Wednesday, June 5, 2013

KIJANA AKAMATWA MSIKITINI AKITAKA KUMTAPELI IMAMU NA WAUMINI IRINGA





IKIWA ni siku chache zimepita toka kuumbuliwa kwa tapeli mzee aliyekuwa akijifanya hana mikono katika eneo ya Mikyomboni mjini Iringa ,wimbi la utapeli laendelea kutikisha mkoa wa Iringa baada ya matapeli hao kuja na mbinu mpya ya kuingia katika nyumba za ibada na kuwatapeli waumini .

Mbinu hiyo imebainika leo katika msikiti wa Ijumaa - Miyombini baada ya waumini wa msikiti huo kumnasa kijana Wiliam Daud mkazi wa Majengo mkoani Katavi ambae amekuwa akifanya kazi ya utapeli katika misikiti mbali mbali hapa nchini kwa kutumia jina la Hassan Idd Lumbanga (jina la kutapeli) ambalo amekuwa akilitumia misikitini pekee.


Kama ilivyo ada siku zote za mwizi ni arobaini basi hivi ndivyo ilivyokuwa kwa kijana huyo baada ya jana kufika katika msikiti huo na kuungana na waumini wake katika swala na wakati shughuli hizo za swala zikiwa katikati kwa naibu imamu wa msikiti huo Issa Boki akiendelea kuongoza waumini hao ghafla kijana huyo tapeli alijiangusha chini mfano wa mtu aliyezidiwa na kupoteza fahamu .

Hali hiyo iliwalazimu waumini hao kusitisha shughuli za ibada na kutafuta gari haraka haraka na kumkimbiza katika Hospitali ya mkoa kijana huyo tapeli .

Alisema naibu imamu huyo Issa Boki alipozungumza na mtandao huu wa www.matukiodaima.com kuwa baada ya kufika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa kijana huyo alitakiwa kulazwa kutokana na kuonyesha kuzidiwa zaidi.

Hata hivyo baada ya wao kuondoka Hospitali hapo na kijana huyo kupelekwa wodini kulazwa inadaiwa alionekana ni mtu kama mwenye utindio wa ubongo kutokana na vurugu alivyokuwa akiwafanyia wagonjwa wenzake kiasi cha kuhamishwa na kupelekwa katika wodi la vichaa ambako pia alifanya vurugu kubwa na kufanikiwa kutoroka wodini hapo.

Alisema kuwa katika hali ya kushangaza ni pale tapeli huyo aliporudi tena msikitini hapo leo na kuungana na waumini hao katika swala ya mchana wa leo na kuwaomba waumini hao kumsaidia fedha ili kurejea kwao Katavi .

Kutokana na maombi hayo Naibu Imamu huyo aliwaomba waumini wake kumchangia fedha na kupatikana kiasi cha Tsh 55,200 na wakati wakijiandaa kumkabidhi fedha hizo mmoja kati ya waumini aliweza kumtambua kijana huyo kuwa ni tapeli ambae amekuwa akitumia mbinu hizo na kwa mara ya mwisho alikuwa jijini Dar es Salaam katika msikiti mmoja na kunusurika kichapo kwa utapeli huo wa kujiangusha na baada ya siku moja kurejea kuomba fedha ili arejee kwao.

Katibu wa Msitiki huo Juma Kibasila alisema kuwa fedha hizo hawajaweza kumkabidhi tapeli huyo baada ya kumhoji na kukiri kuwa si mgonjwa ila amekuwa akiendesha maisha yake kwa kutapeli katika nyumba mbali mbali za ibada kwa kutumia mbinu hiyo ya kujiangusha kama mgonjwa .

Kibasila alisema kuwa kwa ujumla waumini wa dini ya Kiislamu ni watu wa kujitolea kwa watu wenye shida na kuwa iwapo kijana huyo angefika na kuomba msaada kama msaada bila kutumia mbinu ya utapeli kama hiyo hakukuwa na tatizo ila kutokana na utapeli huo wamelazimika kumfikisha polisi kutokana na kudai kuwa ana miliki funguo malaya zinazofungua milango mbali mbali ya nyumba na magari hivyo wanahisi ni mtu hatari zaidi .

Kijana huyo baada ya kuhojiwa na mtandao huu alikiri kuwa ni tapeli anayetafuta maisha kwa mbinu hiyo na kuwa amefanya utapeli huo katika misitiki ,makanisa na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu wengi na kusaidia na kuwa kila anapofanya utapeli kama huo huwa hakosi kiasi kati ya Tsh 50,000 hadi 500,000 kwa tukio moja .

Hata hivyo alisema katika Misitiki amekuwa akitumia jina hilo la Hassan Idd Lumbanga ila anapokwenda makanisani amekuwa akitumia jina la Wiliam Daud .

No comments:

Post a Comment