JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 14/12/2012
KWA NINI LAMBALAMBA WANAPIGWA VITA
DODOMA
Kwanza ni lazima tufahamu Lambalamba
ni nini?
Hili ni kundi la watu
ambalo wameliunda kwa lengo la kujihusisha na vitendo vya kitapeli na ulaghai
kwa wananchi hususani wa vijijini, ili kujipatia mali zikiwemo fedha na mifugo
ya aina mbalimbali toka kwa wanavijiji katika mkoa wetu wa Dodoma.
Kundi hili ni mkusanyiko wa
watu wa jamii tofauti ambao wanatoka maeneo ya Rufiji , Pwani, Tanga na Morogoro ambao wamekuja
kuivamia jamii ya watu Dodoma ambayo
nayo ina mila na desturi zake katika mambo ya jadi.
Wamekuwa wakitumia mtindo
wa kujifanya kuwa wao ni waganga wa tiba za jadi kwamba wana uwezo wa kutoa
vitu vya kichawi katika majumba ya watu,
sehemu za biashara na pia kufichua wachawi, vitu ambavyo kwa hakika hawana uwezo
navyo.
Ili mtu akubalike kuwa ni
mganga wa tiba za jadi ni lazima afahamike katika eneo analofanyia shughuli
zake hizo kuanzia uongozi wa ngazi ya chini hadi wa juu wa serikali na awe na kibali
cha kuendesha tiba hizo kisheria kitu ambacho kundi la lamba lamba hawakidhi
matakwa hayo.
Pia Mganga wa jadi kwa
asili yake hatakiwi kufanya kazi zake kwa kuita baadhi ya watu ni wachawi.
Hutakiwa kutoa tiba na kinga kwa kutumia miti shamba kulingana na uwezo wake, na
sio wanachofanya hao wanaojiita lambalamba hii ni tofauti na sheria
zinavyoelekeza.
Kwanza wanavijiji
huchangishwa na ndipo huitwa kundi hilo
kuja kufanya kazi wanayodai ni ya kufichua wachawi au washirikina, ambao wanadai
wanavuta mali za watu wengine kwao na kuwa matajiri.
Uchunguzi wetu umebaini kwamba
wanachofanya kundi la lambalamba kwa
kushirikiana na washirika wao, huwa wanapandikiza vitu kwenye nyumba, mashamba
au sehemu za biashara za mlengwa nyakati za usiku.
Baada ya kufanya hivyo
ndipo wanaondoka na kundi la watu na kwenda kutoa vitu ambavyo
walishavipandikiza kabla, kisha kinachotokea kwa anayefanyiwa hivyo ni kudhalilika
yeye na familia yake kuwa ni mchawi na
kibaya zaidi hulazimishwa kutoa kiasi cha fedha na mifugo kama adhabu na kutishiwa wasithubutu kwenda kutoa taarifa
Polisi.
Hili ni kosa la jinai na
ukiukwaji mkubwa wa haki za Binadamu, hatuwezi kuvumilia na kuwaacha wananchi wenzetu
kuendelea kupoteza fedha na mali zao kwa kuwanufaisha hao matapeli.
Zipo taarifa kuwa
lambalamba hao wanapofika vijijini hutafutiwa wanawake wa kuwapikia na
kuwastarehesha. Huu ni unyanyasaji wa kijinsia na jambo la hatari ambalo
litachangia kuenea kwa magonjwa ukiwemo UKIMWI.
Haya yanayofanyika ni
utapeli mkubwa uliobuniwa na watu hao wa kujipatia fedha. Ni jambo
linalodhalilisha, linalojenga chuki, na uchochezi ndani ya jamii. Pia
linahatarisha usalama na amani pamoja na
afya za wanawake na jamii kwa ujumla.
Hili ni jambo la kukemea
kuanzia ngazi ya Familia, Kitongoji, Mtaa, Kata hadi Taifa. Wote kwa pamoja
tunaona athari zake tukemee kwa nguvu zote na wale wanaoendesha na kushabikia kundi
hilo watolewe taarifa ili wakamatwe.
Watu wasiogope kutoa
ushahidi dhidi ya kundi la lamba lamba na washirika wake hao wanaovuruga amani,
utulivu, usalama na kurudisha maendeleo nyuma.
Tupo kwenye karne ya
Sayansi na Teknolojia tusijiaibishe kwa kukumbatia mambo ya zama za kiza kwa
kupumbazwa akili zetu na matapeli waliobuni mradi wa kujipatia fedha na mali
kwa ujanja wa kupandikiza vitu kwenye nyumba, sehemu za biashara na mashamba, kisha
baadaye wanakuja kuvitoa na kudai wamefanya hivyo kwa uwezo wao wa kubaini
wachawi na kuifanya jamii yetu iishi kwa chuki na kukosa amani na kushindwa
kufanya shughuli za kujiletea maendeleo
Mwisho
napenda kutoa wito kwa wananchi kwa
ujumla kupitia
dhana ya utii wa
sheria kwa hiari kushirikiana kwa pamoja na
Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za watu
hao ili kuutokomeza uhalifu huu ili jamii yetu iendelee kubaki salama na yenye amani na utulivu.
[D. A. MISIME – ACP]
KAMANDA WA POLISI
[M] DODOMA
CONTACT:
POLISI
MKOA WA DODOMA
DAWATI
LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Phone: 0715 006523, Luppy Kung’alo – Mrakibu
msaidizi wa Polisi (ASP)
Phone: 0712
360203, Silyvester Onesmo – Police
Konstebo (PC)
No comments:
Post a Comment