Askari wa
Idara ya Uhamiaji DRC, akiwauzia wachezaji wa Azam FC ya Dar es Salaam kuingia
mjini Kinshasa baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa N’djili, mjini Kinshasa usiku
wa jana
|
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
WAWAKILISHI
wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, (CAF), Azam FC
wamewasili salama mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) majira
ya saa 5:58 usiku wa jana kwa saa za huku na saa 7:58 kwa saa nyumbani
Tanzania, tayari kucheza mashindano ya Kombe la Hisani mjini hapa.
Hata hivyo,
Azam wamewasili pungufu ya watu watano katika msafara wao wa watu 27, kufuatia
maofisa na wachezaji wa kigeni kuzuiliwa mjini Nairobi, Kenya kwa kutokuwa na
viza za kuingia DRC.
Wenyeji wa
Azam, waandaaji wa mashindano waliwahakikishia wageni wao hakutakuwa na tatizo
la kuingia DRC bila viza, kwa kuwa wamekwishaandaa utaratibu mzima na msafara
mzima utapatiwa viza mara utakapowasili Kinshasa.
Hata hivyo,
kwa ujumla hali ilikuwa tofauti, Kocha Mkuu Stewart Hall, Msaidizi wake, Kali
Ongala, wote raia wa Uingereza, Daktari Paulo Gomez, raia wa Ujerumani na
wachezaji Kipre Tcheche na Kipre Balou raia wa Ivory Coast walizuiwa mjini Nairobi.
Mkuu wa
msafara, Katibu wa Azam, Nassor Idrisa alitumia busara kwa kuwapatia fedha za
malazi na kujikimu watu hao watano ili wabaki Nairobi kushughulikia viza na
wataungana na timu leo baadaye.
Aidha, baada
ya kufika Uwanja wa Ndege wa Njili mjini hapa, msafara wa Azam pia ulipata
misukosuko mingine, kuanzia uwanjani hapo, wakati Maofisa wa Idara ya Uhamiaji
walipokataa kuupokea kwa sababu ya viza.
Ilifikia
hatua Maofisa hao wakaagiza msafara urejeshwe kwenye ndege ili kurejea
Tanzania, kwa kuwa haukuwa na viza, hata hivyo wenyeji wa mabingwa hao wa Kombe
la Mapinduzi, wakafanya jitihada na kufanikiwa kumalizana na Maofisa hao wa
Idara ya Uhamiaji.
Kufika
katika hoteli ya Florida walipopangiwa kufikia, lilikuwa ni tatizo lingine,
kwanza chakula kilikuwa kichache na baadhi ya wachezaji walilala bila kula
kabisa. Lakini kwa ujumla mazingira ya hoteli hayakuwa yenye kuridhisha.
Hata hivyo,
kwa mara nyingine Katibu, Nassor akatumia busara kwa kukubali timu ilale hadi
asubuhi na kupatiwa na hoteli nyingine yenye hadhi, jambo ambalo wenyeji wao
waliafiki na kuomba radhi kwa usumbufu wote uliojitokeza.
Katika
michuano hiyo, Azam inatarajiwa kufungua dimba leo kwa kumenyana na Dragons
kwenye Uwanja wa Martyrs, saa 9:30 za huku, yaani saa 11:30 za nyumbani
Tanzania.
Azam ambao
ni washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame
na Ligi Kuu, wamepangwa katika Kundi B pamoja na Dragons na Shark FC, ambayo
watacheza nayo Desemba 17.
Ikifuzu
kwenye kundi lake, Azam itaingia Nusu Fainali moja kwa moja, ambazo zitachezwa
Desemba 25 na Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu. Kundi B, lina timu za DC Motema Pembe,
Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa.
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa amesema wamekuja kushiriki mashindano
haya kwa lengo la kuwapa mazoezi na uzoefu wachezaji wake kabla ya kuingia
kwenye Kombe la Shirikisho mwakani.
Alisema Azam
pia, itatumia mashindano hayo kama fursa ya kuwapima wachezaji wake kabla ya
kuanza kwa Kombe la Shirikisho mwakani, ambako wamepangwa kuanza na Al Nasr
Juba ya Sudan Kusini.
Kikosi cha
Azam kilichowasili jana hapa, ukiondoa waliozuiwa Nairobi ni; Mwadini Ally,
Jackson Wandwi, Gaudence Mwaikimba, Himidi Mao, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz,
Luckson Kakolaki, Samir Hajji Nuhu, Zahoro Pazi, Seif Abdallah, Malika Ndeule,
Omar Mtaki, Abdi Kassim, Uhuru Suleiman, Brian Umony na David Mwantika.
Wachezaji
wengine ambao hawahusiki katika safari hiyo, ni wale waliopo kwenye kikosi cha
timu ya taifa, Khamis Mcha ‘Vialli’, John Bocco ‘Adebayor’ na Salum Abubakar.
Wachezaji wapya, Joseph Mieno na Joackins Atudo kutoka wanaweza kujiunga na
timu baadaye mjini hapa.
Katika
mchezo wa leo, timu itaongozwa na kocha wa makipa, Iddi Abubakar Mwinchumu
ambaye ni ‘Azam Damu’, aliyeipandisha timu kutoka Daraja la Tatu hadi Ligi Kuu
kwa kulinda lango vema, huku John Bocco ‘Adebayor’ akitupia nyavuni.
No comments:
Post a Comment