Wajawazito
Tanzania wakimbilia unafuu Malawi
WAZIRI WA AFYA DK.HUSSEN MWINYI
Na
Gordon Kalulunga
SERA ya Afya ya mwaka 2007 haifahamiki wilayani
Ileje katika mkoa wa Mbeya. Ni katika sera hii ambamo inatamkwa kwamba
wajawazito nchini watapewa huduma za afya bure.
Kama sera inafahamika, basi haitekelezwi. Baadhi
ya wajawazito katika wilaya ya Ileje wanaacha zahanati, vituo vya afya na
hospitali wilayani mwao na kuvuka mpaka hadi nchini Malawi kufuata kinachoitwa
“huduma bora.”
Kwa mfano, wajawazito kutoka kata za Bupigu,
Itumba na Isongole wanafahamika kwa kwenda nchini Malawi kwa wingi ili waweze
kujifungulia huko na kupata huduma nyingine za afya.
Lakini kutoka Isongole hadi hospitali maarufu ya
Chitipa nchini Malawi ni umbali wa kilometa 45; wakati umbali wa kwenda
hospitali ya serikali ya Ileje ni kilomita tatu tu.
Mwanamke mkazi wa kijiji cha Ikumbilo, kata ya
Chitete wilayani Ileje, aliyejitambulisha kuwa anaishi na virusi vya ukimwi (VVU)
anasema aliwahi kujifungulia hospitali ya Chitipa na mpaka sasa anapata
matibabu yake huko.
Kuna nini katika hospitali ya Chitipa nchini
Malawi hadi wajawazito wakimbilie huko? Jibu analo Neema Mbughi mkazi wa kijiji
na kata ya Bupigu.
“Pale hospitali ya Chitipa hubebi chochote wakati
unakwenda kujifungua. Hatuendi na madishi, karatasi za nailoni (ambako mjamzito
huhala wakati wa kujifungua) wala glovu. Kila kitu ni bure, hata chakula
ambacho kimepikwa kama kimetoka nyumbani,” anaeleza Neema.
Wilaya ya Ileje ina hospitali kubwa mbili –
hospitali ya serikali mjini Ileje na ile ya misheni ya Isoko. Hizi ndizo
hospitali ambazo zinategemewa kwa huduma ya uzazi.
Wanawake wapatao 27 waliohojiwa, pamoja na
kutofautiana katika mambo mengine, wengi waliafikiana kuwa katika hospitali ya Chitipa,
wauguzi wanatumia “lugha nzuri” inayompa matumaini mjamzito.
Sababu nyingine walizotaja ni kutotozwa fedha
yoyote ikiwa gharama kwa kujifungulia hapo; kupewa dawa zinazohusiana na uzazi
bila kulipia na kupewa chakula bure.
Hivi wanapitaje mpakani penye idara ya uhamiaji?
Jibu unalopewa ni kwamba hawapiti mpakani kwenye ofisi za serikali. Wanapita
vichochoroni ambako wanaita “njia za panya.”
Bali wakifika hospitalini Chitipa wanajieleza kuwa
wanatoka vijiji vya ndani ya Malawi – wengine wakitaja hata ndugu zao na
viongozi katika maeneo hayo kuthibitisha kuwa wanatoka humohumo.
’Neema anasema wanalazimika kusema kuwa wanatoka
Malawi “…ili tuweze kupata huduma za kliniki, mahali bora na bure pa
kujifungulia na matibabu mengine.”
Siyo wajawazito peke yao wanaoingia Malawi kwa
matibabu. Wananchi wengine huenda hospitali za Chitipa na Kameme kupata matibabu;
tena bila kutozwa fedha zozote.
Henry Kayuni, mkazi wa Bupigu anasema licha ya
kufuata matibabu na mahitaji mengine kama mafuta ya taa, mbegu za mahindi,
sukari na mbolea, baadhi yao wanapeleka pia watoto wao shuleni.
Anasimulia kwamba kujieleza kuwa unatoka Malawi
kunasaidia “…hata kusomesha watoto nchini humo mpaka Darasa la VIII. Baada ya
hapo wanakuwa tayari wamejua vema Kiingereza; ndipo wanahamishiwa Tanzania na
kuwaombea nafasi Kidato cha II.”
Lida Kibona wa kijiji cha Itumba, anasema yeye
alianza kupata matibabu bure katika hospitali ya Chitipa hata kabla hajapata
ujauzito na kwamba manesi ya madaktari “wanasikiliza na kujali sana wagonjwa.”
Kuna kichocheo kingine kwa wananchi wa Tanzania
kutibiwa Chitipa. Katika mahojiano nao Novemba mwaka jana walieleza, mmoja
baada ya mwingine, kuwa ikitokea “bahati mbaya” mama au mtoto akafariki na
wakati huo umejitambulisha kuwa unatoka Tanzania, basi inasafirishwa hadi mpakani
bila gharama yeyote.
Katika hospitali za mkoani Mbeya karatasi la
kutandika wakati wa kujifugua linauzwa kwa Sh. 3,000, paketi ya glovu Sh. 2000,
beseni Sh. 3,000 na kama mjamzito amelazwa, basi hujitegemea pia kwa chakula.
Jane Kabuje mkazi wa kata ya Isongole anasema kuwa
yeye ni mmoja wa wanawake wanaopata huduma za afya Chitipa nchini Malawi ingawa
hospitali ya wilaya ya Ileje ipo ndani ya kata yake.
Mkazi wa Bupigu wilayani Ileje, Amos Shimwela anasema
tatizo linalowakumba wakazi wa vijiji vya mpakani hadi kuamua “kujitambulisha” kama
raia wa Malawi, ni kutokana na kutopata huduma za afya nchini ambazo alisema ni
ghali wakati nchini Malawi ni bure.
Naye mkazi wa kijiji cha Bulambya, Joseph Kapange
anasema bora kujitambulisha kuwa ni raia wa nchi nyingine ili upate huduma,
kuliko kung’ang’ania utokako ambako hupati huduma muhimu kwa afya yako.
Anasema wakati matibabu katika hospitali ya
Chitipa na huduma kwa wajawazito ni bure, nchini Tanzania bado wanatozwa fedha
na wengi wanashindwa hata kulipa Sh. 500 ili kupewa kadi ya kumwona daktari.
Hata wanaomudu kulipa kiasi hicho cha fedha, bado wanalazimika
kununua dawa katika maduka nje ya hospitali.
Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama
Minga, anasema baadhi ya wanaume wamekuwa wakipeleka wake zao wajawazito katika
hospitali ya Chitipa miezi mitatu kabla ya kujifungua.
Amesema hii ni kwa tahadhari kwa vile wanaishi
mbali na hospitali hiyo; na kwamba hawataki kusubiri hadi wajawazito wazidiwe,
“…kwani usafiri wa barabara siyo wa uhakika.”
Mwandishi wa makala aya anapatikanakwa simu 0754
440749 barua pepe kalulunga2006@yahoo.com
na website; kalulunga.bogspot.com
No comments:
Post a Comment