Sunday, September 23, 2012

JOGOO LIMEWIKA DODOMA




Mizengwe imetawala katika uchaguzi wa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM ) baada ya wagombea kuzibiana na makundi ya wazi wazi yakiendelea kukiandama chama hicho.
Hali imejitokeza huku Chama hicho kikitarajiwa kufanya mchujo wa majina ya wagombea kuanzia kesho na Jumanne
Habari za ndani ambazo NIPASHE imezinasa ni kuwa mgawanyiko ndani ya chama hicho umesababisha baadhi ya wagombea kuenguliwa na kuwekwa wagombea wengine.
Kutokana na makundi kukiandama chama hicho, baadhi ya mikoa wanachama wanadaiwa kutishwa kuchukua fomu ili kutoa nafasi kwa wagombea wanaowataka wao.
Habari zaidi kutoka Wilaya ya Nzega, zinaeleza kuwa imeibuka hoja kwamba wagombea wote kutoka wilaya hiyo, Saidi Kigwangala na Hussein Bashe, waondolewe kwenye kinyang’anyiro hicho.
Sababu zilizoelezwa za kuondolewa kwa wagombea hao ni kutokana na Kigwangala kukutwa na tuhuma za kutishia kwa bastola katika zoezi la kurudisha fomu za kuwania nafasi hiyo.
Kwa upande mwingine, zengwe lililoibuka ni kuwa Bashe amekuwa akitoa taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari kuhusu chama hicho na kudaiwa kutokubaliana na dhana ya kujivua gamba na pia kutuhumiwa kuwa mzee wa kuunda makundi.
Wakati maamuzi hayo yakifanyika, Kamati ya Usalama na Maadili ya wilaya hiyo imemtia hatiani Kigwangallah kwa kukutwa na bastola na kuwekwa chini ya uangalizi kwa muda wa miezi 12.
Kamati hiyo, ilimchunguza Kigwangallah baada ya madai ya kumtishia Bashe kwa bastola wakati wakiwa kwenye zoezi la kurudisha fomu za kuwania nafasi hiyo.
Habari za ndani kutoka wilayani humo zinasema taarifa za kamati hiyo kuhusu uchunguzi juu ya tuhuma dhidi ya Dk. Kigwangallah zilipelekwa mkoani lakini katika hali ya kushangaza waliikalia bila kusema uchunguzi ulibaini nini.
Wakati maamuzi hayo yakifanyika, kuna taarifa kuwa mkakati huo wa kuwaengua wagombea hao ni wa kumharibia mtu sifa kama hofu ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Chanzo chetu cha habari kimeliambia gazeti hili kuwa wagombea walioteuliwa kuwania nafasi hiyo badala ya Dk.Kigwangallah na Bashe ni Majaliwa Bilali, Yasin Memba na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Msigalo.
Habari zaidi zinaeleza kuwa wagombea wengine walioenguliwa katika uchaguzi huo ni Naibu Waziri wa Habari na Michezo na Mbunge wa Mvomero, Amos Makalla na Said Sadik .
Chanzo chetu kimesema kuwa Sadik ameondolewa kwa sababu anawania nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha katika wilaya hiyo na Makalla, amewekwa kwenye kapu (kundi la kifo).
Katika Wilaya ya Monduli, idadi ya wagombea imeongezwa na kufika watatu baada ya wajumbe kuhoji kwa nini wagombea wawe wawili. Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Dk. Toure, ndio waliokuwa wakiwania nafasi hiyo. Hoja hiyo ilisababisha mgombea mwingine kuingizwa aliyetambulika kama, Nanai Kaoni.
Katika kuonyesha kuwa uchaguzi huo umejaa mizengwe, mzozo mwingine uliibuka baada ya wajumbe kuhoji iweje Wilaya ya Bariadi kuwe na mgombea mmoja aliyepitishwa bila kupingwa, jina la Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Chenge, kugombea nafasi hiyo.
Aidha, wajumbe hao walihoji mkoa wa Simiyu kutokuwa na mgombea. Habari kutoka katika mkoa wa Simiyu kwenda kwa Sekretarieti ya Chama, zimedai kuwa wanachama wanatishwa kujitokeza kuchukua fomu za kuwania ujumbe huo. Habari zaidi zimedai kuwa mzozo ulikuwa mkubwa huku wajumbe wakitaka watangaze wagombea wa nafasi hiyo upya.
Wakati harakati hizo zikiendelea, kutoka Wilaya ya Hanang, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu, amewekewa zengwe ili atemwe kwenye nafasi hiyo kwa madai kuwa ana nafasi nyingi katika chama na serikali. Dk Nagu anapambana na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Hata hivyo, wakati zengwe hilo likiwekwa, Jenister Muhagama ambaye ni Katibu wa Wabunge wa CCM anaelezwa aliwahi kumwandikia Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, kumuuliza kimaandishi kama Wabunge hawaruhusiwi kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa Mukama alimjibu Mhagama kimaandishi kuwa hakuna kitu kama hicho.
NAPE: MCHUJO MKALI SASA KUJULIKANA JUMANNE
HATMA ya mawaziri na vigogo wengine wenye nyazifa zaidi ya moja serikalini na ndani ya chama ambao waliomba kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), itategemea busara za vikao vya Kamati Kuu (CC) vilivyoanza jana mjini hapa.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Makao Makuu ya Chama hicho mjini Dodoma.

Nape alisema Kamati Kuu imekuwa ikitumia busara katika kupitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali kwa maslahi ya chama.

“Hata kanuni inasema kuwa anaweza kugombea kwa kibali maalum cha Kamati Kuu. Majina yanapofika tunasema huyu ni mbunge, tunaangalia je anafaa tena kugombea nafasi nyingine inaporidhika basi inatoa kibali kwa mtu kuwania nafasi ya uongozi,” alisema.

Alisema CC imeawahi kuruhusu na kukataa maombi ya watu mbalimbali kwa hivyo hilo halitakuwa jambo geni kama litatokea katika vikao vinavyoendelea.

Alitoa mfano wa kanuni inayomkataza mtu kutoka chama cha upinzani kupewa fursa ya kugombea ikiwa hajatimiza miaka mitano ndani ya chama hicho lakini Danhy Makanga aliyehamia CCM akitokea chama cha upinzani cha UDP aliwahi kupatiwa nafasi mara tu baada ya kujiunga na chama hicho tawala.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wajumbe wa NEC kuwaonea aibu wenzao walio omba nafasi za uongozi kwa kuwapa kura, Nape alisema ni vigumu kwa wajumbe kuwaonea aibu wajumbe wenzao walioomba nafasi za uongozi na kwamba atakayechaguliwa kugombea atakuwa ana sifa zinazotakiwa.
“Mtakumbuka Gachuma na Chambiri mwaka 2007 waliwahi kugombana huko Mara, walipokuja katika vikao tukasema hawa wote hawafai, wanaosema kuwa wajumbe wa Nec

 ( Halmashauri Kuu) wanaweza kushawishiwa na wajumbe wenzao hawajui jinsi vikao hivi vinavyofanya kazi,” alisema.
Vikao vya CC vilitarajiwa kuanza jana na kumalizika leo ambapo vikao vya NEC vimepangwa kuanza Jumatatu na kumalizika Jumanne ambapo agenda kuu itakuwa ni kuchuja majina ya wanachama walio omba kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Kuchelewa kuanza kwa kikao hicho ambacho awali kilipangwa kuanza saa 4 asubuhi jana, kumetokana na kuchelewa kumalizika kwa Kamati ya Maadili ya chama jana.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment