RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
amesema kuwa Serikali yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano,
zitaendelea kushirikiana katika kuendeleza na kuulinda muungano
ulioipatia sifa Tanzania kutokana na kuimarika kwake.
Dk Shein aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya
miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Aman
mjini Zanzibar.
“Muungano wetu upo imara na umepata heshima kubwa
sana katika mataifa mbalimbali, Serikali zetu mbili zitaendelea
kushirikiana katika kuendeleza muungano wetu na kamati za pamoja za
kushughulikia kero za muungano, zitaendelea kuyapatia ufumbuzi yale
ambayo wameanza kuyashughulikia,” alisema Dk Shein.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais Dk
Mohammed Gharib Bilali, Dk Shein alisema kwamba Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar umekuwa mfano wa kuigwa, ndani na nje ya nchi kutokana na
mafanikio yaliyofikiwa kiuchumi na kisiasa.
“Muungano huu umekuwa chachu ya maendeleo kwa
Wazanzibari, ndiyo maana Serikali ya Umoja wa Kitaifa itaendelea
kuudumisha. Nafahamu kuna changamoto za Muungano, ambazo Ofisi ya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano inazishughulikia. Tunachotakiwa ni
kuendelea kuudumisha, ili ushirikiano wetu uzidi kuwa imara kwa faida
na maslahi ya Watanzania wote,” alisema Dk Shein.
Dk Shein pia aliwakumbusha wananchi umuhimu wa
mapinduzi yaliyotokea Januari 12, 1964, akisema mapinduzi hayo
yamerudisha utu na heshima ya Wazanzibari, ambao sasa wanaishi kwa
mshikamano na maelewano.
Dk Shein aliwataka wananchi wote wa visiwa hivyo
kufanya kazi kwa bidii, ili kujiletea maendeleo kama sehemu ya kumuenzi
Mzee Abeid Amani Karume na waasisi wengine wa mapinduzi hayo.
Alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli za kimaendeleo ili kujenga uchumi imara wa Zanzibar.
Alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli za kimaendeleo ili kujenga uchumi imara wa Zanzibar.
“Tuna changamoto nyingi za kimaendeleo. Vijana
wetu wengi hawana ajira, lakini Serikali itahakikisha inawapatia mikopo
na mafunzo kupitia vikundi vyao, ili waweze kushiriki katika uzalishaji
mali. Pia wajasiriamali nao tutajitahidi kuwawezesha ili kuongeza tija
katika shughuli zao za kimaendeleo,” alisisitiza Dk Shein.
Mafanikio ya Serikali
Akizungumzia mafanikio Dk Shein alisema kwamba Serikali yake imepata mafanikio makubwa katika sekta ya afya, elimu na miundombinu, huku akiwahakikishia Wazanzibari kuimarika kwa upatikanaji wa maji na umeme katika kipindi kifupi kijacho.
Akizungumzia mafanikio Dk Shein alisema kwamba Serikali yake imepata mafanikio makubwa katika sekta ya afya, elimu na miundombinu, huku akiwahakikishia Wazanzibari kuimarika kwa upatikanaji wa maji na umeme katika kipindi kifupi kijacho.
Dk Shein alisema ukuaji wa uchumi unatazamiwa
kufikia asilimia saba kutoka asilimia 6.8 katika mwaka 2011, huku pato
la taifa likiongezeka kwa Sh1,198 bilioni katika mwaka 2011 kutoka
Sh946.8 bilioni katika mwaka 2010.
Alisema kuwa mafanikio hayo ya kukua kwa uchumi
yamesaidia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa
mbalimbali za chakula kutoka asilimia 20.8 Desemba mwaka 2011, hadi 4.2
Novemba mwaka 2012 na kutoa faraja kubwa kwa wananchi.
Rais huyo wa Awamu ya Saba wa Zanzibar alisema
kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kutoka Sh181.4 bilioni
mwaka wa fedha 2010-2011 na kufikiya Sh212 bilioni katika mwaka
2011-2012, ikiwa ongezeko la asilimia 17.
No comments:
Post a Comment