Sunday, December 9, 2012

GAMBOSHI:MAKAO MAKUU YA WACHAWI




 Na: Miguel Suleyman, Bariadi 

WAKAZI wa Kijiji cha Gamboshi, kilichopo wilayani Bariadi, Mkoa wa Shinyanga, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete awasaidie kusafisha kijiji chao kutokana na jina baya lililoenezwa duniani kwamba  hapo ni makao makuu ya maovu ya uchawi  ulioshindikana.

Kijiji hicho ambacho ni nadra sana kutembelewa, kimepata umaaurufu mkubwa ndani na nje ya nchi kikielezwa kuwa ni kitovu cha uchawi na wachawi wanaoweza kufanya miujuza, hali ambayo imekifanya kijiji hicho kupitwa na mkondo wa kimaendeleo.

“Sisi ni wakulima wakarimu wa pamba, mahindi na mpunga. Yote mnayoyasikia kwamba sisi ni magwiji wa uchawi ni uvumi uliotiwa chumvi nyingi. Tunamwomba Rais wetu kwa kushirikiana na Mbunge wetu, Andrew Chenge watusadie kulisafisha jina letu,”alisihi  Zephania Maduhu, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Gamboshi.
Maduhu pamoja na wanakijiji wenzake walidai kuwa, hofu iliyoenezwa ndani na nje ya nchi kuhusua uchawi uliovuka mipaka wa Kijiji cha Gamboshi umesababisha madhara makubwa kwa kijiji chao kiasi chakutengwa na jamii yote ya Watanzania.
“Hakuna aliyetembelea kijiji hiki kwa miaka mingi sana. Hata sisi tunapotoka nje ya kijiji, wengi hawataki kutusogelea wakiamini tutawadhuru, ”  alisema Musa Deus (26), mmoja wa wakulima walionufaika kilimo cha mkataba kijijini Gamboshi.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, tangu Uhuru mwaka 1961, hakuna kiongozi yoyote wakitaifa aliyewahi kukanyaga kijijini hapo.
Anaongeza kuwa mtu wa pekee aliyewahi kuzuru kijijini hapo ni mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, aliyefika kijijini hapo mwaka 2010, wakati akifanya kampeni za ubunge.
“Tume ya Katiba ilitupita, mwenge wa Uhuru nao haujawahi kupita hapa.Tuko kisiwani mbali na Watanzania wengine,” anasema Maduhu.
Kikiwa mafichoni kabisa, kiasi cha kilometa 44 kutoka mjini Bariadi, Kijiji cha Gamboshi si rafiki wa watu wa Kanda ya Ziwa kama ambavyo Mwananchi Jumapili ilibaini katika utafiti wake wa muda mrefu.
Mijini na vijijini, kumekwepo na ubishani mkali kuhusu ni mkoa gani unaokimiliki kijiji hicho, ambacho baadhi ya wakazi wake wanadai kuwa miongoni mwa vioja vyake ni mauzauza yanayoweza kuifanya Gamboshi ionekane kama Jiji la New York, Marekani au London, Uingereza wakati wa usiku.
Pamoja na umaarufu wake, bado uwepo wa Gamboshi umekuwa ni kitendawili kikubwa kwa jamii ya Wasukuma kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu.Mbali na ubishani mkali kuhusu kuhusu mahali hasa kilipo kijiji hicho cha miujiza, wengi wamekuwa wakidai wakazi wake siyo jamii ya Kisukuma.
 
Wakazi wa Shinyanga wanadai kuwa Gamboshi iko wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, wakati wale Mwanza wakidai kuwa iko mkoani Shinyanga.Kwa mujibu wa Maduhu, Gamboshi iko katika Wilaya Bariadi, karibu na mpaka unaotenganisha na Wilaya ya Magu iliyoko mkoani Mwanza.
“Tunaomba sana ndugu mwandishi, waambie Watanzania kuwa mengi wanayoyasikia kuhusu Gamboshi siyo kweli kabisa. Tunawakaribisha wote waje hapa kufanya biashara na sisi, waoleane na vijana wa Gamboshi kama wafanyavyo katika vijiji vingine. Sisi ni binadamu wema,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Malimi Kidimi ambaye ni mkulima

No comments:

Post a Comment