KESI inayowakabili Wakenya wanne kuhusu vurugu za Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2008 iliyopo katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Uhalifu wa Kivita (ICC), imechukua sura mpya baada ya mmoja wa
watuhumiwa hao, Uhuru Kenyatta kwenda na ujumbe wake kwa Rais Jakaya
Kikwete kumwomba amuunge mkono katika harakati zake za urais.
Kwa
mujibu wa gazeti la Standard la Kenya, Rais Kikwete alikutana na
kiongozi huyo wa Chama cha The National Alliance Ikulu na kufanya naye
mazungumzo yaliyodumu kwa saa tatu.
Katika kikao hicho
pia kulikuwa na wajumbe wengine kutoka chama cha URP cha William Ruto
na wale wa New Ford Kenya wakiongozwa na Waziri wa Sheria, Eugine
Wamalwa anayetajwa kuwa mgombea mwenza wake.
“Kenyatta
alisema kuwa malengo yake na viongozi wenzake ni kuipeleka Kenya mbele
wakiwa na umoja. Kwa kumalizia akasema, wanalenga kuwafikia viongozi wa
vyama vya siasa,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kenyatta, Munyori
Buku.
Ujumbe wa Uhuru umekuja ikiwa ni siku moja
kabla ya kuwasili Nairobi kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou
Bensouda kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo na kujionea
maeneo yaliyoathiriwa na vurugu hizo.
Umuhimu wa
safari hiyo pia umetokana na safari ya Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa
Mataifa, Kofi Annan na Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa nchini
Kenya hivi karibuni, huku wakiwa na ujumbe kwamba Kenyatta na Ruto
hawana sifa mbele ya Wakenya na jumuiya ya kimataifa ya kugombea urais.
Annan ndiye aliyesimamia mchakato wa amani katika kazi ambayo alisaidiana na Rais Kikwete na Mkapa.
Annan
na Mkapa inasemekana walikwenda Nairobi na kufanya majadiliano na Rais
Mwai Kibaki yanayoaminika kujikita katika kesi hiyo ya ICC sanjari na
Uchaguzi Mkuu wa Machi 4, 2013.
Inaaminika kuwa ujumbe
huo kutoka Kenya ulikuja makusudi kwa Rais Kikwete hasa kwa kuwa ana
uhusiano mzuri na viongozi wakubwa wa mataifa ya Magharibi akiwa pia
amechangia katika kuleta amani nchini humo baada ya vurugu za Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2008.
Hivyo wamelenga kumtuma Rais
Kikwete kupeleka ujumbe ICC ili kuwaruhusu wagombee katika Uchaguzi Mkuu
kwa manufaa ya uchaguzi wa amani na Kenya kwa jumla.
Katika
ziara yake, Annan alikaririwa akisema: “Ni kweli kuna mambo ambayo kila
mtu angependa yaangaliwe hasa kwa watu wanaotajwa kugombea urais.”
Kauli hiyo imewatisha Uhuru na Ruto ambao walilipuka wakimtaka Annan kuachana na mambo ya Kenya.
Kuhusu
hilo Buku alisema: “Wakenya ndiyo waamuzi wa hatima yao … Rais Kikwete
ameombwa kushawishi kuheshimiwa kwa uamuzi wa Wakenya. Ndiyo waamuzi wa
hatima yao hivyo ni lazima waruhusiwe kuchagua viongozi wao bila
kuingiliwa. Rais amegusia kwamba, Afrika ingeheshimu uamuzi, Wakenya
wangefanikisha uchaguzi mkuu wa Machi mwakani.
“Hatuna
matatizo na marafiki zetu, lakini kama hawatuheshimu hilo ni shauri
yao, tuna marafiki wengi wa kufanya nao kazi ulimwenguni kote,” alisema
Uhuru wiki iliyopita jijini Nairobi.
Akiwa nchini,
inasemekana kuwa Uhuru alikuwa akirudia maoni yake kwa Rais Kikwete
kwamba ni makosa kwa wageni kuingilia uchaguzi wa Kenya.
Katika
hatua nyingine, mwandishi wa Mwananchi alimshuhudia Kenyatta akiwa
katika Mgahawa wa Rose Garden, Dar es Salaam akipata vinywaji na nyama
choma.
Baada ya kuingia Rose Garden akiongozana na
Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mutinda Mutiso, wateja na watu
mbalimbali walikwenda kumsalimia mtoto huyo wa Rais wa Kwanza wa Kenya,
Jomo Kenyatta ambaye alionekana mwenye furaha na hakukuwa na ulinzi
mkubwa.
No comments:
Post a Comment