Thursday, January 17, 2013

MDHAMINI AMKANA SHEKH PONDA




MWENYEKITI wa Baraza la Wadhamini la Bakwata, Masoud Ikome (72), amemkana Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Ponda Issa Ponda, mshirika wake, Shekhe Mukadam Abdallah Swalehe (45) na wafuasi wao kuwa hawatambui hata kwa sura.

Shekhe Ponda, ambaye ni mwanaharakati maafuru wa kutetea kile anachokiita haki na mali za Waislamu anakabiliwa na mashtaka ya wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni.

Ikome ambaye ni shahidi wa nne wa upande wa mashtaka, jana alikana kumfahamu Shekhe Ponda na wafuasi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nongwa.

Hatua hiyo ilikuja baada ya kuambiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumain Kweka awaangalie washtakiwa hao kwa jumla yao na aieleze mahakama kama anawatambua.
“Hata mmoja simtambui na hakuna hata mmoja aliyewahi kuwa mjumbe wa Baraza la Maulamaa,” alidai Ikome.

Ikome alidai kuwa amekuwa akifanya kazi Bakwata tangu Mei 15 mwaka 2010 na kwamba majukumu yake ni kudhibiti mali za Bakwata zinazohamishika na zile zisizohamishika.
Alizitaja mali hizo kuwa ni pamoja na nyumba, viwanja, magari na vifaa vya maofisini.

Alidai kuwa mamlaka ya utendaji kazi huo anayapata kutoka, katika Baraza la Maulamaa na kwamba anakifahamu kiwanja namba 311/32 kwa sababu aliwahi kuitisha kikao kupitia Baraza la Wadhamini na kukijadili kuhusu kubadilishwa na kiwanja kilichokuwa kinamilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd huko Kisarawe mkoani Pwani.

“Mabadilishano hayo yalikuwa yana lengo la kupata kiwanja kikubwa ambacho kingeweza kujengwa Chuo Kikuu cha Kiislamu. Tulipata ekari 40 zilizokwishapimwa huko Kisarawe ambapo tulibadilishana na ekari nne za Malkazi Chang’ombe.” alisema shahidi huyo.

Alisisitiza kuwa nguvu ya kufanya mabadilishano ya kiwanja cha ekari nne na ekari 40 walizipata kutoka katika Baraza la Maulamaa ambalo lilikaa na kuamua kibadilishwe na kwamba hayo yalifanyika Januari 24.

Shahidi huyo wa upande wa mashtaka alidai kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maulamaa ndiyo katibu wa Baraza la wadhamini Bakwata, Suleiman Said, hivyo habari za utekelezaji wa mabadilishano hayo walikuwa wakizipata kutoka kwake.

Alibainisha kuwa kwa sasa eneo la Chang’ombe Malkazi, linamilikiwa kihalali na Kampuni ya Agritanza Ltd baada ya kukamilishwa kwa taratibu zote za mabadilishano hayo.


Kwa upande wake shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, Hafidhi Othman (42), alidai kuwa aliwahi kukutana na Shekhe Ponda ambaye ana mgogoro na Bakwata wa muda mrefu.
Alidai kuwa katika mazungumzo yake na Ponda alimweleza kuwa walichokifanya siyo sahihi kwa sababu wao kama Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, hawakushirikishwa katika mabadilishano hayo.
Shahidi huyo, anadaiwa kuwa baada ya kuambiwa hivyo na Shekhe Ponda, alimweleza kuwa kama wanaona Bakwata wamenufaika na ekari 40 na wao watafute ekari nyingine 40 ili aweze kuwanunulia.
Alidai kuwa Shekhe Ponda alikwenda na mzee mmoja ambaye alisema ana eneo la ekari 30 huko Mkuranga ambapo Ponda alimwambia kuwa “Tuache tukaangalie tutakujibu mwishoni mwa wiki na lakini usijenge ukuta.”
Hafidhi alidai kuwa ilipofika Alhamisi alipata habari kuwa Ponda na wafuasi wake watakwenda kuvamia, baada ya kupata taarifa hiyo.
Alidai kuwa ilipofika siku ya Ijumaa baada ya swala nilipita katika eneo hilo la Malkazi Chang’ombe, kweli nikawakuta watu wengi wakiwa wamening’iniza mbao na mabati katika eneo tunalolimiki bila ya idhini yetu.
Aliongeza kudai kuwa alikwenda katika kituo cha Polisi cha Kati kutoa taarifa juu ya tukio hilo.
Alidai kuwa katika eneo hilo kulikuwepo na mchanga lori tatu, kokoto tani 36, matofali 2,000, nondo na mifuko 50 ya simenti na kwamba baadhi ya vitu hivyo viliibwa.
Pia shahidi huyo alibainisha kuwa fedha zilizotumika kununua ekari 40 za Kisarawe zilitolewa na Kampuni mama ya Agritanza Ltd, Kampuni ya Ali Hillary Ltd.
Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 31, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

No comments:

Post a Comment