ZIKIWA zimebakia siku 33 kufanyika Uchaguzi mkuu wa
Urais wa Marekani hatimaye wagombea Urais Barack Obama na mwenzake Mitt
Romney wamefanya mdahalo wao wa kwanza kupitia televisheni ambao
umeshangaza wengi baada ya kwenda kinyume na matarajio yao.
"Miaka
minne iliyopita niliposimama katika jukwaa hili nilisema kuwa
nitapunguza kodi kwa familia zenye kipato cha kati. Na hivyo ndivyo
nilivyofanya. Tumepunguza kodi kwa familia za kipato cha kati kwa kiasi
cha dola 3600. Na sababu ni kuwa naamini tutakuwa na mafanikio kama watu
wa kipato cha kati watakuwa na mafanikio"
Hivyo ndivyo
alivyoanza mazungumzo Rais Obama katika mjadala huo uliofanyika Chuo
Kikuu cha Denver mjini Colorad na kutazamwa moja kwa moja kupitia
televisheni na watazamaji wanaokadiriwa kufikia milioni 50.
Obama
alizungumza kwa muda mrefu lakini mpinzani wake Romney alimkosoa zaidi
kwa namna anavyoendesha utawala wake jambo ambalo lilionekana kumgusa.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Siasa na Masuala ya Umma, Terry Madonna alisema kuwa Obama
hakuwa katika hali yake ya kawaida hivyo hakufanya vile ambavyo wafuasi
wake na watu wengine duniani walivyotarajia.
Romney
alimshambulia Rais Obama juu ya histora yake ya kushughulikia matatizo
ya kiuchumi lakini safari hii hakuropoka wala kutoa matamshi ya
kutatanisha kama alivyozoeleka.
Romney alitumia mtindo wa
kushambulia na kisha kurejea katika nukta zake akionyesha namna
atakavyoshughulikia kila kosa la Obama alilolionyesha.
Wachambuzi wanasema kuwa Romney ameweza kumbwaga mpinzani wake katika awamu hiyo ya kwanza ya mdahalo.
"Sina
shaka akilini mwangu kuwa kama rais atachaguliwa tena mtaendelea kuona
watu wa kipato cha kati wakishuka zaidi huku kipato kikipungua na bei
zikipanda juu.
Nitainua kipato tena. Tuna ukosefu wa ajira wa
asilimia nane zaidi mwezi huu na kama nikiwa rais nitatoa nafasi mpya za
ajira milioni 12 kwa nchi hii," alisema Romney.
Kwa upande wa
masuala ya afya , Romney aliuponda mpango wa afya, maarufu kama
Obamacare, wenye thamani ya dola za Marekani trilioni 2.8 na kusema
haufai lakini hakuweza kuja na mbadala sahihi kwa wapigakura.
Masuala
ya afya ni moja kati ya ajenda kuu kuelekea uchaguzi wa Novemba 6,
mwaka huu. Mpango wa huduma za afya wa Marekani ndiyo wenye gharama
zaidi kuliko nchi zote na unalaumiwa kuwa kuchangia katika kushuka kwa
mishahara ya Wamarekani.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kituo
cha Televisheni cha CNN kwa watu wenye umri wa kupiga kura na
walioangalia mdahalo huo unaonyesha kuwa Romney amepata asilimia 67 huku
Obama akiambulia asilimia 25.
Uchunguzi kama huo umefanywa pia na Kituo cha Televisheni cha CBS na Romney amepata ushindi.
Huu ni mdahalo wa kwanza kati ya mitatu iliyopangwa kufanyika.
Wagombea
wenza kutoka pande zote mbili watakutana pia kwa mdahalo wiki ijayo.
Watu wanasubiri kuona nini kitajiri kati ya mgombea mwenza wa Obama Joe
Biden kutoka Chama cha Democrat na yule wa Romney Paul Ryan kwa tiketi
ya Chama cha Republican
No comments:
Post a Comment