Sunday, December 9, 2012

AJALI YAUA 10 IRINGA NA KUJERUHI WENGINE KADHAA




 Na Francis Godwin
ZIKIWA  zimepita  siku takribani  tatu  toka ajali mbaya  itokee katika kata ya Mseke katika wilaya ya Iringa  vijijini mkoani Iringa na  kupelekea  vifo  vya  watu  watano  wa familia  moja na mmoja  kujeruhiwa  vibaya , ajali nyingine mbaya  imetokea  katika  kata  hiyo ya Mseke  katika barabara ya Iringa -Mbeya na kupelekea vifo vya abiria zaidi  ya 10  huku  wengine  zaidi ya 42  wakijeruhiwa  vibaya.

Huku baadhi ya  watu  wanaodaiwa  kuwa ni vibaka  wakivamia eneo hilo na  kujaribu  kupora mali za majeruhi wa ajali  hiyo  wakati  wakisogea  eneo hilo kwa ajili ya  kusaidia majeruhi na kunusurika  kichapo kutoka kwa  baadhi ya abiria ambao  mbali ya kupata ajali  hiyo  walikuwa na nguvu ya  kupambana na vibaka  hao.i hilo.

Pamoja na  vibaka  kujitokeza  eneo hilo bado  wananchi  waliofika  eneo hilo zaidi ya 200 walilazimika  kufanya maandamano  kuwafuata  askari  polisi wa usalama barabarani  waliokuwepo  eneo  hilo wakishiriki  zoezi la uokoaji  ,wakitaka askari  hao  kumbana mkandarasi wa kampuni  inayoendelea na ujenzi  wa barabara  ya Iringa -Mafinga  ili  kutoa mitambo  yake kwa ajili ya  kusaidia  kunyanyua basi  hilo ambalo lilikuwa  limeangukia shimoni ili kuokoa majeruhi  waliofunikwa na basi hilo .

Mashuhuda  wa ajali  hiyo ambao  walipata  kuzungumza na mwandishi  wa habari  hizi kwa njia ya  simu leo  walisema  kuwa ajali  hiyo ilitokea majira ya saa 8 za mchana na  chanzo  cha ajali  hiyo ni kugoma  kuingia gia na kufeli kwa breki wakati likijaribu  kupanda mlima mdogo uliopo eneo  hilo pamoja na  ubovu  wa basi  hilo lenye namba za usajili  T 803 APV Nissani mali ya Msanya  Trans ambalo lilikuwa  likitoka mjini Iringa  kwenda Usokami  wilaya ya Mufindi .

John  Kalinga ni mmoja kati ya mashuhuda  wa tukio  hilo alisema  kuwa basi lilikuwa likielekea Usokami na baada ya  kufika katika  eneo la Kichakani  lilikosa mwelekeo kutokana na mwendo kasi ambao  dereva  wa basi  hiyo alikuwa akiendanao na hivyo kuyumba na  kupinduka .

Hata  hivyo  alisema  kuwa mara baada ya ajali  hiyo kutokea  abiria  wote  zaidi ya 50  waliokuwemo  walifunikwa na basi  hilo na kufanyika  jitihada mbali mbali kutoka kwa  wasamaria  wema na kuweza  kuokoa majeruhi hao ambao  walikuwa  wamefunikwa na basi hilo.

Kwa upande  wake mmoja kati ya majeruhi  wa ajali  hiyo alisema  kuwa basi  hilo ni bovu ila  kila  wakati  askari wa usalama barabarani  wamekuwa  wakiliacha kuendelea na safari  jambo ambalo ni hatari kwa usalama  wa  wananchi  wanaotegemea usafiri  huo katika eneo  hilo la Usokami  wilaya ya Mufindi.

Alisema  kuwa bado ni vema  polisi  wa usalama barabarani  kuchukua hatua  ya kukagua mabasi  yote ya vijijini ambao  yameendelea  kufanya kazi ya kusafirisha abiria  huku yakiwa katika hali ya ubovu  zaidi.

Mbali ya  taarifa  za kiusalama  kudai  kuwa  mtu  aliyepoteza maisha katika ajali  hiyo ni mmoja ambae ni mwanaume mtu mzima taarifa  kutoka kwa  mashuhuda wa ajali  hiyo pamoja na taarifa  zilizothibitishwa na diwani  wa kata  hiyo ya Mseke Robert Lawa alidai  kuwa  jumla ya maiti  watano   walikuwa  wametolewa katika  eneo  hilo la ajali hadi majira ya 10;45 jioni  wakati jitihada za  kulivuta basi hilo ili 
kuwavuta abiria  waliobanwa na kuangalia maiti  wengine  zikiendelea na kukiri  kuwa kazi ya  uokoaji iliendelea  kuwa ngumu zaidi baada ya kutumia masaa zaidi ya mawili kuendelea kuwaokoa majeruhi na kuwakimbiza  Hospitali ya mkoa  wa Iringa.

Hadi  tunakwenda mitamboni  bado  jitihada za uokoaji wa zilikuwa  zikiendelea na  wananchi pamoja na askari wa usalama barabarani na  wananchi mbali mbali kutoka maeneo hayo huku miili 11 ikiwa  imetolewa eneo hilo na baadhi ya majeruhi  ni mahututi  zaidi.

No comments:

Post a Comment