UBALOZI wa Kenya nchini, umesema unajiandaa kutoa taarifa rasmi
ya kiofisi kuhusu raia wake, Joshua Mlundi, anayekabiliwa na kesi ya
kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk. Stephen
Ulimboka.
Ubalozi huo umetoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana juu ya sakata
linalomkabili raia huyo wa Kenya, ambaye mapema wiki hii, aligoma na
kupanda juu ya paa la gereza kupinga kunyanyaswa na kutotendewa haki
katika mashtaka yake.
Kitendo hicho kilisababisha raia huyo kupata kipigo kikali na
kulazimika kuhamishwa na kuwekwa sehemu ya siri kwa sababu ambazo
hazijawekwa wazi na Idara ya Magereza nchini.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa masharti ya kutotajwa jina, katika
ofisi za ubalozi huo jana, ofisa mmoja katika ubalozi huo alisema tuhuma
za raia wao ni nzito na zitajadiliwa kwa kina na kisha kuzitolea
ufafanuzi.
Ofisa huyo, alisema balozi wa Kenya nchini, na msemaji wake jana
walikuwa katika kikao, hivyo ilikuwa vigumu kupatikana, lakini akakiri
kuwa wanafuatilia kwa makini mkasa mzima wa tuhuma za Mlundi na yale
yanayoendelea akiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Raia huyo wa Kenya anayeshikiliwa kwa tuhuma za kumteka, kumtesa na
kutaka kumuua Ulimboka na ambaye yuko mahabusu, aliliambia gazeti hili
kuwa anataka upelelezi wa kesi yake ukamilike haraka, ili atendewe haki,
lakini kubwa kuliko yote anaitaka serikali imlete Dk. Ulimboka
mahakamani ili aweze kumtambua.
Mwanzoni mwa wiki hii akizungumza kwa kificho kwa njia ya simu kutoka
ndani ya gereza la Keko alikohifadhiwa, raia huyo wa Kenya alisema
ameamua kutoa kauli hiyo baada ya kusoma taarifa ya gazeti hili
zilizoonyesha polisi wakirushiana mpira na kutoa kauli zinazopingana
kuhusu tukio la Dk. Ulimboka.
Alisema hadi sasa haoni maendeleo ya kesi hiyo kwani kila ikifika
mahakamani, upande wa mashtaka hutoa hoja ya kutaka iahirishwe kwa madai
kuwa upelelezi haujakamilika.
“Kila ninapoenda mahakamani naiomba mahakama imlete Dk. Ulimboka
anitambue, nahoji kwa nini upelelezi haujakamilika. Kwa bahati mbaya
sana siku hizi kesi hii inapokuja mahakamani, hata vyombo vya habari
havijulishwi. Nashukuru Mungu nimepata namba zenu za simu kutoka kwenye
gazeti lenu ili nitoe ya moyoni...
“Naomba Dk. Ulimboka aletwe mahakamani ili anitambue, kama atasema
mimi ndiye niliyemteka na kumtesa, basi kesi iendelee na sheria ichukue
mkondo wake, kama atasema sikuhusika, basi kesi iishe maana sioni sababu
ya mimi kuteseka hapa gerezani kwa kusubiri upelelezi ambao haujulikani
utaisha mwaka gani.
Wiki hii gazeti hili liliandika kuwa kijana huyo Mkenya aligoma
akishinikiza madai yake kusikilizwa. Askari mmoja wa gerezani humo
alilithibitishia gazeti hili na alinukuliwa akisema, “Ni kweli huyo
Joshua Mlundi amegoma, uongozi wa gereza umefanya juhudi za kuzungumza
naye na kilio chake anasema anataka upelelezi wa kesi yake ukamilike
haraka ili atendewe haki, lakini kubwa kuliko yote, ameitaka serikali
imlete Dk. Ulimboka mahakamani ili aweze kumtambua,” alisema askari
huyo.
Kova kuanika mbichi, mbivu leo
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar esSalaam,
leo linatarajia kufumbua kitendawili cha muda mrefu juu ya hatima ya
tume iliyoundwa na jeshi hilo kuchunguza kutekwa, kuteswa, kupigwa,
kuumizwa na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwe Pande kwa Ulimboka,
tukio lililotokea Juni 26 mwaka jana.
Mbali na kutegua kitendawili hicho pia jeshi hilo litatoa ripoti ya
jopo la wapelelezi wa jeshi hilo waliopewa jukumu la kuchunguza madai ya
kuwepo kwa askari waliokimbia na mfuko wa fedha kiasi cha sh mil. 150
katika tukio la ujambazi lililotokea mwishoni mwa mwaka jana katika eneo
la Kariakoo ambapo watu wawili walifariki. Akizungumza na mwandishi wa
gazeti hili kwa njia ya simu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, alisema leo ni siku ya Watanzania kukata kiu yao, juu ya
matukio hayo yaliyoteka hisia za watu wengi baada ya kutokea huku kukiwa
na ukimya mrefu wa jeshi hilo juu ya kile kinachoendelea.
“Mimi ninakualika katika mkutano wangu na waandishi wa habari
utakaofanyika kesho (leo) hapo nitazungumza kila kitu likiwemo suala la
Dk. Ulimboka na hata sakata la askari kudaiwa kukimbia na milioni 150,”
alisema Kamanda Kona.
Dk. Ulimboka alitekwa Juni 26 mwaka jana na kisha kuteswa kunyofolewa
kucha na meno na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwe Pande jijini
Dar es Salaam, tukio lililokuwa likihusishwa na serikali.
Hata hivyo, kutokana na utata wa tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam chini ya kamanda wake, Suleiman Kova, liliunda
tume ya wataalam kutoka ndani ya jeshi iliyoongozwa na ACP Ahmed Msangi
ili kuchunguza sakata hilo.
Hatua hiyo ilikuja kutokana na Dk. Ulimboka kuwataja baadhi ya watu
aliodai kuwa ndio walihusika kumteka na kumtesa, lakini mpaka sasa licha
ya mtu mmoja raia wa Kenya, Joshua Mulundi, kufikishwa mahakamani
akituhumiwa kuhusika na tukio hilo, watuhumiwa wengine hawajawahi
kuhojiwa.
Tume hiyo hata hivyo, haikuwahi kutoa ripoti yake kama Kova
alivyoahidi pamoja na kwamba hata majeruhi mwenyewe, Dk. Ulimboka
hajawahi kuhojiwa huku vigogo wa jeshi hilo wakitupiana mpira kuhusiana
na sakata hilo.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza hivi karibuni, jeshi hilo
kupitia kwa msemaji wake, Advera Senso, lilikanusha kuwepo kwa tume hiyo
na kusema kuwa walioteuliwa ni polisi ambao wanafanya kazi za
kiuchunguzi kwa taratibu za jeshi hilo.
Kauli ya Senso ilipingana na ile ya Kova, aliyoitoa Juni 27 mwaka jana
juu ya kuwepo kwa tume ya kufuatilia sakata hilo ambapo alimteua
Kamishna Msaidizi wa Polisi Ahmed Msangi kuongoza tume hiyo.
Msemaji wa magereza ashambuliwa
Katika hatua nyingine, msemaji wa jeshi la magereza nchini, Omari
Mtiga, ameshambuliwa vikali kwa kauli yake ya vitisho dhidi ya mwandishi
wa habari wa gazeti hili aliyekuwa akifuatilia suala la mtuhumiwa
Joshua Mulundi.
Mwandishi mkongwe nchini, Salim Saidi Salim, akizungumza na Tanzania
Daima jana, alisema kuwa kauli ya Mtiga ni ishara ya ulevi wa madaraka
walionao baadhi ya watendaji wa serikali, na akataka achukuliwe hatua
za kinidhamu na jeshi hilo.
Juzi akihojiwa na Tanzania Daima, msemaji huyo aling’aka na kumtishia
mwandishi kumkamata na kumweka ndani kwa madai kuwa suala la magereza ni
nyeti na halipaswi kujadiliwa nje ya utaratibu.
“Huyu ofisa anapaswa kuelewa kuwa jeshi la magereza siyo familia yake
na Watanzania wanapaswa kuelewa mambo yanayoendelea kupitia kwa
waandishi wa habari.
“Hivi kwangu ni vitisho na ninyi waandishi mnapaswa muandike barua
Baraza la Habari Tanzania (MCT) ili waweze kumkemea huyu aliyeshindwa
kutambua wajibu wake na kuishia kutishia wenye kuwajibika,” aliongeza
Salim Salim.
Salim, amewahadharisha waandishi wa habari nchini kuchukua tahadhari
ya hali ya juu katika kazi zao kwa madai kuwa kile alichoeleza kuwa
maisha ya waandishi kwa sasa yapo hatarini kutokana na watenda maovu
kutotaka kuumbuliwa kwa maovu yao.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Freemedia
inayochapisha gazeti hili pamoja na Sayari, Salim Salim alisema kwa sasa
watenda maovu ndani ya nchi wamekuwa wakijihami kwa kila namna ikiwwemo
hata kuwaua wale wanaowaona ni vikwazo katika kutekeleza uovu wao.
Alisema kuwa waandishi wanaoandika habari zenye kuwagusa watu hao
wahakikishe majina yao hayajitokezi katika vyombo vya habari
wanavyovitumikia juu ya habari za hatari walizoandika kwa ajili ya
kujiweka salama na kujitenga na wahalifu hao.
Akizungumzia kifo cha mwandishi wa habari wa Redio Kwizera
kilichotokea hivi karibuni mkoani Kigoma Salim Salim, alisema kuna haja
ya waliohusika kuchukuliwa hatua kali zaidi.
“Mnaandika habari za watu ambao hawapendi mambo yao yajulikane,
fikirieni mnapowaandika wakwepa kodi na waingiza madawa ya kulevya hawa
tayari wameshaamua kuua wananchi kwa njia hiyo na wakiona wewe ndiye
kikwazo kwao sidhani kama watakuacha ukiwa hai,” alisema Salim Salim.
No comments:
Post a Comment