MKAZI mmoja wa Kijiji cha Kivuga Wilayani Kilindi,
anashikiliwa na jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumiliki shamba la bangina
kuendesha biashara hiyo ya dawa za kulevya.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Tanga, Costantine Massawe alisema jana
kuwa mtuhumiwa
huyo alikamatwa juzi saa 10.30 katika kijiji cha Kivuga kata ya Kimbe
Wilayani Kilindi baada ya kuvamiwa shambani kwake.
Alisema
wakati akikamatwa, mtuhumiwa huyo alikutwa na bangi yenye uzani wa kilo
60 aliyokuwa ameiandaa kwa ajili ya kuisafirisha nje ya Wilaya ya
Kilindi kwa ajili ya kwenda kuiuza.
Alisema jeshi la
Polisi liliweza kumkamata mtu huyo baada ya wananchi wema kutoa taarifa
za siri zenye kudai kuwa amekuwa akijishughulisha na kilimo zao la
bangi kwa mda mrefu.
Katika taarifa hizo za siri
zilizotolewa na wananchi wema ni kuwa mtuhumiwa huyo huuza katika mikoa
jirani kwa watu ambao hujishughulisha na biashara hiyo haramu ya
mihadharati.
Alisema mkulima huyo,awali alikuwa
akijishuhurisha na uuzaji wa bangi na alipoona biashara hiyo inamuendea
vizuri akaona alime shambani kwake ambapo amekutwa akimiliki shamba
lenye ukubwa wa robo ekari na kisha kuvuna na kuzisambaza katika mikoa
ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
“Jeshi la Polisi
limeweka mkakati maalumu wa kuendesha kampeni ya kuyateketeza mashamba
yote lakini wale wanaolima na kuuza bangi wajue wanafanya kazi iliyo
kinyume cha sheria na kwamba tutahakikisha tunawakamata na kuwadhibiti,"
alisema Massawe.
Alisema mkulima huyo anatarajiwa
kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kulima na kuuza bangi ikiwa
anafahamu kwamba ni kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment