo mwaka 1994 baada ya kuwa gerezani kwa miaka 27 kwa harakati zake za kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.
Obama na Zuma walikuwako kwenye Majengo ya Umoja ambako ndiko kuliko ofisi za serikali na ndiko mahala ambapo Mandela alikoapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini hapo mwaka 1994 baada ya kuwa gerezani kwa miaka 27 kwa harakati zake za kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.
Mandela mwenye umri wa miaka 94 amelazwa katika hospitali mjini
Pretoria kwa wiki tatu sasa kutokana na maambukizi ya mapafu. Zuma
amewaambia waandishi wa habari hali ya Mandela ni mbaya lakini imara na
kwamba taifa zima linamuombea apone.
Obama na mke wake wamekutana na baadhi ya ndugu wa familia ya Mandela
lakini kutokana na matakwa yao hakupanga kumuona Mandela ambaye ni
mmojawapo wa watu adhimu kabisa duniani. Obama akimtaja Mandela kwa jina
lake la kiukoo amepongeza mjumuiko wa kijamii wa Afrika Kusini kutoka
utawala wa kibaguzi na kusema kuwa ni alama inayon’gara duniani.
Obama amesema mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi kwa ajili ya
uhuru, moyo ya uadilifu wa Madiba kipindi cha nchi cha kihistoria cha
taifa hilo kubadilika na kuwa huru na la demokrasia yamekuwa ni mambo
yaliomshajiisha yeye mwenyewe binafsi na kuwa kichocheo kwa dunia.
Zuma amemwambia Obama kwamba yeye na Mandela wamefungamanishwa na
historia kwa kuwa marais wa kwanza weusi kwa nchi zao na kwa kuwasilisha
matumani ya mamilioni ya watu barani na Afrika na wale wanaoishi nje
ambao huko nyuma walikuwa wakikandamizwa.
Katika masuala mengine Obama amekataa kujifunga moja kwa moja katika
kuunga mkono juhudi za Afrika Kusini kuwania kiti cha kudumu katika
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesema mfumo wa Umoja wa Mataifa
unahitaji kurekebishwa na litakuwa sio jambo la kawaida kulitanuwa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bila kujumuisha uwakilishi wa
Afrika.
Obama pia amesema anataka kuimarisha biashara na Afrika na kuanzisha
mazungumzo mapya ya mkataba wa biashara na Afrika ili kuuboresha kwa
kampuni za biashara za Marekani. Pia amesema anakaribisha juhudi kubwa
zinazofanywa na nchi nyengine kutafuta fursa za biashara barani Afrika
ikiwemo China.
Amesema hatishwi na jambo hilo na anafikiri ni zuri ila tu ushauri
wake ni kuhakikisha tu kwamba ni kwa ajili ya manufaa ya Afrika kwa
kuhakikisha miradi ya uwekezaji ya kigeni inawaajiri Waafrika,
haindekezi rushwa au kuchukuwa rasimali zake za asili bila ya kuwafidia
Waafrika.
Obama pia ametowa heshima zake kwa mapambano dhidi ya utawala wa
ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini kwa kutembelea kitongoji cha
Soweto ambapo amehutubia wanafunzi katika ukumbi wa jiji wa Chuo Kikuu
cha Johannesburg. Takriban vijana 176 wameuwawa katika kitongoji cha
Soweto wakati wa maandamano ya vijana dhidi ya marufuku ya utawala wa
ubaguzi wa rangi ya kufundisha lugha za kienyeji za Kibantu. Uasi wa
Soweto uliimarisha uungaji mkono wa kimataifa dhidi ya utawala wa
ubaguzi wa rangi na mwezi wa Juni hivi sasa unatambulika kuwa ni Mwezi
wa Vijana nchini Afrika Kusini.
Obama atakamilisha ziara yake Afrika Kusini Jumapili ambapo anapanga
kutowa hotuba kubwa kuhusu sera ya Marekani kwa Afrika katika Chuo Kikuu
cha Cape Town na ataipeleka familia yake katika kisiwa cha Robben
kuzuru gereza ambalo Mandela alitumikia miaka 18 ya kifungo chake cha
miaka 27 gerezani.
No comments:
Post a Comment