JALADA la kesi ya kuua bila kukusudia la msanii nyota wa filamu nchini,
Elizabeth Michael 'Lulu' tayari limetua Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam na kesi yake imesajiliwa.
Lulu anakabiliwa na mashtaka ya kumuua bila kukusudia, aliyekuwa msanii
maarufu wa fani hiyo nchini, Steven Kanumba kinyume cha kifungu cha 195
cha Kanuni za Adhabu.
Awali, kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa
ajili ya kukamilisha hatua za awali ukiwamo upeelelezi, huku
akikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia kinyume cha kifungu cha
196.
Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP), alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia.
Desemba 21, 2012, Lulu alisomewa maelezo ya kesi, yakiwemo ya mashahidi
watakaotoa ushahidi dhidi yake na maelezo yake aliyoyatoa polisi, kisha
Mahakama ya Kisutu ilifunga rasmi kesi hiyo na kutamka rasmi kuihamishia
Mahakama Kuu, ambako ndiko itakakosikilizwa.
Habari zilizopatikana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana zilisema
kuwa, tayari kesi hiyo imeshapokelewa mahakamani hapo na kupewa usajili
wa shauri la jinai namba 125 mwaka 2012.
Hata hivyo, habari hizo zilisema kuwa kwa sasa kesi hiyo inasubiri
kupangiwa Jaji atakayeisikiliza baada ya taratibu zote za kimahakama
kukamilika, kwa tarehe itakayopangwa na msajili kulingana na ratiba ya
vikao vya mahakama hiyo.
Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, Aprili 7, 2012, nyumbani
kwake Sinza Vatican, Dar es Salaam. Wakati akisoma maelekezo ya kesi
hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro alidai kuwa, upande
wa mashtaka utawaita jumla ya mashahidi tisa.
Wakili Kimaro pia alidai kuwa, upande wa mashtaka utawasilisha
mahakamani vielelezo kadhaa vitakavyotumika kama sehemu ya ushahidi
katika kesi hiyo, ikiwamo ramani ya eneo la tukio kwenye chumba alimofia
Kanumba, ripoti ya uchunguzi wa kifo na maelezo ya onyo la Lulu.
Wakili Kimaro alidai kuwa, Aprili 7, 2012, Lulu alitoa maelezo ya onyo,
kuhusiana na tuhuma zinazomkabili, katika kituo cha polisi cha
Oysterbay, yaliyochukuliwa na askari wa kituo hicho, mpelelezi Sajenti
Renatus.
Kwa mujibu wa maelezo hayo ya onyo, Lulu alizaliwa mwaka 1994 na
alimaliza kidato cha nne katika shule ya sekondari Midway na kwamba
baada ya hapo, aliendelea na shughuli za sanaa kuanzia mwaka 2000.
No comments:
Post a Comment