Sunday, December 23, 2012

SIMBA WAPELEKWA ANGOLA HUKU AZAM SUDAN KUSINI



MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba wataanza kampeni za kusaka taji la Ligi ya Mabingwa kwa kucheza na C.R. Libolo ya Angola, huku Azam  wakipanga kuanzia Sudan Kusini dhidi Al Nasir Juba katika Kombe la Shirikisho.

Katika ratiba iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Afrika CAF, inaonyesha timu hizo za Tanzania zitaanza kampeni zo nyumbani mapema mwezi Februari15, 16, 17 na kucheza mechi zao za marudiano ugenini Machi 01, 02, 03.

Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa wenye watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya mabingwa wa Angola, C.R.Libolo kwenye mchezo wa awali na endapo watafuzu basi watakutana na El Merrikh ya Sudan  kwenye hatua ya 16 bora hapo mwezi Machi 15, 16, 17.

Azam wanaoshiriki kwa mara ya kwanza katika Kombe la Shirikisho watacheza na wageni wenzao Al Nasir Juba ya Sudan Kusini mchezo utakaofanyika Dar es Salaam kati ya Februar 15, 16, 17  na marudiano yatakuwa mwezi Machi jijini Juba.

Endapo Azam itafanikiwa kuitoa Al Nasir na kusonga mbele kwenye hatua ya 32 bora na watacheza na mshindi kati ya Barrack Y. C. II ya Liberia dhidi ya Johansens ya Sierra Leone mchezo utakaopigwa Machi15, 16, 17 ili kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya 16 bora.

Simba wenye wanaingia kwenye michuano hiyo wakiwa na kumbukumbu ya kutolewa mwaka 2011, na Wydad Casablanca kwa kuchapwa mabao 3-0, ikiwa ni baada ya kushinda rufaa yao dhidi ya TP Mazembe.

Ratiba hiyo ya CAF inaonyesha Simba watacheza na Merreikh ya Sudan kwenye raundi ya pili klabu iliyozua mzozo kubwa hivi karibuni baada ya kutangaza kumsajili Mrisho Ngassa.

Nia hiyo ya Merreikh imesababisha klabu za Simba na Azam kuingia kwenye utata juu ya nani mwenye haki ya muuza nyota huyo.

Uongozi wa klabu ya Simba umesema kuwa hauna kipengele katika mkataba wao wa mauzo unawapa fursa Azam FC kumuuza Ngassa kwenye klabu yoyote ikiwa pamoja na El Mereikh ya Sudan.

Akizungumza jijini jana, Mwenyekiti wa Simba,  Ismail Aden Rage amesema kuwa kitendo kilichofanywa na klabu hiyo si za kiungwana ni sawa na kutaka kuwadhulumu haki yao ya kumiliki Ngassa mpaka mwezi Mei mwakani.
Rage alisema kuwa Azam FC haijui sheria za soka zaidi ya kutoa maamuzi ya kukurupuka bila ya kusoma vipengele vya mkataba huo ambao pamoja na timu hiyo kumsajili mchezaji huyo kwa mkopo, bado wana fursa ya kumiliki kutokana na mkataba ambao wamesaini pamoja na klabu hiyo.

Alisema kuwa wameshangazwa sana na kauli ya mmoja wa viongozi wa Azam FC, Patrick Kahemele aliyoitoa hivi karibuni katika vyombo vya habari kuhusiana na sakata hilo huku akiwakashifu wao kuwa ni mbumbumbu wa sheria.

ìKwanza nataka kumjibu Kahemele, sisi siyo mbumbumbu wa sheria, haya ni matusi na wala sisi siyo watu wa kukurupuka, yeye (Kahemele)  hakuwahi kucheza mpira, hata huyo bosi wake (Bakhresa) hawezi kusema hayo kwani alikuwa mweka hazina wangu nikiwa kiongozi wa Simba, anajua mimi ni kiongozi wa aina gani,î alisema Rage

ìNataka kumpasha au kumjulisha kuwa mimi ni nani katika soka, nimekuwa kiongozi wa DRFA na kuwa katibu mkuu wa FAT (sasa TFF) kwa kipindi kirefu, nimekuwa kamishina wa CAF na Fifa, mbali ya kuucheza mpira katika klabu ya Simba, huo ni wasifu wangu kwa ufupi ambao unamzidi yeye pamoja na kupewa nafasi ambayo haiwezi ndani ya Azam FC,î alisema.

Wakati tunamchukua Ngassa kutoka kwao, wao walituomba tumfuate yote yaliyoandikwa kwenye mkataba wao ikiwa pamoja na kumpa mshahara waliokuwa wanamlipa na mambo mengine kwa mujibu wa mkataba ambao tumeununua kwa mujibu wa sheria za soka kwani kila mchezaji anatakiwa kuwa na mkataba kutokana na ligi yetu kuwa ya kulipwa.

Alisema kuwa Ngassa hana kitu chochote kinachomfanya aonekane kuwa mchezaji wa Azam FC mpaka hapo mkataba uliopo kumalizika mwakani. ìHata leseni anayoitumia ni ya Simba SC, watashindwa kupata ITC kwani lazima wapate idhini kutoka kwetu, hilo lipo wazi nah ii tunatoa taarifa kwa TFF,î alisema.

Alisema kuwa wapo wapo tayari kukaa na Azam FC kulimaliza suala hilo kwa wao kukubali kuwa hawana mamlaka ya kuumuza mchezaji huyo na haki hiyo ikiwa kwa Simba.

No comments:

Post a Comment