Tuesday, March 12, 2013

WATOTO HESHIMA YAZIDI BARAKA KWA WALEZI


 Watoto wengi hasa wale wa shule za awali (chekechekea) na shule za msingi kote nchini zikiwa ni zile za watu wenye vipato vikubwa michepuo ya kiingereza au wale wa shule za sisi akina bora kumekucha wana hekima sana.

Hekima za watoto wetu hao inajionesha hasa pale mmoja wao anaponunua hata kitumbua kimoja na kuweza kuwagawia wenzake hata wawe kumi.

Ni kitu kinachoonekana ni kidogo sana lakini hiki ni kitu kikubwa sana kwasababu kinaonesha upendo na kuwa na mtazamo wa mbele kuwa kuna siku huyo aliyenunua leo kesho atakwama hivyo akiwagawia wenzake naye watamgawia kesho na siku zijazo.

Lakini kitu kama hicho kwa watu wazima wa enzi hizi ni kigumu kukiona na kukifanya kutokana na kila mtu kujijali mwenyewe.

Kwa wenzetu wakristo wanajua mifano hii kimaandiko hasa ukisoma katika Biblia kitabu cha 1 Wakorintho 10;23-24 ambako inasema kuwa ‘’Vitu vyote ni halali;bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali bali si vitu vyote vijengavyo. Mtu asitafute faida yake  mwenyewe, bali ya mwenzake’’ mwisho wa kunukuu.

Kwa watoto hao hao, ukiwaambia wajisaidie kwenye sufuria ambayo anajua kuwa inatumika kusongea ugali hawezi kukubali lakini watu wazima wa enzi hizi wapo tayari kufanya hivyo mradi tu aliyewaambia ni mwanasiasa ambaye hata yeye hafanyi.

Hata ukimuuliza  kwanini imekuwa hivyo au amefanya hivyo si jambo lahisi kukiri na kutubu bali atakachokifanya ni kujitetea huku akisahau kuwa dawa ya dhambi siyo kujitetea bali ni kutubu.

Ndivyo ilivyo hivi sasa hasa kwa watu wazima wa enzi hizi ambao wanajificha kwenye kivuli cha kuwa wao ni wanaharakati huku wakitumia vibaya uhuru wa siasa uliopo kwa nguzo ya kuimarisha demokrasia.

Nikiwa safarini kuelekea mkoani Mara tarehe 19.02.2013 nilikuta pale Jijini Mwanza kuna msongamano wa watu jioni hasa eneo la Ghana huku vijana wengine wakiwa wamevua mashati huku jasho likiwatoka.

Kwa macho niliona baadhi wamevaa sare za Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadhi wakawa wamevaa nguo zenye rangi anazopendelea kuvaa mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe zile zenye rango ya kaki.

Nilipofuatilia kuwa ilikuwaje nikaambiwa kuwa walitoka kwenye mkutano aliohutubia Mbowe siku hiyo hivyo walikuwa wakirudi makwao kwa maandamano ambapo kila mmoja atakapochoka anachomoka kwenye maandamano hayo ambayo nilielezwa kuwa hayakuwa rasmi bali ulikuwa ni mzuka wa ushabiki…

Nilijaribu kudodosa zaidi na baadaye majira ya saa mbili za usiku nikaona taarifa ya habari iliyoonesha mkutano huo na kwamba Mbowe alitoa siku 14 kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr. Shukuru Kawambwa awe amejiuzulu.

Mbowe aliyasema hayo kwa uchungu sana akisema kuwa anatoa tamko hilo kutokana na kufeli wanafunzi wa kidato cha Nne 2012 huku akishindwa kutoa suluhu ya tatizo husika.

Wakati zimebaki siku tatu kutimia siku 14 alionekana tena kwenye Luninga na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini akinukuliwa kuwa sasa yeye na wenzake wataandamana nchi nzima.

Hapo alikuwa mkoani Mbeya ambapo sihitaji zadi kuzungumzi safari yake ilivyokuwa kwasababu sihitaji kumfananisha na mtu anayekula matapishi yake.

Lakini ngoja nigusie kidogo kuwa alisafiri kutoka Jijini Dar es Salaam na ndege na kutua katika uwanja wa ndege wa Songwe uliopo nje kidogo ya Jiji la Mbeya huku gari lake likitumia mafuta ya walipa kodi kutoka Dar es Salaam na dereva wake.

Hivyo hivyo baada ya mkutano wake alirudi kwa ndege huku gari hilo tena la Serikali likirejea Dar es Salaam na dereva na mafuta yakiedelea kutumika.

Swali linabaki kuwa je ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma wanaoupinga viongozi wa Chadema na hata CCM tofauti yake ni ipi? Hapa binafsi ni kwamba naungana mkono na wale wanaosema kuwa waliopo madarakani hatuwataki lakini wanaotaka kuja hatuwaamini kabisa.

Katika mkutano huo aliwachangisha wafusi wa chama hicho zaidi ya Shilingi Milioni tatu kwa madai kuwa fedha hizo zitatumika katika kununua maji ya kunawa ili kupambana na polisi katika maandamano yaliyotarajiwa kufanyika.

Usihoji kuwa fedha hizo zipo wapi au akaunti ipi kwa manufaa ya nani. Kwani tulio wengi hatuamini kuwa ndani ya Chadema kuna mafisadi na mtapeli wanaotumia njia za kisayansi kama vilivyo vyama vingine na hata CCM inayoshutumiwa kwa kila aina ya ‘’uchafu’’.

Hao ndiyo watu wazima wa enzi hizi ambao hawawezi kuhoji wala kuwaza mema badala ya mabaya huku wakitanguliza ubinafsi badala ya maslahi ya taifa.

Hawajaweza kuhoji kuwa kwanini tununue maji ya kunawa kuzuia mabomu na kupambana na polisi badala ya kuomba kibali cha maandamano na kutoa kero zao, hawawezi kuhoji kuwa kwanini maandamano yasianzie Moshi safari hii badala ya Mwanza, Mbeya na Arusha!

Wanashindwa kufanya hivyo kwasababu wengi wamezoea kufikiriwa badala ya wao kufikiri na kujega mashaka, hao ndiyo watu wazima wa enzi hizi.

Nampongeza sana bosi wangu Freeman Mbowe kwa kuendelea kuangalia uelewa wa watu anaowaongoza na hata kufikia hatua ya kuwaambia ukweli kuhusu uelewa wao mdogo wa kiutawala ndani ya vikao vya ndani na kuwaeleza kuwa hawawezi kutawala nchi wala kushika dola kwa siasa za harakati.

Hayo aliyaeleza akiwa katika kikao cha ndani ukumbi wa mikutano wa Mkapa uliopo Jijini Mbeya kabla ya mkutano wa hdhara aliowachangisha mamilioni wenye tamaa ya kuandamana bila kujua kuwa matokeo yake ni nini wakiandamana au wasipoandamana.

Sidhani kama kuna RPC wa mkoa wowote atakayekubali kuulizwa na Mungu siku ya mwisho kuwa alipokuwa kamanda wa Polisi katika mkoa huo alifanyaje kuruhusu maandamano ya watu waliotoka katika mikoa ya jirani na kuharibu mali na uporaji wa kijinga huku yeye akiangalia bila kuwajibika katika hilo hakika naye tutamwekea maandamano ya kujiuzulu.

Sishawishi kuwa wakuu hao wa polisi wazuie maandamano yenye hoja lakini katika maandamano haya ambayo watu wanajiandaa kufanya fujo na tayari wametamka hadharani kuwa siku hiyo wamejipanga kupambana na polisi, hapana tuwe wakweli na hapa tuwe kama watoto wadogo si kama watu wazima wa enzi hizi.

Hebu kwa pamoja tujiuluze kuwa, bahati mbaya yakatokea machafuko hapa nchini nani atakayeweza hata kushauri au kutuliza ghasia kwa kuheshimika na jamii? Je sampuli za watu wazima wa enzi hizi wanaweza? Tutafakari na tuseme imetosha kuburuzwa bali tufikiri kwanza hata kama wao watasema…

No comments:

Post a Comment