SIMBA SC imekubali kuvunja
mkataba na beki wake Juma Said Nyosso kulingana na maombi yake, na imemtaka
afike kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe kujadili suala hilo.
Habari za
ndani kutoka Simba SC, zimesema kwamba Nyosso amewasilisha
maombi ya kuvunja mkataba na klabu hiyo, baada ya kushushwa kikosi cha pili,
akidaiwa kiwango chake kimeshuka hivyo amepewa fursa ya kwenda kukiboresha.
Lakini
Nyosso mwenyewe ameona kama hastahili
kushushwa timu ya pili na ameomba asitishiwe mkataba wake aondoke, jambo ambalo
uongozi wa klabu umelikubali.
Nyosso si kama anatuhumiwa kuhujumu timu, bali anaambiwa uwezo wake
umeshuka mno na kwamba amekuwa akiigharimu timu katika siku za karibuni, hivyo
amepewa fursa ya kwenda kupandisha kiwango chake.
Adhabu kama
hii amewahi kupewa mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina,
Carlos Tevez katika klabu ya Manchester
City ya England msimu uliopita na
aliitumikia vizuri hadi aliporejeshwa tena kikosi cha kwanza, ambako aliisaidia
timu kumalizia msimu vizuri kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu.
Mbali na
Nyosso, kiungo Haruna Moshi Shaaban amesimamishwa kwa wiki tatu kwa tuhuma za
utovu wa nidhamu na katika kipindi hicho atakuwa akipokea nusu mshahara.
Boban
ameamua kurudi nyumbani kwake kupumzika na mkewe hadi adhabu hiyo iishe ajue
mustakabali wake, ila amesema anaonewa kwa sababu hakupewa nafasi ya kujibu
tuhuma zake kabla ya hatua kuchukuliwa, ingawa amechukulia poa tu
.
.
Wakati huo
huo, habari zaidi kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba Mwinyi Kazimoto
Mwitula, Ramadhan Suleiman Chombo na Mrisho Khalfan Ngassa nao wanaangaliwa kwa
‘jicho la tatu’ juu ya mwenendo wao kwenye timu hiyo na kwa nyakati tofauti
wote wamekwishaitwa kuhojiwa masuala mbalimbali.
No comments:
Post a Comment