Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu
Ikiwa ni siku chache tu tangu dunia ilipoadhimisha
Siku ya Wanawake Machi 8 mwaka huu, mauaji ya wanawake yameendelea
kushika kasi nchini, ambapo katika kitongoji cha Senta A, katika kijiji
cha Bupandwa, wilayani sengerema, mkoani Mwanza mwanamke mmoja ameuawa
kikatili kwa kukatwa mapanga kisha mkono wake kuondolewa baada ya
kuvamiwa nyumbani kwake na watu
wasiojulikana.
Aliyeuawa ametambulika kwa jina la Juliana Masele (55) mkazi wa
kijiji hicho ambaye alivamiwa nyumbani kwake majira ya saa 2:30 usiku wa
kuamkia jana na watu wasiojulikana wakati akila chakula cha usiku na
watoto wake wanne.
Baada ya watu hao kumvamia walimkata kwa mapanga sehemu mbalimbali
za kichwa kisha kuukata mkono wake wa kushoto hadi kudondoka chini hali
iliyosababisha kutokwa na damu nyingi zilizopelekea mauti yake.
Akizungumza na NIPASHE, mmoja wa watoto wa mama huyo ambaye
alishuhudia tukio hilo, Masele Japhet, lilitokea wakati mama yake akila
chakula cha usiku na watoto wake ambapo watu
wasiofahamika waliwavamia na kufanya mashambulizi hayo kwa
kutumia mapanga huku wakiwa wamevalia makoti marefu na kufunika nyuso zao mithili ya ninja.
Alisema baada ya kumjeruhi mama yao watu hao waliondoka pasipo
kuchukua kitu chochote wala kumdhuru mtu mwingine na kwamba hakuna
taarifa zozote walizoziacha hivyo hawajafahamu chanzo cha watu hao
kuamua kufanya mauaji ya mzazi wao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Vicent Thobias, alisema unyama huo
ulifanywa na watu wawili waliokuwa na silaha za jadi ambao baada ya
kutekeleza mauaji hayo walitoweka na kutelekeza panga moja lililotumika
kwenye mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu amethibitisha
kutokea kwa mauaji hayo na kwamba jeshi lake linaendelea na upelelezi
ili kubaini waliohusika na unyama huo ili waweze kufikishwa mahakamani
No comments:
Post a Comment