Friday, November 2, 2012

YANGA WATEGESHEA OKWI WAMHAMISHE DAR

Yar

Emmanuel Okwi
MICHAEL MOMBURI
TAJIRI aliyeikomoa Simba kwenye usajili hivi karibuni, Abdallah Bin Kleb ametamka kwamba Kocha Ernest Brandts akiwaambia kwamba mwezi ujao anamtaka Emmanuel Okwi watamsaka kwa gharama yoyote na kumpeleka Jangwani.

Lakini, Simba tayari wamemhamisha Okwi kwenye nyumba aliyokuwa akiishi maeneo ya Keko na kumpeleka Sinza Mori jijini Dar es Salaam na kumkabidhi gari aina ya Toyota GX 110 ingawa bado hawajamsainisha mkataba mpya kutokana na kushinikiza dau kubwa, ingawa mazungumzo bado yanaendelea.

Bin Kleb, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano ya Yanga, aliizidi kete Simba baada ya kumsajili kiraka Mkongomani, Mbuyu Twite aliyekuwa amesaini mkataba na Simba na kupokea kitita cha dola 30,000 kabla ya kuwageuka na kutua Jangwani.

Okwi yupo katika mazungumzo ya usajili na Simba na mkataba wake unamalizika Juni mwakani, ikiwa ni miezi minane tu kutoka sasa.

Straika huyo amewapa masharti Simba kwamba anataka Dola 50,000 (Sh 80 milioni), nyumba, gari na mshahara wa Dola 3,000 (Sh.4.8 milioni) kila mwezi.

Bin Kleb aliiambia Mwanaspoti kuwa wanamsikiliza kocha tu kwani iwapo akimnyooshea kidole Okwi watatangaza dau kubwa.

"Kama Kocha akitutamkia kwenye ripoti yake ya mwisho kwamba anamtaka Okwi kwenye safu yake, sisi tutatangaza dau, tutamchukua kwa gharama yoyote. Hatuwezi kushindwa ilimradi tu kocha ametuhakikishia kwamba anamtaka, ila bado hatuna uhakika na mkataba wake umebaki muda gani Simba,"alisema Bin Kleb.

"Si yeye tu mchezaji yeyote yule. Tunachotaka sasa ni kuhakikisha timu inakaa vizuri na inashinda mechi zote zilizobaki kwa kuwa tulianza ligi vibaya na wenzetu walikuwa vizuri.

"Tulisajili wachezaji wengi kwenye usajili uliopita lakini kocha ataangalia utendaji wa kikosi kizima nadhani anaweza kufanya mabadiliko, sisi hatuhusiki kabisa, tunasubiri ripoti yake kama kuna watu anataka kuwachomoa au kuwaongeza sisi tutamletea,"alisisitiza kiongozi huyo aliyewezesha pia usajili wa kiungo, Haruna Niyonzima `Fabregas' kutoka APR msimu uliopita.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo, alisema hawajafanya mazungumzo rasmi ya usajili na Kabange Twite ambaye yupo Dar es Salaam mpaka wapate uamuzi wa kocha.

Yanga ambayo tayari ina wachezaji watano wa kigeni huenda ikamchomoa mchezaji mmoja ambaye hajacheza mechi nyingi kupisha usajili wa Kabange.

Wageni waliopo Yanga ni pamoja na Yaw Berko (Ghana), Didier Kavumbagu (Burundi), Hamisi Kiiza (Uganda), Mbuyu Twite (Congo) na Haruna Niyonzima (Rwanda).

Tayari kocha Brandts ameliambia Mwanaspoti kuwa anamuhitaji Kabange kwa sababu anamjua tangu walipokuwa APR ya Rwanda.

No comments:

Post a Comment