Saturday, January 19, 2013

ISOME TAARIFA YA MAENDELEO WILAYA MAKETE


Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akisoma taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya nne katika Ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo


Wilaya ya Makete hii leo imetoa taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya nne tangu mwaka 2005-2012 kwa kuelezea mafanikio hayo katika sekta mbalimbali kufuatia agizo la waziri mkuu Mizengo Pinda alilolitoa kwa wakuu wa mikoa na wilaya kufanya hivyo

Akisoma mafanikio hayo mbele ya viongozi wa serikali na binafsi pamoja na wananchi, Mkuu wa wilaya ya Makete mh. Josephine Matiro amesema kuwa wilaya imepiga hatua katika nyanja mbalimbali zikiwemo elimu, kilimo, afya, maji, na maliasili

Akizungumzia sekta ya kilimo mh. Matiro amesema wilaya imekuwa na ongezeko la mavuno kutoka tani 74,219 mwaka 2005 hadi 145,436 mwaka 2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 95 huku matumizi ya pembejeo za kilimo yakichangia ongezeko hilo



Amesema matumizi hayo ya pembejeo yanatumika katika shughuli zote za kilimo ikiwemo mahindi na viazi


Pamoja na mambo mengine katika sekta hiyo pia serikali imefanikiwa kujenga mifereji mitatu ya umwagiliaji kwani tangu mwaka 2005 mifereji hiyo haikuwepo ambayo ni mifereji ya Mfumbi, Luwumbu na Ikuwo na miradi hiyo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 430

 

Kwa upande wa sekta ya afya mkuu huyo wa wilaya amesema kumekuwa na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya hadi kufikia 41, hospitali 3 vituo vya afya 5 na zahanati 33 huku vituo vya kutolea huduma za unasihi na upimaji zikiongezeka kutoka vituo 3 mwaka 2005 hadi 15 mwaka 2012


Amesema idadi ya watu wanaopima virusi vya ukimwi kwa hiari imeongezeka kutoka 109 sawa na asilimia 18 mwaka 2005 hadi 21,417 mwaka 2012

Akishukuru kwa niaba ya waalikwa waliofika kusikiliza taarifa hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh. Daniel Okoka ameshukuru kwa utaratibu huo ulioanzishwa na serikali huku akiikubali taarifa hiyo na kusema ndiyo hali halisi

“sisi kama halmashauri tunakubaliana na taarifa hiyo iliyosomwa na mkuu wa wilaya na imelenga karibu sekta zote hivyo ni wajibu wetu kuzidi kufanya kazi ili taarifa ijayo ikija iwe nzuri zaidi ya hapa” alisema Okoka



Amesema wilaya imepiga hatua ya kimaendeleo huku akitolea mfano kuwa wilaya ya makete imejitahidi kujenga madaraja ya zege kwenye mito mikubwa iliyopo wilayani humo tofauti na wilaya nyingine jambo linalopelekea TANROADS kuipongeza wilaya kwenye vikao mbalimbali



“Ukiangalia kwenye mito mikubwa yote tumejenga madaraja ya zege kwani ni ukweli usiopingika kuwa kuna wilaya zinatumia madaraja ya miti hadi sasa, kwa kweli hili ni jambo la kujivunia tena sana” alisema Okoka


Pia kwenye kikao hicho mkuu wa wilaya alitoa fursa ya wadau mbalimbali walioshiriki kuchangia maoni ama kuuliza maswali kuhusiana na mafanikio hayo, huku wadau hao wakitoa maoni yao pamoja na ushauri huku wengine wakiuliza maswali ambayo yalipatiwa majibu kutoka kwa wataalamu waliohudhuria kikao hicho


Kutokana na agizo hilo la waziri mkuu taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya nne itakuwa ikisomwa kwa wananchi kila baada ya miezi minne



Wajumbe wakifuatilia kwa makini taarifa hiyo ya mkuu wa wilaya      


Mtangazaji wa Kitulo Fm Aldo Sanga (kulia) akimhoji mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula 
Mtangazaji wa Kyela Fm na mwandishi wa gazeti la majira bw. Israel Mwaisaka 
 
 
SHUKURANI KWA ; http://eddymoblaze.blogspot.com
 
 

No comments:

Post a Comment