Tuesday, June 4, 2013

JWTZ YAWATOA HOFU WANANCHI



JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewaondoa hofu wananchi kutokana na ujumbe unaotumwa kupitia simu za mikononi kuwa kuna bomu limerushwa kutoka nchini Malawi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Makao Makuu ya Jeshi, ilieleza ujumbe huo haujatolewa na JWTZ na kwamba haiwezi kutumia mfumo huo kuwapa wananchi taarifa za hatari kama hizo.


Taarifa hiyo ilieleza kuwa JWTZ hutangaza kupitia vyombo rasmi kama vile magazeti, radio na televisheni.

Jana kulikuwa na ujumbe umesambazwa kwa wananchi mbalimbali ukisadikishwa kuwa unatolewa na JWTZ.

 Ujumbe huo unasema: “Habari zilizotufikia hivi punde. Mtanzania yeyote, kaa makini usiokote kitu chochote ambacho una shaka nacho, kuna mabomu yamerushwa toka nchi jirani Malawi zaidi ya 30 yenye uzito usiopungua tani 100. Hivyo basi uonapo kitu kiko kama chupa ya chai chenye rangi ya fedha usikiguse.”

“Piga namba 0756 000042. SMS hii tuma kwa watu uwezavyo. Imetolewa na JWTZ.”

Iliendelea kueleza kuwa mzinga wa aina hiyo hauko duniani kote na wala hakuna ndege yenye uwezo huo, hasa kwa bomu lenye umbile dogo kama hilo (chupa ya chai).

“Habari hizi hazina ukweli kisayansi wala kiuhalisia au fikra za kawaida. Tunawaomba wananchi wazipuuzie taarifa hizi. JWTZ iko kwa ajili ya wananchi hivyo, kwa taarifa hizi za hatari, lazima ingewajulisha wananchi kwa njia ilizoeleza na si kwa simu za mkononi,” ilieleza taarifa hiyo.



No comments:

Post a Comment