Hali ya usalama nchini imeendelea kuwa tete kufuatia matukio mbalimbali ya kuzorota kwa usalama kutokea, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa askari polisi mmoja kisiwani Zanzibar, maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kutoa tamko zito, kufikishwa mahakamani kwa Katibu wa Jumuiya za Kiislamu na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kususia kikao.
Kisiwani Zanzibar askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Koplo Said Abdulrahman, ameuawa kwa kupigwa mapanga na wafuasi wanaidaiwa ni wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kislamu (Jumiki) katika vurugu zinazoendelea mjini Zanzibar.
Kamishina wa Jeshi la polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema wafuasi wa Uamsho walimvamia askari huyo majira ya saa 6:30 juzi usiku wakati akitokea kazini.
Alisema askari huyo alivamiwa katika eneo la Bububu wakati akiendesha pikipiki aina ya Vespa ambayo ilichomwa moto.
Alisema Marehemu Said alicharangwa mapanga sehemu ya shingoni, kichwani na kumkata vidole vya mkononi.
“Tukio kubwa na la kusikitisha lililosababishwa na fujo hizi ni kuuliwa kinyama kwa askari wa Jeshi la Polisi namba F 2105 CPL Said Abdulrahman wa kikosi cha kuzuia Ghasia (FFU) Mkoa wa Mjini Magharibi,” alisema Kamishina Mussa.
WATU 10 MBARONI
Alisema jana watu 10 walikamatwa wakihusishwa na matukio ya vurugu na uharibifu wa mali za wananchi na serikali.
“Tuelewe kuwa aliyeuliwa ni askari polisi, ni raia wa Tanzania ni lazima tuhakikishe waliofanya unyama huu wanakamatwa na kupelekwa mbele ya vyombo vya kisheria,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vyengine vya ulinzi na usalama vitaendelea ili kuhakikisha amani inarejea.
Alisema chimbuko la vurugu hizo limetokana na viongozi wa Uamsho kulalamika kuwa kiongozi wao, Sheikh Faridi Hadi, amekamatwa wakati siyo kweli.
Alisema polisi baada ya kupokea taarifa ya kutoweka kiongozi huyo walianza uchunguzi kwa kushirikiana na viongozi wa Jumuiya hiyo ikiwamo kumuhoji dereva wake, Said Omar Said, kabla ya kutokea kwa vurugu hizo. Kamishina Mussa alisema baada ya dereva huyo kuhojiwa, alisema majira ya jioni walikwenda kununua umeme katika kituo cha Mazizini.
“Sheikhe Farid alimuamuru dereva wake amuache eneo hilo ili azungumze na watu aliowakuta na kumtaka apeleke umeme nyumbani, aliporudi kutoka nyumbani kwake hakumkuta katika eneo alilomwacha,” alisema Kamishina Mussa nakuogeza: “Polisi kamwe hatuhusiki na kutoweka kwa kiongozi huyo.”
Alisema viongozi wa Uamsho walipeleka taarifa siku ya pili yake majira ya saa 6:30 mchana wakati wafuasi wao wakikusanyika na kuanza vurugu.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limefanikiwa kufungua barabara kuu ya kuingia katikati ya mji wa Zanzibar baada ya kufungwa kwa matangi ya chuma ya kuhifadhia mafuta.
Askari wa FFU walifanikiwa kuyaondoa matangi mawili, mawe na miti mikubwa majira ya saa 7:45 usiku katika eneo la Bububu kwa kutumia gari maalum la kunyanyua vitu vizito.
Magari manne yakiwa na askari wa FFU yenye namba PT 2086, PT 0954 na PT 0920 yalitumika kuimarisha ulinzi wakati wa kuondoa vizuizi hivyo juzi usiku.
Matangi makubwa ya kuhifadhi mafuta yalipakiwa katika gari aina ya Scania tani saba na kwenda kuhifadhiwa katika kituo cha Polisi Bububu.
Askari baada ya kufika katika eneo hilo walipokea taarifa za askari wa FFU kucharangwa mapanga na kutupwa katika mtaro mita chache kutoka barabarani.
Askari huyo alifariki kabla ya kufikishwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja majira ya saa 8:21 usiku.
Daktari bingwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk. Msafiri Marijani, alisema alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi kufuatia majeraha ya kichwani.
KANISA LASHAMBULIWA
Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar lilivamiwa na wafuasi wanaoaminika kuwa ni wa kundi la Uamsho na kusababisha uharibifu wa mali ikiwamo kuvunjwa vioo na madirisha kung’olewa.
Mchungaji wa Kanisa hilo, Emmanuel Masoud, alisema wafuasi wa Uamsho walilivamia kanisa hilo na kulishambulia kwa mawe.
Alisema walipokea taarifa kutoka kwa msamaria mwema juu ya kuwapo kwa mpango wa kuvamiwa kwa kanisa hilo na kulazimika kuomba msaada wa ulinzi kutoka kituo cha Polisi Malindi bila ya mafanikio.
“Kumefanyika uharibifu mkubwa wa mali za kanisa letu, wamevunja vioo na madirisha, hatujui nini tena kitafuta baada ya uharamia huu kupita,” alisema Mchungaji huyo. “Zanzibar tunasema ni kisiwa cha amani, mwenye kutaka na aje leo, kimekuwa kisiwa cha vurugu, ni mambo ya kusikitisha,” alisema.
WATALII WAONDOLEWA
Mchungaji Masoud alisema wakati wa vurugu hizo zinatokea makundi ya watalii kutoka Italia na Uingereza walikuwa wakitembelea eneo hilo la historia ya biashara ya utumwa na kulazimika kuwaondoa haraka kabla hawajashambuliwa kwa mawe. Alisema watu waliokuwa wakirusha mawe walifanya jaribio la kulichoma moto kanisa bila mafanikio.
WAJUMBE WA CCM WASUSIA BARAZA
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana waligoma kuingia Barazani wakishinikiza serikali kuchukua hatua dhidi ya wafuasi wa Uamsho kufutia vurugu hizo.
Kiongozi wa Wawakiklishi hao, Hamza Hassan Juma, alisema wameamua kuitisha mgomo huo kutokana na matukio ya kutisha yanayoendelea kutishia amani ya visiwani humo.
Wawakilishi hao walitoa maazimio matatu juu ya msimamo wao likiwamo kumtaka Waziri wa Sheria na Katiba, Abubakary Khamis Bakary, kuifutia usajili Jumiki kutokana kufanyakazi za kisiasa badala ya kazi za kiroho.
Walisema Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema na Kamishina wa Polisi Zanzibar wajiuzulu kutokana na kushindwa kulinda usalama wa raia na mali zao na kutochukua hatua za kisheria dhidi ya watu waliohusika na mauaji ya askari Polisi.
“Serikari ya Zanzibar itumie vikosi vyake kunusuru kushamiri vita vya wenyewe kwa wenyewe isitokee Zanzibar,” alisema Mwakilishi huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi.
Alisema Serikali ya Zanzibar na ya Muungano zinatakiwa kufanya uchunguzi wa kina kujua chimbuko la Uamsho na vurugu zinazoendelea kujitokeza visiwani.
Alisema katika kipindi cha miezi sita tayari matukio matano ya vurugu za Uamsho yametokea na kusababisha uharibifu wa mali na makanisa kuporwa na kuchomwa moto.
Alisema wananchi wamekuwa wakiishi Zanzibar bila ya amani kutokana na vitendo uharibifu wa mali na kudhalilishwa kutokana na hisia za ukabila na udini.
HOJA BARAZANI LEO
Hamza alisema baada ya Wajumbe kutafakari matukio hayo, leo watawasilisha hoja ili wajumbe wapate nafasi ya kujadili matukio ya vurugu zinayoendelea kujitokeza visiwani.
WA CUF WASHANGAA
Hata hivyo, Mnadhimu wa wajumbe wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdalla Juma Abdallah, alisema haikuwa hatua mwafaka kwa Wawakilishi wa CCM kususia Baraza wakati ni Wawakilishi wa wananchi.
Abdallah alisema wawakilishi wa CUF kupitia Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake, Ali Omar Shehe, alitoa hoja ya kutaka Baraza kusitisha shughuli zake ili kujadili matukio yaliyojitokeza, kushamiri kwa vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani.
Alisema wamesikitishwa na kitendo cha askari kuuawa bila hatia na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika. Alisema wakati umefika kwa serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha wafuasi wa Uamsho kufanya vurugu na kutafuta ufumbuzi.
SPIKA AJIWEKA KANDO
Spika Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alikataa kuzungumza chochote juu ya mgomo wa wajumbe wa CCM.
“Mie sina taarifa yoyote juu ya mgomo wao naomba waulizeni wenyewe,” alisema Kificho alipotakiwa kutoa msimamo wake.
Hata hivyo, alisema kwamba amesikitishwa sana na vitendo vya vurugu vinavyoendelea kutokea na kuvuruga matunda ya amani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema mabadiliko ya 10 ya Katiba yalifanyika ili kujenga msingi wa amani ambayo ndiyo yaliruhusu muundo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini kumeibuka watu ambao wameamua kuyaharibu mafanikio hayo. “Haya ni matukio mabaya katika mwelekeo wa kujenga misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, naomba wananchi wajiepushe kushiriki katika vitendo hivi haramu,” alisema Kificho.
Hata hivyo, pamoja na wajumbe wa CCM kususia kikao, Spika Kificho aliamuru shughuli za Baraza kuendelea huku wakihudhuria mawaziri na manaibu mawaziri pamoja na wajumbe wa CUF.
UKIMYA WATAWALA ZANZIBAR
Mji wa Zanzibar jana ulitawaliwa na ukimya kufuatia vurugu zilizotokea na askari wa FFU kulazimika kutumia mabomu ya machozi.
Vurugu hizo zilianzia katika msikiti wa Mbuyuni baada ya wafuasi wa Uamsho kukusanyika na kuanza kusonga mbele huku wakiituhumu Serikali kuwa imemkamata kiongozi wao.
PONDA KIZIMBANI
Sheikh Ponda Issa Ponda (54) na wenzake 49 walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka matano.
Mashitaka hayo ni kula njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai, wizi wa mali ya Sh. milioni 59.6 na sheikh huyo kufanya uchochezi wa kuhamasisha wafuasi wake kutenda makosa.
Washtakiwa hao walifikishwa katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana kati ya saa 5:30 asubuhi na saa 6:20 mchana wakiwa kwenye magari tofauti chini ya ulinzi mkali wa zaidi ya askari polisi 50.
Viunga vya mahakama hiyo vilifurika watu waliodhaniwa kuwa ni wanafamilia na wafuasi wa Sheikh Ponda ambaye ni mwalimu wa madrasa Ubungo Kibangu, jijini Dar es Salaam kwa ajili kusikiliza mwenendo wa kesi hiyo.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Stuwart Sanga, baada ya Hakimu Victoria Nongwa aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru wa kikazi.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, akisaidiana na Zuberi Mkakatu, uliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Kuluthumu Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma Mpanga, Farida Lukoko, Adamu Makilika, Athum Salim, Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.
Wengine ni Halima Abbas, Maua Mdumila, Fatihiya Habibu, Hussein Ally, Shaban Ramadhani, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhani, Yusuph Penza na Alawi Alawi. Wengine ni Ramadhani Mlali, Omary Ismaili, Salma Abduratifu, Khalidi Abdallah, Said Rashid, Feswali Bakari, Issa Wahabu, Ally Mohamed, Mohamed Ramadhani, Abdallah Senza, Juma Hassani na Mwanaomary Makuka.
Kweka aliwataja wengine kuwa ni Omary Bakari, Rashid Ndimbu, Hamza Ramadhani, Ayubu Juma, Maulid Namdeka, Farahan Jamal na Smalehes Mdulidi. Wamo pia Jumanne Mussa, Salum Mohamed, Hamis Halidi, Dite Bilali, Amiri Said, Juma Yassin, Athuman Rashid, Rukia Yusuph, Abubakari Juma na Ally Salehe.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa katika shtaka la kwanza Oktoba 12, mwaka huu huko Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walikula njama ya kutenda makosa.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, eneo la Chang’ombe Markas, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja mali ya Agritanza Ltd.
Katika shitaka la tatu, Kweka alidai kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang’ombe Markas, washtakiwa hao walijimilikisha ardhi ambayo ni mali ya Agritanza Ltd.
Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang’ombe Markas, washtakiwa wote waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 59,650,000, mali ya Agritanza Ltd.
Wakili huyo mwandamizi alidai kuwa katika shtaka la tano linamkabili Sheikh Ponda peke yake, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu Chang’ombe Markas, mshtakiwa akiwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya jinai.
Washtakiwa wote walikana mashtaka dhidi yao.
Wakili Kweka alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), amewasilisha hati ya kiapo ya kuzuia dhamana ya Sheikh Ponda kwa madai ya usalama wake na maslahi ya Taifa.
Pia, aliomba mahakama kwa kuzingatia mazingira ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa mahakama ijielekeze kutoa masharti ya dhamana ambayo yatawazuia washtakiwa kutorudia makosa hayo.
Hata hivyo, wakili wa utetezi Nassoro Juma alidai kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa wote yana dhamana na kwamba hata kiapo kilichowasilishwa na DPP hakijafafanua kuhusu kuzuia dhamana ya mshtakiwa wa kwanza kwa usalama gani na maslahi yapi.
Hakimu Sanga alisema kwa kuwa hakimu aliyepangiwa kesi hiyo ana udhuru wa kikazi, kesi hiyo itatajwa na kutolewa masharti ya dhamana Novemba Mosi, mwaka huu.
HALI ILIVYOKUWA MAHAKAMANI
Jana askari polisi waliokuwa na sare pamoja na askari kanzu walifurika mahakamani hapo na kulazimika kuwadhibiti mamia ya watu waliokuwa wamefurika nje ya ukumbi namba moja wa mahakama hiyo kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na ukumbi huo kuwa mdogo kuliko uwingi wa watu na walitii amri na kwenda nje ya jengo la mahakama kusubiri kesi kusikilizwa.
Baada ya kusikilizwa na kupangwa tarehe ya kutajwa tena, askari wengine zaidi ya 15 wa usalama barabarani walitanda katika viunga vya mahakama kwa ajili ya kupanga na kuongoza msafara wa magari yaliyokuwa yakisindikiza msafara huo uliokuwa na mabasi matatu yaliyowabeba washtakiwa hao.
MAASKOFU WATOA TAMKO ZITO
Maaskofu wa Dayosisi 20 za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wakiongozwa na Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Alex Malasusa, wamekutana na kutoa tamko kali kuhusiana na tukio la kuchomwa makanisa lililotokea Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza jana baada ya ibada ya pamoja iliyofanyika katika Usharika wa KKKT Mbagala, walihoja kitendo cha serikali kutoonyesha umakini katika kushughulikia matukio ya uvunjivu wa amani ambayo yameanza kujitokeza nchini vinavyofanywa na watu wanaojiita wanaharakati wa dini.
Walisema: “Katika majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa. Majibu haya na machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya itakayojali upendo, uvumilivu, ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa kuabudu na dola isiyo na dini,”
Maaskofu hao pia walisema: “Tumefikia kuhoji watu hawa wavamie nini ndipo hatua zuichukuliwe, wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke, wamuue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama wa Taifa letu.”
Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari, Askofu KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, kwa niaba ya maaskofu wote wa kanisa hilo, alisema: “Kwa macho na masikio yetu tumeendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala.”
Alisema wakati wote uvumilivu wa Wakristo huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga, lakini huwa inafika wakati wanyonge na waoga hufikia wakati wakasema sasa basi pale wanapodhalilishwa kupita kiasi, jambo ambalo Wakristo hawataki ifike hapo.
Askofu Shao alisema katika hali ya kushangaza, watu wanaofanya vitendo hivyo vya kusikitisha wametunukiwa hadhi ya kuitwa kuwa ni wanaharakati tofauti na wanaharakati wanaotambuliwa na Watanzania walio wengi.
“Tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote kuwa uanaharakati wao wasitumike kuvunja nchi na sheria za nchi, Tanzania yenye amani na mshikamano ni tunda la dini zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi, hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii,” alisema.
Alisema kitendo kikichotokea Mbagala cha kuchoma makanisa katika wiki ya kuadhimisha siku ya Baba wa Taifa ni kebehi si kwa Baba wa Taifa, bali pia kwa wanaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa.
Askofu Shao alisema kilichotokea Mbagala ni mateso ya kimbari ambayo ni matokeo ya mbegu ya magugu iliyopandwa katika bustani njema na sasa magugu hayo yanazaa matunda machungu.
“Dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya kanisa zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa Taifa, dalili hizo ni pamoja na uchochezi wa wazi kuwa Taifa hili linaendeshwa na unaoitwa mfumo wa Kristo na kuwa Baba wa Taifa alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa hili,” alisema.
Aliongeza kuwa dalili nyingine ni ubishi usiyo na tija juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali nchini, matumizi mabaya ya baadhi ya vyombo vya habari vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko ya kidini miongoni mwa Watanzania.
Alisema madai yasiyo ya kawaida ya mara kwa mara kwa serikali inayodaiwa kutokuwa na dini ambayo ni kulazimisha uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na kuratibisha tofauti za Watanzania.
“Tunajiuliza likitokea la Mbagala katika mashule yetu na vyuo vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa wangapi, pia yapo madai na mashinikizo ya uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini, madai ya kutaka balozi za nchi fulani kufungwa hapa nchini na mashinikizo ya kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria,” alisema Dk. Shao.
Askofu Shao alisema viongozi wa dini zote walioitwa kwa njia ya nadhiri na viapo vitakatifu waendelee kuwasihi waumini wa dini zote na Watanzania kwa ujumla wenye wajibu wa kutii viongozi wa dini na wasiolazimika kutii wazingatie kuwa Mwenyezi Mungu analipenda Taifa hili na watu wake hivyo wasiache likaangamia.
Aliongeza kuwa kwa Wakristo huu ni wakati wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya Taifa hasa kwa kuzingatia kuwa Mkristo wa kweli ni yule aliye tayari kuteswa kwa ajili ya Yesu Kristo na Kanisa.
“Wakristo hatuko tayari kuua, kutesa, kulipiza kisasi ili kumtetea Mkristo, Mungu wetu hatetewi kwa kuua wengine na kuchoma madhabahu ya dini nyingine. Katika mateso haya, kanisa litaimarika zaidi na katika majivu haya ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana,” alisema.
Askofu Shao alisema Wakristo waendelee kusamehe na kuwa raia wema sambamba na kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa.
“Wakati wengine wanaweka mikakati ya kuchoma madhabahu, Wakristo tuweke mikakati ya kuomba na kushiriki vema katika haki zetu za uraia pamoja na kuwa wapole kama njiwa, imetupasa pia kuwa na busara kama nyoka (Mathayo 10:16),” sehemu ya tamko hilo ilisema.
Kwa upande wake, Kiongozi wa KKKT na Asakfu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, aliwasihi Wakristo kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na kutoshiriki katika kulipiza kisasi.
Maaskofu waliotoa tamko hilo mbali na Dk. Malasusa na Dk. Shao na dayosisi zao kwenye mabano ni Dk. Stephen Munga (Kaskazini Mashariki); Dk. Thomas Laizer (Kaskazini Kati); Dk. Benson Bagonza (Karagwe); Isaya J. Mengele (Kusini); Levis Sanga (Kusini Kati); Elisa Buberwa (Kaskazini Magharibi) na Andrew Gulle (Mashariki ya Ziwa Victoria).
Wengine ni Michael Adam (Mkoani Mara); Renard Mtenji (Ulanga-Kilombero); Dk. Israel-Peter Mwakyolile (Konde); Job Mbwilo (Kusini Magharibi); Dk. Owdenburg Mdegella- (Iringa); Jacob Ole Mameo- (Morogoro); Zebedayo Daudi (Mbulu); Paulo Akyoo (Meru); Charles Mjema (Pare); Askofu Mteule Amon Kinyunyu (Dodoma) na Askofu Mteule Dk. Alex Mkumbo- (Kati).
Oktoba 12, mwaka huu kulitokea vurugu eneo la Mbagala na watu wanaodhaniwa kuwa ni waumini wa dini ya Kiislamu walichoma makanisa kadhaa na kuharibu mali mbalimbali kutokana na kitendo cha mtoto mmoja kudaiwa kukojolea Kur’ani.
Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Zanzibar na Hellen Mwango na Thobias Mwanakatwe, Dar.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment